Askari wa Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo la Mzinga, Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ya Temeke.
Akizungumza
kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa kwenye doria kwa kutumia
pikipiki maarufu kama Tigo na walipofika eneo la Mzinga walimkamata
dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa kwenye pikipiki yake.
“Polisi
walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika kwamba alikuwa na
makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva wenzake
walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa askari kwa
kumpiga chupa usoni,” alisema Kihenya.
Aliongeza kuwa “Tumekamata
bodaboda kumi na tano na tayari tunaendelea na uchunguzi ili kuweza
kubaini wahusika wakuu na tuweze kuwafikisha mahakamani kwa kosa la
shambulio,” alieleza.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema fujo hizo zilikuwa kubwa kiasi kwamba polisi
walilazimika kuwatawanya washambuliaji kwa kupiga risasi za moto hewani.
“Mimi
nilifunga duka nikakimbia maana kulikuwa hakukaliki hapa, walipompiga
yule askari, uso wote ulitapakaa damu ndipo wakarusha risasi hewani.
Kila mtu alikimbilia anakojua mwenyewe,” alisema moja wa mashuhuda aliyeogopa kutajwa jina lake.
Kwa
upande wake, Sanja Justin, alisema yeye alikuwa ana safari ya kwenda
Mbagala na alipokaribia kituoni cha basi, alisikia mlio wa risasi na
kuamua kukimbia na kurudi nyumbani.
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.