NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Thursday, February 26, 2015

Andrew Chenge Agoma Kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma.....Adai kuna zuio la mahakama kuu, hatima yake kujulikana leo


MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Mtemi Andrew Chenge, jana ameonyesha utemi wake mbele ya Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, baada ya kusema haiwezi kumjadili kwa sababu kuna kesi mahakamani.
 
Alisema kuna zuio la Mahakama Kuu ambalo limevitaka vyombo vyote vya Serikali kutojadili suala la miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.
 
Tume hiyo inamtuhumu mbunge huyo kuwa alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitumia madaraka yake vibaya katika uuzaji wa hisa za Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwenda Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited.
 
Itakumbukwa wakati suala la Tegeta Escrow likijadiliwa bungeni, Chenge alidaiwa kupewa sh bilioni 16 na mmiliki wa VIP Engineering Tanzania Limited, James Rugemalira.
 
Jana, kabla ya Chenge kuieleza Tume ya Maadili kuwa haiwezi kumuhoji, Mwanasheria wa tume hiyo, Hassan Mayunga, alisoma mashtaka yanayomkabili.
 
“Mlalamikiwa akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwaka 1995 aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 wa kuongeza uzalishaji wa umeme na Kampuni ya IPTL.
 
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye Kampuni ya IPTL.
 
“Kitendo cha kuingia mkataba na Kampuni ya VIP ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(i) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha katika utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kwa masilahi binafsi,” alisema Mayunga.
 
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri wa Kampuni ya VIP huku akiwa na wadhifa wa ubunge, ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(e) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgogoro wa kimasilahi.
 
Mayunga alisema mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na VIP, ulimpatia masilahi ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume na kifungu cha 12(1)(e) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
 
“Mwaka 2014 mlalamikiwa aliingiziwa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 na kampuni hiyo katika Benki ya Mkombozi wakati hakutamka mapema kama aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali na kwamba ana masilahi binafsi na kampuni hiyo wakati alikuwa akijua kuwa Shirika la Umeme (Tanesco) lina mgogoro na IPTL,” alisema. Chenge
 
Baada ya kusomewa mashtaka, Chenge aliyakana na kuomba mwongozo kwa madai kuwa suala hilo lina zuio la Mahakama Kuu, hivyo basi tume hiyo haiwezi kujadili suala hilo hadi kesi ya msingi itakapokwisha.
 
“Napata shida kujadili suala hili, mimi nikiwa kama mwanasheria linanisumbua kidogo, kutokana na umahiri wako jaji, ninaomba upitie zuio lililotolewa na Mahakama Kuu kwa kina ili uweze kuangalia kisheria, je inaruhusiwa kujadili au la,” alisema Chenge.
 
Baada ya majadiliano hayo, Mwanasheria Mayunga alisema amri ya mahakama haihusiani na kazi za baraza kwani katika oda ya mahakama, hakuna kipengele cha kuzuia kujadili suala hilo.
 
“Ibara ya 132 ya sheria ya mwaka 1987, ibara ndogo ya kwanza ambayo inaeleza kuwa kutakuwa na sekretarieti ya maadili ya utumishi wa umma ya kuchunguza mienendo ya viongozi na watumishi wa umma.
 
“Taasisi hii ni huru na kwamba inafanya kazi endapo kuna taarifa ya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi katika suala la rushwa au kutumia madaraka yao vibaya,” alisema Mayunga.
 
Baada ya kusema hayo, Mwenyekiti wa barza hilo, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alihairisha shauri hilo na kusema watapitia zuio la mahakama hiyo ili waweze kuangalia kama ni kweli linaweza kuwazuia kufanya kazi zao au la na leo waweze kutoa uamuzi.
 
“Tumeomba muda kidogo ili tuweze kuipitia hii oda ya mahakama na kuiangalia kwa umakini kama ni kweli inatuzuia tusijadili suala hili au la, leo tutatoa uamuzi kamili,” alisema Jaji Msumi.
 
Aliongeza kutokana na hali hiyo, baraza hilo linapitia hoja ya mlalamikiwa na mlalamikaji ili kuangalia mambo ya kisheria yanayohusu kujadili au kutokujadili suala hilo.
 
Chenge akiwa nje ya Ukumbi wa Karimjee ambako mashauri hayo yanasikilizwa, waandishi walitaka kusikia maoni yake juu ya suala hilo na yeye akawajibu: “Andikeni kama mlivyoona na kusikia.”
 
Mbunge huyo alifika katika viwanja vya Karimjee saa 3:00 asubuhi kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri lake saa 3:15 baada ya jopo la majaji na mwenyekiti wa baraza hilo kuwasili.
 
Baraza hilo pamoja na kutolea uamuzi wa shauri la Chenge wa kusikilizwa au kutosikilizwa leo, pia linatarajia kumuhoji Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kwa siku mbili – leo na kesho.
 
KASHFA ZA CHENGE
Chenge ametajwa kuhusika katika kashfa mbalimbali, zikiwamo za rada, ajali iliyoua watu wawili na uchotwaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Rada
Chenge alitajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada, ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri.
 
Rada hiyo ilinunuliwa kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa dola milioni 40 mwaka 2001, kiwango kilicholistua Bunge la Uingereza.
 
Katika uchunguzi wa suala hilo, ilibainika kuwa Chenge alikuwa na akaunti kwenye Kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya dola milioni 1 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.8) hali iliyofanya ashinikizwe kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa miundombinu.
 
Ajali iliyoua wawili
Wakati kashfa ya rada ikiendelea, Chenge alihusika katika ajali iliyoua wanawake wawili mmoja akitajwa kuwa mtu wake wa karibu.
 
Baada ya ajali hiyo, alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha gari kizembe na bila kuwa na bima.
 
Alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 700,000 ambazo alilipa.
 
Tegeta Escrow
Mwaka jana alijikuta kwenye kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambapo alidaiwa kuchotewa Sh bilioni 1.6.
 
KAULI TATA
1. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.8 za rada, alisema ‘Ni vijisenti’.
 
2. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.6 za Escrow, alikuja na kauli mbili: “Mimi ni tumbili, hata kwenye hii (kashfa ya Escrow)” na “Mimi ni nyoka wa makengeza, nawatafutia wananchi fedha.”
 
3. Wakati wa kelele za kumtaka Chenge na wenzake kujivua gamba, mbunge huyo alisema: “Gamba limevuka limeishia kiunoni”.
 
4.Ashauri waliohusika na kashfa ya Escrow, mamlaka ya uteuzi (Rais) iwashughulikie na wapinzani wakaungana naye, lakini CCM wakagoma.
 
NYADHIFA ALIZOWAHI KUSHIKA
2014: Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya.
2006/15: Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.
2006/08: Waziri wa Miundombinu.
2006: Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
1993-05: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1991-93: Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1972-73: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM