NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Saturday, February 7, 2015

RIPOTI YA REPOA: Polisi Yaongoza kwa Rushwa.....TRA, Mahakama na TAKUKURU Nao Wamo


Baadhi ya watendaji wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), pamoja na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ni miongoni mwa watendaji wa taasisi nne ambao wametajwa katika utafiti kuwa wamekithiri kwa kupokea rushwa.

Takukuru na TRA zimetajwa kuwa na kadhia hiyo katika ripoti ya Taasisi ya Afro Barometer iliyofanywa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupunguza Umasikini (Repoa).
 
Kwenye  ripoti  hiyo, Polisi bado wanaongoza kwa kupokea rushwa wakifuatiwa na TRA, Mahakama na Takukuru inashika nafasi ya nne, jambo ambalo limewashitua watu wengi waliohudhuria kwenye mkutano huo.
 
Akiwasilisha ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya wadau mbalimbali, mtafiti wa Repoa, Rose Aiko alisema maofisa wa serikali za mitaa, maofisa serikalini na baadhi ya wabunge na wananchi wamewataja kuwa wanashiriki kwenye vitendo vya rushwa.
 
Ripoti hiyo imeeleza kuwa asilimia 67 ya watu waliohojiwa ambao ni 2,386 walikiri kuwa vitendo vya rushwa vimeongezeka kuanzia mwaka 2013 hadi 2014; licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali za kuajiri maofisa wengi wa kupambana na rushwa katika taasisi ya Takukuru.
 
“Habari kwamba rushwa imeongezeka, imeongelewa na watu wa kawaida mijini, wanaume, wasomi na wakazi wengi wa Zanzibar,” ilieleza ripoti hiyo.
 
Miongoni mwa walihojiwa, asilimia 50 waliitaja polisi kukithiri kwa rushwa, TRA (asilimia 37), Mahakama asilimia 36, Takukuru asilimia 29 wakati maofisa wa Serikali za mitaa ni asilimia 25.
 
Hata hivyo, utafiti huo umebaini kuwa miongoni mwa watu watatu ambao wanaenda kupata huduma Polisi na mahakamani, mmoja kati ya watu hao anadaiwa rushwa.
 
Mtazamo wa wananchi ambao ni asilimia 53, wanaona kwamba wananchi wa kawaida wanaweza kusaidia katika mapambano ya rushwa, huku asilimia 33 wakisema wananchi wa kawaida hawawezi. Pia utafiti huo ulibaini kuwa wananchi wengi hawatoi taarifa kwa mamlaka husika hata pale wanapodaiwa rushwa.
 
Watu wanane kati ya 10 ambao walihojiwa ambao tayari walishatoa rushwa, walikiri kuwa hawakutoa taarifa mahali popote licha ya kutoa rushwa. 
 
Pia utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 34 ya wahojiwa, walitoa rushwa wakati wanatafuta haki mahakamani na wengine asilimia 34 walitoa rushwa kwa kuepuka usumbufu wa Polisi.
 
Pia utafiti huo wa Repoa ulisisitiza kuwa, ili jamii iondokane na tatizo la rushwa, ni lazima watu wakatae kutoa rushwa na wengine wawaripoti kwenye mamlaka zinazohusika wale wote ambao wanawaomba rushwa.
 
Sababu ya watu kutoripoti matukio ya rushwa kwenye mamlaka zinazohusika, utafiti uliainisha kuwa ni mazingira magumu ya upatikanaji wa ushahidi kwa kuwa watuhumiwa wengi wamekuwa rahisi kukataa kuhusika na vitendo vya rushwa.
 
Pia mamlaka zinazohusika na kupambana na rushwa, zimetajwa kuwa ziko mbali, jambo ambalo linawafanya wengi wanaokutwa na janga la kuombwa rushwa, wasiripoti kwa kuepuka gharama za kwenda huko.
 
Pia utafiti huo ulibaini kuwa watu wanaamini bila kutoa rushwa, hawawezi kupata huduma na kwamba mtu ambaye amekusaidia baada ya kupewa rushwa sio vizuri kumripoti Takukuru.
 
“Kubwa hapa ni kwamba jamii haina uelewa wa kutosha kwa maana mtu anaamini kwamba hawezi kupata huduma wakati mwingine atakapokuwa na shida iwapo ataripoti tukio la rushwa Takukuru au Polisi,” alisema Rose.
 
Hata hivyo, wananchi wengi walipongeza vyombo ya habari kwa kuwa mstari wa mbele kutangaza vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya maofisa wa Serikali katika taasisi mbalimbali.
 
Naye Ofisa wa Takukuru, Mary Mosha alipochangia kuhusu ripoti hiyo, alisema Takukuru imekuwa na mpango mkakati   uliowahusisha wadau mbalimbali wa namna ya kuielimisha jamii ielewe juu ya madhara ya rushwa.
 
Alisema pia kuwa juhudi nyingi zimefanywa na Serikali kuziba mianya ya rushwa; “Bahati mbaya ni kwamba juhudi hazionekani na watu wanataka kuona watu wanapelekwa mahakamani."
 
Mosha aliwataka wadau wote kuendelea kushirikiana na Takukuru kupambana na rushwa na akasisitiza kuwa kuna mabadiliko miongoni mwajamii.
 
“Ila tu matukio kama haya ya Escrow wakati mwingine ndio yameifanya jamii ione kuwa tatizo hili bado ni kubwa,” alisema.
 
 Mkurugenzi wa Masuala ya Uchumi wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema kuitaja Takukuru ni kuwapa fursa viongozi wa taasisi hiyo kumulika watu wake ili taasisi hiyo isije ikapoteza imani miongoni mwa wananchi.
 
“Sisi ndio maana tumemwita hapa ofisa wa Takukuru na kuitaja kwenye utafiti sio jambo baya, tunataka kumwonesha kinachofanywa na watu wa ofisi yake na wachukue hatua kuanzia sasa,” alisema Mmari.
 
Lakini Dk Benson Bana, alikuwa na mtazamo tofauti kuwa utafiti huo ni mzuri lakini kuitaja Takukuru hadharani, kutakatisha watu tamaa.
 
“Watu wanajenga imani mbaya kwamba mwizi hawezi kumkamta mwizi mwenzake,” alisema Dk Bana.