Watu saba wakiwamo wanafunzi sita wa darasa la nne katika shule ya msingi Nyakasanda na Mwalimu wa shule hiyo, Anderson Kibada wamekufa baada ya kupigwa na radi huku watu wengine 11 akiwemo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Laurence Sesegwa (42) wakijeruhiwa.
Kaimu
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kigaga Daga alisema kuwa watu hao
walifikwa na mauti hayo kufuatia mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na
radi zilizoanza majira ya saa tano asubuhi zilizotokea katika kijiji
cha Nyachenda wilaya ya Kasulu mkoani.
Mbali
na Mwalimu Kibada aliyekufa hapo hapo, Mganga huyo Mkuu wa Wilaya
aliwataja wanafunzi kuwa ni pamoja na Mary Steven (11), Severine Mussa
(11) na Joseline Joseph (12).
Aliwataja wanafunzi wengine waliofariki kuwa ni Joyness Simon (14), Nehemia Kepha (14) na Robin Gabriel (14).
Alisema
kuwa hadi sasa wanafunzi wanne wanaendelea na matibabu katika Hospitali
ya Wilaya ya Kasulu ambao aliwataja kuwa Fadhila Emanuel (13), Matilda
Moses (11), Bizimana Manjo (12) huku wanafunzi wengine saba wakiruhusiwa
baada ya hali zao kuwa nzuri.