Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma ACP Jafari Mohamed amesema, risasi
524 na bunduki moja ya kivita aina ya SMG zimekamatwa katika eneo la
kijiji cha Nduta baada ya polisi katika kizuizi cha Nduta kufanya
ukaguzi ndani ya basi.
Wakati kazi hiyo ikiendelea mtu anayesadikiwa kumiliki begi
lililokuwa na risasi na bunduki alitoroka, ambapo amesema vizuizi vya
barabarani vilivyowekwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kigoma
vimesaidia kukamata wahalifu na silaha zinazosafirishwa mara kwa mara.
Pia ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali wilayani Kibondo kwa kutoa pikipiki tatu kwa jeshi la polisi.
Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kibondo Venance Mwamoto,
ambaye amehamishiwa wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, amewataka wananchi
kutoa ushirikiano na kuisadia serikali kuimarisha ulinzi kwa kuwa jukumu
la ulinzi ni la wananchi wote.