Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kuwa haikurupuki katika kuwashughulikia na kuwafikisha mahakamani viongozi wanaotuhumiwa kujipatia fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba ushahidi pekee ndiyo itakaofanya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.
Akizungumza
mara baada ya kuzindua jengo la ofisi ya mkoa la Taasisi hiyo mjini
Kigoma juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema
hakuna atakayeachwa katika sakata hilo iwapo ushahidi utathibitisha pasi
na shaka kwamba alihusika.
Alisema
uchunguzi dhidi ya viongozi na watu mbalimbali waliohusina na uchotaji
wa fedha hizo unaendelea na kwamba ushahidi utakapokamilika kila mmoja
atapata kile anachostahili bila kumuonea mtu.
“Hatutaki
kukurupuka katika kushughulikia watuhumiwa wa sakata la Escrow na
muhimu ni ushahidi ambao utawatia hatiani watuhumiwa, ni aibu kwangu
kumfikisha mtuhumiwa mahakamani na mwisho wake siku ushahidi hautoshi na
mtuhumiwa kuachiwa huru,” alisema Dk Hoseah.
Aliwataka
wananchi kuwa na imani na chombo hicho katika kushughulikia suala hilo
na kwamba haki itatendeka kwa kuwashughulikia watuhumiwa wote kwa haki
badala ya kufuata kelele zinazopigwa kwamba hawafanyi kitu au
kuwashughulikia watuhumiwa wakubwa.
Tangu
kuibuka kwa sakata la kuchotwa kwa fedha katika Akaunti ya Tegeta
Escrow iliyokuwa imefunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada
ya kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Nchini
(Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, hatua kadhaa zimechukuliwa
na Serikali.
Hizo
ni pamoja na kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, kutenguliwa kwa
Uwaziri wa Dk Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, lakini pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema alijiuzulu mwishoni mwa mwaka jana, kama ilivyokuwa kwa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu
mwezi uliopita.