MBUNGE wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya (CUF), ameitaka Serikali kupiga marufuku unywaji wa pombe kwa kuwa ni kichocheo cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Akiuliza
swali bungeni jana, Sanya alisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kupiga
marufuku uuzwaji wa pombe hizo zikiwemo za kienyeji na pombe za
viwandani.
“Kama
hilo haliwezekani basi katika bajeti ijayo iongeze tozo pombe kwa
asilimia 100 ili fedha zitakazopatikana ziende zikasaidie waathirika wa
Ukimwi au miradi ya REA (Mradi wa Umeme Vijijini),” alisema Sanya.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe,
alisema Serikali imepiga marufuku unywaji wa pombe haramu.
“Vile
vile tunapiga marufuku unywaji wa pombe kupita kiasi, unywaji wa pombe
kupita kiasi haukubaliki, unywaji wa bia sio kunywa kreti zima.
“Kwa
jinsi tulivyoumbwa binadamu tuna uwezo wa kunywa bia moja kwa kila saa
moja, hata hivyo kimaumbile kwa mwanamke anaruhusiwa kunywa angalau bia
moja hadi tatu kwa saa 24 na mwanaume anatakiwa kunywa bia tatu hadi nne
kwa saa 24,” alisema.
Awali
akijibu swali la msingi la Sanya, Dk. Kebwe alisema Serikali kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali imetengeneza miongozo maalumu kwa ajili
ya kuwasaidia watumishi wa afya kutoa ushauri kuhusu lishe bora kwa
waathirika wa VVU wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU.
“Ushauri huo ni pamoja na aina ya vyakula vinavyomfaa mtumiaji wa dawa ambavyo vinapatikana kwenye jamii yake.
“Pia
waathirika wa VVU wote wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi
wanafanyiwa uchunguzi mara kwa mara kubaini hali yao ya lishe na kupewa
ushauri au matibabu stahiki ikiwa ni pamoja na virutubisho kama vile
vitamin, madini na chakula na dawa,” alisema Dk. Kebwe.
Katika
swali lake Dk. Kebwe alitaka kujua Serikali inawasaidiaje waathirika wa
VVU wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU kupata lishe bora