SERIKALI itakayoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) imeahidi kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogowadogo ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo katika shughuli za uchimbaji wa madini huku ikihakikisha kuwa kampuni kubwa za uwekezaji zikilipa kodi stahiki ya Serikali.
Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa
Ibrahimu Lipumba, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Kahama katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja CDT mjini hapa.
Lipumba alisema kuwa kwa sasa Serikali imekuwa haiwajali wachimbaji
wadogowadogo wa madini hususani wa madini ya dhahabu ambapo wamekuwa
wakigundua maeneo yenye madini kisha baadaye huondolewa na Serikali kwa
kile kinachodaiwa kuwa hawana leseni za kumiliki maeneo hayo.
Alisema kuwa wachimbaji hao wamekuwa waathirika kila wanapoibua
maeneo ya mgodi kwani hutolewa badala ya Serikali kuwajengea uwezo wa
uchimbaji pamoja na kuwaongezea mitaji hali ambayo ingesaidia kupunguza
kukosekana kwa ajira tatizo ambalo ni kubwa kwa vijana nchini.
Aidha Lipumba aliitaka Serikali kutokuwakumbatia wawekezaji wakubwa
hasa wa madini na kuwasahau wale wadogo ambao ndio chanzo cha kupatikana
kwa maeneo ya uchimbaji na kuwa chanzo cha kukua kwa miji midogo katika
maeneo ya uchimbaji wa madini.
Pamoja na mambo mengine Lipumba alisisitiza kwa Serikali kuwatafutia
wakulima wa zao la tumbaku na pamba masoko ya uhakika yatakayoleta tija
kwa wakulima na kuondokana na malalamiko yaliyopo kwa wakulima wa mazao
hayo kwa sasa katika Kanda ya Ziwa.
Pia Lipumba alisema Ukawa itakapoingia madarakani haitatoa nafasi kwa
kampuni kubwa kusamehewa kodi kwani kwa kufanya hivyo kunarudisha nyuma
maendeleo ya taifa na kukosekana pato ambalo linaweza kuwasaidia
wajasiriamali wadogo ambao hawana kipato kwa sasa.