Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimejipanga kuhakikisha katika uchaguzi Mkuu hawaibiwi kura.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freemon Mbowe wakati
akizindua mafunzo ya Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha chama hicho (Red
Brigade), kwa vijana 200 wa Kanda ya Kati pamoja na Kikosi maalum cha
Karate.
“Katika
uchaguzi huu hatutaki kulalamika tena kwamba tumeibiwa kura na
tutahakikisha tutaomba kura kwa wananchi na tutazilinda,” alisema Mbowe.
Alisema endapo watakubali kuibiwa kura maana yake hawapo tayari kuongoza.
Mbowe
aliwataka vijana hao wa Brigade kutokukilinda chama peke yake bali pia
kiwe chachu ya ulinzi kwa jamii inayowazunguka kwenye maeneo yao.
Alibainisha kuwa Chadema kitaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi kwa vijana nchi nzima.
"Vijana
hawa lazima wajenge moyo wa kujitolea, chama kilijengwa na watu wenye
moyo huo ambao baadhi walipata madhara mbalimbali ikiwamo kupoteza
maisha,” alisema Mbowe.
Awali akisoma risala kwa niaba ya kikosi hicho, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Anatoly Isidory, alisema kikosi hicho kinachojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, kina jumla ya vijana 4,271.
Alisema kati ya hao, 200 wamepewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kulinda chama na mali zake, viongozi pamoja na kura katika Uchaguzi Mkuu.
“Hadi sasa yapo mafanikio mengi ambayo tumeyapata, ikiwamo kulinda mikutano ya chama pamoja na kuwalinda viongozi wetu katika mikutano hiyo,” alisema Isidory.