KUSHUKA kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hakujawapa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) unafuu wa kuwafanya washushe bei ya umeme.
Aidha,
serikali imesema haifumbii macho suala hilo na imeziagiza Mamlaka
husika za Tanesco na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA),
kuangalia inapotokea fursa, ili iweze kwenda kwa wananchi.
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alisema hayo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Athumani Mfutakamba (CCM), aliyetaka
kufahamu sababu za kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Alihoji,
kutokana na anguko hilo kwa nini gharama mbalimbali, ikiwemo bei ya
umeme unaozalishwa na TANESCO, IPTL, Aggreko, Symbion haujashuka wakati
mafuta yameshuka bei.
Akijibu
swali hilo, Mwijage alisema uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini
kwa sasa ni MW 1,226.24 ,mitambo ya kufua umeme kwa maji inazalisha MW
561.84, gesi MW441, na mafuta MW 223.40.
Alisema
kampuni za IPTL na Aggreko zinaiuzia Tanesco umeme kwa senti za
Marekani 28 hadi 40 kwa uniti wakati Tanesco inawauzia wananchi umeme
kwa senti za Marekani 16.4 kwa uniti.
“Kwa
kuangalia takwimu hizo, ni dhahiri kuwa Tanesco inanunua umeme kwa bei
juu kuliko inavyowauzia wananchi, hivyo kushuka kwa bei ya mafuta katika
soko la dunia hakujawapa nafuu wa kufanya washushe bei,” alisema Mwijage.