SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake kupigwa na polisi, Rais Jakaya Kikwete amesema tukio hilo limetokea kwa sababu nchi inaongozwa kwa sheria na atakayekiuka atakumbana na mkono wa sheria.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo
ya faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, ambaye yuko
nchini kwa ziara ya siku tano.
Kabla ya Rais Kikwete kutoa kauli hiyo, Rais Gauck aliimwagia sifa
Tanzania kutokana na namna inavyofuata utawala wa sheria, uhuru wa
vyombo vya habari na kulinda haki za binadamu.
Baada ya viongozi hao kuzungumza mbele ya waandishi wa habari juu ya
ziara hiyo, waandishi walipewa fursa ya kuuliza maswali na ndipo mmoja
wa wanahabari kutoka Ujerumani, alipotaka kauli ya Rais Kikwete na Rais
Gauck, juu ya msingi wa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu
nchini, wakati hivi karibuni gazeti la The East African lilifungiwa na
wanachama wa CUF kupigwa na polisi walipotaka kuandamana.
Akijibu swali hilo, Rais Kikwete alisema: “Tuna sheria zinazoongoza
mambo hayo, huwezi kuamka tu ukaamua kuandamana, tuna taratibu zetu za
vyama vya siasa kukusanyika, wala hatubani haki na uhuru wa wapinzani,
ukivunja sheria hiyo utawajibishwa.
“Na hapa wapinzani ndio wanafanya mikutano mingi kuliko chama tawala,
ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha waendelee kuvunja
sheria,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Profesa Lipumba
alisema walifuata sheria zote na pia kutii amri ya polisi ya kuwataka
kuacha kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara.
CUF walipanga kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara kukumbuka wenzao waliouawa mwaka 2001.
Kuhusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la The East African
linalochapishwa nchini Kenya na Kampuni ya Nation Media Group (NMG) na
kusambazwa Tanzania, Rais Kikwete alisema halijafungiwa bali lilibainika
kusambazwa nchini bila kuwa na kibali.
Alisema baada ya kubainika hilo, kampuni inayochapisha gazeti hilo
ilitakiwa kutoendelea kulisambaza nchini hadi kibali cha kufanya hivyo
kitakapopatikana.
Rais Kikwete alisema kwa sasa utaratibu wa kutoa kibali hicho unaendelea.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinajali
uhuru wa vyombo vya habari, na hata sasa kuna magazeti mengi
yaliyosajiliwa na yanachapishwa kila siku.
Akizungumzia kuhusu hali ya usalama na tishio la ugaidi, Rais Kikwete
alisema hawezi kusema kuwa Tanzania iko salama asilimia 100, lakini
kutokana na hatua zinazochukuliwa za kulinda amani na usalama, hali iko
shwari.
“Tunashirikiana vizuri na vyombo vya usalama vya kimataifa,
tunadabilishana taarifa kila inapobidi, siwezi kusema kuwa sisi tuko
salama kwa asilimia 100, kwamba hatuwezi kuguswa kutokana na mikakati ya
kulinda amani, hali kwetu ipo shwari,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliiomba Ujerumani kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini, ikiwamo gesi, viwanda na biashara.
Alisema Tanzania baada ya kugundua gesi asilia, pamoja na mambo mengine
itatumika kwa matumizi ya nyumbani kwani kwa sasa zaidi ya tani 40 za
mkaa hutumika Dar es Salaam pekee kila mwaka, hivyo kiasi kikubwa cha
miti huteketea.
Kwa upande wake, Rais Gauck, alisema Ujerumani iko tayari kuendeleza
ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na Tanzania na ndiyo maana katika
msafara wake ameongozana na wadau mbalimbali wa sekta za kiuchumi,
wakiwamo wafanyabiashara wakubwa na waziri husika kwa lengo la kujifunza
na kuangalia fursa za uwekezaji.
Alisema
anaridhishwa na jinsi Tanzania inavyosimamia haki za binadamu na
kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa, umoja wa kitaifa na maendeleo,
na kwamba Ujerumani itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta
mbalimbali za maendeleo na Tanzania.
Rais Gauck alisema nchi hizi mbili zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria
tangu mwaka 1961, na ndiyo maana kuna miradi mbalimbali ya kiuchumi na
kijamii iliyotekelezwa, na kwamba Ujerumani inaisaidia kiuchumi
Tanzania.
Aliipongeza pia Tanzania kutokana na kushiriki katika kutuliza migogoro
ya kikanda, ikiwa ni pamoja na kutafuta amani Sudan Kusini na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa jinsi inavyojituma kupeleka
majeshi yake katika mataifa yenye machafuko, kwani kwa kufanya hivyo
inajilinda yenyewe.
Rais Gauck anatarajiwa pia kutembelea Zanzibar, Bagamoyo, Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti na ameomba akae Arusha kwa muda kabla ya kurejea
Ujerumani, kwani mji huo una sifa ya kipekee duniani.