Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba amevitaka vyama vya siasa kuzingatia matakwa ya wananchi katika suala zima la Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na badala ya kuwagawa.
Aidha,
Warioba amesema anaamini baadhi ya vipengele vilivyokataliwa katika
Rasimu ya Katiba, ipo siku vitafanyiwa kazi kuondoa migongano huku
akisisitiza, kisheria kura ya maoni siyo mwisho wa mchakato.
Warioba
alisema kwa sasa, badala ya kuwaweka wananchi pamoja na kukubaliana
wanachotaka , upo mvutano huku wengine wakitaka Katiba Iliyopendekezwa
ikubaliwe na wengine wakitaka wananchi waikatae.
“Kwa
suala hili la kundi la Ukawa kuwasihi wafuasi wake kutoshiriki katika
upigaji kura ya maoni, inaonyesha dhahiri hakuna maridhiano na wananchi
kwani badala ya kujua matakwa yao, vyama vya siasa vinawagawa wananchi
katika suala hilo jambo ambalo linaonyesha vyama hivyo vinajitazama
vyenyewe,” alisema.
Alikuwa akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Alisema
suala la kupiga kura ya maoni ni kuangalia maridhiano na wananchi na si
vyama vya siasa. Alisema hata katika mchakato wa awali, waliangalia
maridhiano ya wananchi na walihakikisha maoni yao yanaingia kwenye
Katiba pendekezwa.
Alisema vyama vya siasa vinataka maridhiano yao bila kuangalia matakwa ya wananchi na kukubaliana jambo, alilosema ni tatizo.
Alisisitiza kwamba anaamini baadhi ya vipengele vilivyokataliwa, ipo siku vitafanyiwa kazi kuondoa migongano.
Alisema
katika Katiba Inayopendekezwa, suala la mgawanyo wa madaraka
halijaainishwa lakini anavyoona maendeleo katika dunia na matatizo, ipo
siku lazima madaraka yatenganishwe, kwani kutakuwa na migongano kati ya
Serikali na Bunge.
Alisema
ingawa masuala hayo hayajaingizwa katika Katiba Inayopendekezwa, kama
ilivyokuwa kwenye rasimu iliyoandaliwa na Tume aliyokuwa akiiongoza,
anaamini kutakuwa na mabadiliko kabla ya kura ya maoni au baada kwa kuwa
hayaepukiki.
“Matatizo
haya ya wazi ya masuala kama ya mgongano wa madaraka na Muungano
yatafanywa kabla au baada ya kura ya maoni kwani kuna mambo katika
Katiba pendekezwa hayawezi kutekelezwa na hayazungumziki,” alisema.
Akizungumzia
suala la maadili,Warioba alisema sheria ya maadili ipo, lakini haina
nguvu kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine. Alitoa mfano wa Ufilipino
akisema walikuwa na sheria hiyo lakini wakaweka kwenye katiba iwe rahisi
kutekelezwa. Alitaja pia Namibia na Kenya.
Alisema
suala la mgawanyo wa madaraka bado ni muhimu kwani kwa kutenganisha,
kunaweza kusaidia katika uwajibikaji . Alitoa mfano wa sakata la Tegeta
Escrow bungeni na kusema Bunge na Serikali ziliingiliana madaraka
badala ya serikali kuwa na kauli moja.
“Hebu
angalia suala la Bunge kumfukuza Katibu Mkuu, hii siyo kazi yake,
lilichanganya madaraka, kama Bunge haliridhiki na mwenendo wa serikali
haliwezi kwenda kufukuza watumishi wa serikali. Bunge linatakiwa kusema
kutokuwa na imani na serikali na siyo kufurahia kusema fulani afukuzwe.
Siyo utaratibu mzuri,” alisema.
Waziri
Mkuu huyo mstaafu alisema kazi ya Bunge ni kusimamia serikali na siyo
kufukuza watu, kwani wakati mwingine kunakuwa na suala la visasi na
kufukuza watumishi ambao hawahusiki.
Kuhusu Muungano, alisema, “Hili
jambo ni ‘serious’(nyeti) lazima kufika wakati kuwa na nchi moja na
hata kuangalia jinsi ya kuweka sawa suala la muundo wa serikali.”
Alisisitiza
msimamo wake kwamba yeye ni muumini wa Muundo wa serikali mbili kwenda
moja na siyo muumini wa serikali tatu. Alipendekeza kwenda hatua kwa
hatua hata baada ya miaka 100 kupata serikali moja.
Warioba
alisema siku ya kupiga kura ya maoni, inaweza kubadilishwa kwani
haiko kisheria na haitaathiri mchakato wa kupata Katiba mpya.