NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Saturday, July 4, 2015

ACT yailalamikia CHADEMA kuhujumu mikutano yake


CHAMA cha Alliance for Change and Transparency(ACT), kimebaini kuwepo kwa mipango inayoratibiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kuhusika kuhujumu mikutano yake mbalimbali.
 
Hujuma hizo zimebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Mipango na Mikakati Taifa  wa ACT Habibu Mchange, aliyesema kuwa chama hicho kimekuwa kikihangaikia ACT na kusahau kushughulikia matatizo ya watanzania.
 
“Chadema wamekuwa wakitufuatilia kila mahali tunapofanya mkutano na hilo wamekuwa wakifanya kwa sababu ya kutuhofia. Kwa mfano tulipokuwa na mkutano Mwanza na wao wakatangaza kufanya tukawashinda, kesho tumetangaza kufanya mkutano na wao wametangaza kufanya Kawe.
 
“Chadema tunawaonea huruma kwa kuwa tutawafanya kitu ambacho hawatasahau katika historia ya siasa za tanzania kwa sababu njia nyingi wanazotumia ni zile tulizoziratibu wakati tukiwa huko,”alisema Mchange.
 
Katika hatua nyingine Mchage alisema baada mbalimbali mikoani hivi sasa ACT kupitia viongozi wake  wa kitaifa wameandaa kufanya mkutano mkubwa kesho jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga.
 
“Mkutano huo utatoa fursa ya kuzindua Ilani ya jiji la Dar es salaam, itakayotokana na ilani Kuu  ya chama ili kukabiliana na kero mbalimbali za jiji.
 
“mkutano huo utatoa fursa ya ACT kuwataka watanzania kuishi katika misingi ya haki, undugu, umoja na mshikamano kwa kutumia azimio la Tabora lilozinduliwa na chama hicho likiwa limewisha azimio la Arusha,”alisema.
 
Chama hicho kinatarajia kusimamisha madiwani, wabunge na nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
 
Akizungumzia tuhuma hizo msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema chama hicho hakina muda wa kuzungumzia tuhuma ambazo hazina mashiko.