NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Monday, February 23, 2015

Mbatia Aikosoa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ifundi......Asema huo ni mpango wa Serikali Kuwalaghai Wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu


Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Taifa, James Mbatia (kulia), akionesha kitabu cha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitoa tamko la chama hicho juu sera hiyo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosene Nyambabe na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Musa Kombo Musa.
 Hapa mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Wanahabari wakiwa katika mkutano huo.
Wajumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) ya chama hicho waliokuwepo kwenye mkutano huo. Kutoka kulia ni Honest Mombory, Katibu wa Wazee, Ernest Mwasada, Dk.Nderakindo Kessy ambaye pia pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Angelina Mutahiwa na Esther Komba.
 
*****
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia amesema kuwa uzinduzi wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ni mpango wa serikali kuwalaghai wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakao fanyika Oktoba mwaka huu.
 
Pia amesema hali ya elimu nchini ni kama mgonjwa aliyekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, hivyo serikali isiwe inatoa majibu mepesi kwenye masuala magumu ambayo yanagusa maisha ya watanzania.
 
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitoa tamko la chama hicho kuhusu sera hiyo , Mbatia  alisema kuwa mnamo Januari 31 na Februari mosi mwaka 2013, aliwasilisha hoja bungeni kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu.
 
Alisema kuwa aliorodhesha athari mbalimbali za udhaifu wa wa elimu itolewayo nchini lakini suala hilo lilionekana kutawaliwa na siasa ambapo haikuwa lengo lake,lengo lilikuwa kuhakikisha kuwa sera mbalimbazi za elimu zinaboreshwa.
 
Mbatia aliongeza kuwa mnamo Februari 13, 2015 mwaka huu Rais Jakaya Kikwete, alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 lakini ikiwa haijajibu hoja alizokuwa amezitoa.
 
Alifafanua kuwa wakati Rais akihutubia alisema kuwa sera hiyo ilitumia miaka saba kukamilika, lakini Mwenyekiti huyo alisema baada ya kuipitia alibaini sera hiyo kuwa na lugha ngumu huku ikiwa na makosa mengine mengi.
 
Mbatia alisema anachokiona kwa serikali kuzindua sera hiyo mwaka huu ni mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu,kwani yaliyomo ndani ya sera hiyo yamelenga kuwalaghai wapiga kura.
 
Aidha alisema mambo hayo ni pamoja na kutangaza kuwa elimu ya msingi kutolewa bure bila karo na lugha iliyotumika inawachanganya watanzania hivyo ni vigumu kwa wananchi wa vijijini ambao wengi wao hawana elimu kutambua yaliyoandikwa ndani ya sera hiyo.
 
"Mfano sera mpya ina matamko mawili ambayo  inawachanganya watanzania kuhusu lugha ya kufundishia,moja inatamka Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia ngazi zote za elimu,na ya pili inatamka kuwa Kingereza kitatumka kama lugha ya kufundishia katikan ngazi zote za elimu.
 
"Matamko haya mawili, kwanza yanakwepa lawama zinazotokana na malumbano ya muda mrefu kuhusiana na lugha gani inafaa kufundishia, pili imehalalisha mifumo miwili ya elimu ndani ya nchi moja" alisema Mbatia kwa msisitizo 
 
Hivyo alisema serikali ilipaswa kutengeneza sera ambayo inazungumza kwa uhakika kuhusu suala la lugha ya kufundishia, kuliko kutoa tamko la sera lisilo na msimamo.
 
Aliweka wazi kuwa wanapendekeza iundwe tume ya kudumu ya elimu nchini itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine kuhakikisha ubora wa elimu unapatikana nchini.
 
Vilevile alisema wanaiomba serikali kupitia upya sera hiyo kabla haijaanza kutumika ili kuepusha taifa na madhara ambayo yameonesha dalili za kutokea hata kabla haijaanza kutumiaka.