Wanajeshi 6 wa JTK Waliotaka Kuandamana Wafikishwa Mahakamani Chini ya Ulinzi Mkali
Wahitimu sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko usio halali.
Washitakiwa
hao ni Mwenyekiti wa Umoja wa wahitimu hao George Mgoba, Makamu
Mwenyekiti Parali Kiwango, Katibu Linus Steven na wahitimu wengine
Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob Mang’wita.
Wote
walikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi yao.
Walifikishwa
mahakamani hapo asubuhi na kupandishwa kizimbani saa 10 kasoro jioni,
wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kufanya mkusanyiko usio
halali na kushawishi wenzao kutenda kosa la jinai.
Wakili
wa Serikali, Nassoro Katuga akisaidiwa na Tumaini Kweka, Hellen Moshi,
Janethroza Kitali na Inspekta Jackson Chidunda, alidai mbele ya Hakimu
Mkazi, Frank Moshi kuwa Februari 15 mwaka huu katika eneo la Msimbazi
Centre, Ilala Dar es Salaam, washitakiwa walipanga njama za kutenda
kosa.
Alidai
siku hiyo katika eneo hilo, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo
la kuandamana kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi
wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na lingesababisha uvunjifu
wa amani.
Katika
mashitaka yanayomkabili Mgoba, Kiwango na Steven, wanadaiwa siku hiyo
katika eneo hilo, walishawishi wahitimu wenzao wa mafunzo ya JKT,
kufanya maandamano kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika
utumishi wa umma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Walikana
mashitaka yanayowakabili na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi
haujakamilika. DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya
washitakiwa hao, chini ya kifungu cha 148 (4) cha Mwenendo wa Makosa ya
Jinai (CPA).
Hakimu
Moshi alisema washitakiwa watarudi rumande hadi Machi 6 kesi
itakapotajwa kwa kuwa DPP amefunga dhamana yao kwa muda mpaka atakapoona
inafaa, hivyo Mahakama haiwezi kutoa masharti ya dhamana.
Awali,
Makamu Mwenyekiti wa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT), Parali Kiwango (25) mkazi wa Temeke Mikoroshini
alijisalimisha Makao Makuu ya Polisi, kwa Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi.