Watu wawili wamekufa papo hapo huku wengine 45 wakijeruhiwa baada ya basi la abiria lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kugongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Vikonje wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema kuwa ajali hiyo
ilitokea jana saa 7.05 mchana wakati basi la Kidia lenye namba za
usajili T663 AXL kugonga lori lenye namba za usajili T 496 CFG na trela
lenye namba za usajili T576 AZX Scania.
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza wakati lori lilikuwa likitokea Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa lori, Fadhili Said (36) na utingo wa basi, Chogo Chigunda.
Kamanda
Misime alisema ajali hilo ilitokea wakati dereva wa basi la Kidia, Adam
Robert (34) alipokuwa akilifuata gari lililokuwa likilipita gari la
mbele yake.
Alisema
dereva wa basi baada ya kushindwa kulipita gari lililo mbele yake
alikutana na lori lililokuwa likija mbele yake na kusababisha ajali
hiyo.
Alisema Jeshi la Polisi wanamfuatilia dereva wa basi ambaye anatibiwa majeraha katika moja ya hospitali mjini hapa.