WAZIRI Mkuu wa Zamani Edward Lowassa, amekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki iliyosema “Lowassa apanga safu”, akisema hana haja ya kufanya hivyo wala kutumia fedha kumnadi mgombea yeyote.
Taarifa iliyotolewa na ofisi yake ilisema habari hiyo ilijengwa na
taswira ya uongo kwamba kuna mpango wa kupanga nani atagombea ubunge
katika Jimbo la Monduli baada ya Lowassa kumaliza muda wake.
“Taarifa hiyo potofu ilikuwa na lengo la kumshushia Lowassa hadhi kwa wananchi wake,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taaifa hiyo, Lowassa anatarajia kupeleka malalamiko
rasmi kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Idara ya Habari
(Maelezo) ili ukweli ujulikane.
Ilisema habari hiyo ilidai kuwa Lowassa amewahonga makada kadhaa wa
CCM wilayani humo ambao wameonyesha au wana nia ya kuwania kiti hicho,
Sh millioni 10 kila mmoja ili wamuunge mkono Mbunge wa Viti Maalum,
Namelok Sokoine.
Taraifa hiyo ilimnukuu Lowassa akisema, “Huu ni muendelezo wa habari za
uongo na uzushi dhidi yangu ambao gazeti hili limekuwa likiufanya kwa
muda mrefu sasa. Gazeti hili limekuwa likitumika kama chombo cha
propaganda dhidi yangu,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Kwa muda mrefu sasa gazeti hili limekuwa likizusha habari za uongo
dhidi yangu. Mfano ni taarifa potofu na ovu ya mimi kufanyiwa upasuaji
mkubwa wa kongosho nchini Ujerumani jambo ambalo ni uongo”.
Alisema inasikitisha kuona gazeti lenye waandishi na wahariri makini
kama hilo linaweza kuacha kufuata maadili ya uandishi wa habari na
kuamua kuandika habari ambazo hazina hata chembe ya ukweli.
“Lazima watambue kwamba wananchi wamekwisha kuelewa uovu na uonevu wa gazeti hili dhidi yangu,” alisema.