HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ametimiza ahadi yake aliyoitoa Agosti mwaka jana katika Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, kwamba amekusudia kufuta ada ya shule za sekondari nchi nzima.
Akizindua
Sera mpya ya Elimu na Mafunzo 2014 katika Shule ya Sekondari ya Majani
ya Chai, Kipawa jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alitangaza
kufutwa kwa ada ya sekondari, kuanzia mwakani.
Kwa
tangazo hilo, Bajeti ya mwisho ya uongozi wa Rais Kikwete itakayoanza
kujadiliwa Mei mwaka huu, itatakiwa kuwa na fungu la kulipa gharama
ambazo wananchi wamekuwa wakitoa kwa watoto wao wanaosoma elimu ya
sekondari katika shule za Serikali nchi nzima.
Kwa
sasa wazazi wamekuwa wakilipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na Sh 70,000
kwa shule za bweni, ili watoto wao wapate elimu ya sekondari.
Ubora
Alisema
sera hiyo imezingatia stadi za msingi ambazo ni kuandika, kusoma na
kuhesabu, ili kuwezesha watoto kujengwa kwenye msingi mzuri na hata
kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hilo limezingatiwa.
“Hata
kwenye mpango wa BRN tumelizungumza ili kuhakikisha inatolewa elimu
bora. Tusifanye mambo ya kuchekesha mtoto anafika madarasa ya juu hajui
kuandika, kusoma na kuhesabu.
“Kuanzia
sasa kama mtoto anafika darasa la pili, hajui kusoma, kuandika na
kuhesabu (KKK), ni bora asiende darasa la tatu…naamini watoto
wakiimarishwa katika stadi za KKK itaondoa matatizo haya,” alisema.
Tathimini
ya Msingi ya Taifa kwa ajili ya uwezo wa wanafunzi katika KKK, kwa
wanafunzi wa Darasa la Pili iliyofanyika mwaka jana, ilibaini kuwa
asilimia 98 ya wanafunzi wa Darasa la Pili nchini, walikuwa hawaelewi
wanachokisoma.
Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema, tathimini
hiyo imefanywa kwa baraka za Wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la
Misaada la Marekani (USAID), ili kupata taarifa kuhusu hali halisi
ilivyo ya wanafunzi wa Tanzania kumudu stadi za KKK wanapofika Darasa la
Pili.
Mafanikio
Mbali
na mafanikio ya kufikia uwezo wa kuanza kutoa elimu ya msingi na
sekondari bure, huku msisitizo ukiwekwa katika utoaji wa elimu bora,
Rais Kikwete pia ilitangaza mafanikio mengine katika sekta ya elimu
ambayo yamefikiwa katika uongozi wake wa miaka kumi.
Rais
Kikwete alisema sasa elimu imepewa kipaumbele katika sera na shughuli
za serikali, ndio maana Bajeti ya Elimu, ndio kubwa kuliko bajeti zote.
Alifafanua kuwa mwaka 2005/06 bajeti hiyo ilikuwa Sh bilioni 6.7, wakati mwaka huu wa fedha imepanda na kufikia Sh trilioni 3.1.
Hatua
hiyo ya kibajeti kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni ongezeko la mara tano
ya Bajeti ya mwaka 2005 sawa na asilimia 20 ya Bajeti ya Serikali ambayo
inatengwa kwa ajili ya elimu.
Katika
suala la mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu, Rais Kikwete
alisema imetoka Sh bilioni 56 kwa mwaka wa fedha 2005/06, hadi kufikia
Sh bilioni 345 kwa mwaka huu wa fedha.
Aidha,
kwa mwaka jana, wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu,
waliongezeka kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000.
Kwa
upande wa shule za msingi, alisema zimeongezeka kutoka 14,000 kwa mwaka
2005 hadi kufikia shule 16,343 kwa mwaka 2014, huku shule za sekondari
zikiongezeka kutoka 531 kwa mwaka 2005, hadi kufikia 4,576, mwaka 2014.
Idadi
wanafunzi wanaojiunga na sekondari, Rais Kikwete alisema imeongezeka
kutoka wanafunzi 524,325 mwaka 2005 na kufikia wanafunzi milioni 1.8.
Rais
Kikwete alisema pia vyuo vya ufundi vimeongezeka kutoka vyuo 184 mwaka
2005 na kufikia vyuo 744 kwa mwaka 2014, huku vyuo vikuu vikiongezeka
kutoka vyuo vikuu 26 mwaka 2005 na kufikia vyuo vikuu 50 kwa mwaka 2014.
Alikumbusha kuwa kama sio kuanzishwa kwa shule za kata, idadi ya wanafunzi pia isingeongezeka.