NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Wednesday, July 1, 2015

Membe Arudisha Fomu Ya Urais......Akana Kuhusika Na Ufisadi Wa Mabilioni Ya Libya.


WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, jana amerudisha fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM ili aweze kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu, kwa tiketi ya chama hicho.

Mbali ya kurudisha fomu hiyo katika Ofisi Kuu ya CCM, Mjini Dodoma, Bw. Membe alitumia fursa hiyo kuzungumzia taarifa za uvumi dhidi yake kuwa anahusika na ufisadi wa mabilioni ya Libya na kusisitiza uvumi huo ambao unaenezwa na wanasiasa wenzake hauna mashiko.

Alisema wanasiasa wanaoeneza uvumi huo, wanafahamu ukweli wa jambo hilo lakini kwa makusudi wanataka kuifanya jamii ya Watanzania iuamini na kuukubali ambapo yupo tayari kujiuzulu nafasi yake ikibainika amehusika kuchukua hata dola moja.

Aliongeza kuwa, hahusiki na ufisadi wowote wa dola za Marekani milioni 20 kama taarifa za uvumi huo zinavyodai na kulitolea ufafanuzi suala  hilo pamoja na mchakato wake ulivyokwenda.

Bw. Membe alisema, Libya ni kati ya nchi wafadhili wa Tanzania kama ilivyo kwa wafadhili wengine ambayo imekuwa ikitoa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa Serikali ya Tanzania.

Alisema Serikali imekuwa ikifanya taratibu za kulipa madeni ya nchi wafadhili kwa njia tofauti ikiwemo ya kubadili madeni na  kuyaingiza katika miradi yaani 'Dept Swap'.

Alisisitiza kuwa, katika utaratibu huo, Julai 20,2005, Serikali ya Tanzania na Libya zilitiliana saini mkataba wa kubadili deni (Dept Swap Agreement) ambapo uliweka utaratibu wa matumizi na urejeshaji fedha za deni la Libya.

Aliongeza kuwa, Machi 4,2009, Serikali ya Libya na Tanzania zilitiliana saini mkataba wa nyongeza ambao pamoja na mambo mengine, ulizungumzia matumizi ya dola za Marekani milioni 20 zilizokuwa zimehifadhiwa katika akaunti ya Libya No. 004-200-0002216-01, Benki ya Rasilimali (TIB).

Bw. Membe alisema nyongeza hiyo ya mkataba, ilitamka wazi kwenye kifungu No. 4.02, kwamba, fedha zilizopo katika akaunti tajwa, zikopeshwe mwekezaji waliyemteua wenyewe Kampuni ya Meis Industries Limited ili iweze kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kiwanda cha Saruji, mkoani Lindi.

Mkopo huo ulipaswa kulipwa ndani ya miaka sita na baada ya hapo, fedha hizo zirejeshwe na ziendelee kukopeshwa Watanzania kwa ajili ya miradi mingine ambayo Serikali za Libya na Tanzania zitakuwa zimeridhia.

Alisema kabla Serikali ya Libya haijatia saini nyongeza ya mkataba huo uliotaka fedha zikopeshwe kwa kampuni hiyo,  upembuzi yakinifu wa mradi husika ulifanywa na Serikali ya Libya kupitia vyombo vyake na wao kujiridhisha juu ya ubora wa mradi huo.

Alifafanua kuwa, Serikali ya Libya kupitia Ubalozi wake nchini, iliendelea kusisitiza kwa maandishi kwamba Serikali ya Tanzania iharakishe mchakato wa kuwezesha fedha hizo zikopeshwe kwa mwekezaji waliyemteua ili mradi huo usiendelee kuchelewa na pia fedha ambazo zitarejeshwa ziendelee kuwanufaisha Watanzania.

"Katika kutekeleza mikataba hii yaani Dept Swap Agreement pamoja na Addendum Dept Swap Agreement pia kwa kuzingatia umuhimu ambao Serikali ya Libya iliuonesha, Serikali ya Tanzania kupitia wataalamu wake wa Wizara ya Fedha, TIB, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Mwekezaji (kampuni ya Meis), walikutana chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na kuandaa hadidu  rejea.

"Hadidu hizo zilisababisha kutengenezewa mkataba wa uwekezaji kati ya Serikali ya Tanzania, TIB, Serikali ya Libya na mwekezaji ambapo Serikali ya Tanzania, TIB na Mwekezaji, walitia sahihi mkataba huo na kuupeleka Libya ili Serikali yao iweze kutia saini," alisema.

Bw. Membe alisema, kwa sababu ambazo hazikufahamika, Serikali ya Libya haikutia saini mkataba huo ambapo baada ya mwekezaji kufuatilia muda mrefu bila mafanikio, alimwandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania yenye No. PC/MEIS/AG/2/10, Septemba mosi, 2010 akieleza kusudio la kuipeleka Serikali ya Libya Mahakamani kwa kitendo chake cha kutokutia saini mkataba huo.

Alisema Septemba 13,2010, mwekezaji alifungua shauri la madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania No. 124/2010 dhidi ya Serikali ya Libya, akiomba Mahakama Kuu itoe tamko kwamba, kitendo cha Serikali ya Libya kukataa kutia saini mkataba huo hakikuwa cha haki.

Kampuni hiyo pia iliitaka Mahakama hiyo itoe amri kuwa fedha hizo zitolewe kwa mwekezaji ili aweze kutekeleza mradi uliokusudiwa ambapo kumbukumbu zinaonesha wito wa Mahakama (Summons), ulipelekwa Ubalozi wa Libya lakini hakukuwa na majibu wala mwakilishi aliyekwenda mahakamani.

"Mahakama Kuu kwa kufuata taratibu zake, iliendelea kusikiliza shauri na kutoa amri ya fedha hizo kutolewa kwa mwekezaji aweze kutekeleza mradi husika...Benki ya TIB na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali walifanya juhudi za kupinga amri hiyo au kupata ufafanuzi zaidi juu ya utekelezwaji wake.

"Hata hivyo, Mahakama Kuu pamoja na Mahakama ya Rufaa kwa nyakati tofauti, zilishughulikia maombi hayo...TIB ilifungua maombi No. 126/2010 Mahakama ya Rufaa kuiomba izuie na kufuta utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu na maombi hayo yalifanyiwa uamuzi wa mwisho Novemba 7,2011 kwa kuondolewa mahakamani," alisema.

Bw. Membe aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufaa, ilisema maombi hayo hayakuwa yamefuata taratibu za kisheria ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, naye alipeleka maombi Mahakama ya Rufaa No. 146/2010 akiomba Mahakama hiyo kufuta mwenendo wa kesi na amri ya Mahakama Kuu.

Alisema Mwanasheria Mkuu pia alipeleka maombi ya pili No. 147/2010 ikiiomba Mahakama ya Rufaa izuie utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ambapo maombi yote yalisikilizwa na kuamuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za kimahakama.

Aliongeza kuwa, wakati mvutano huo ukiendelea, ilijitokeza Kampuni ya Mohamed Enterprises Limited ikidai ina haki juu ya fedha hizo hivyo na wao walipeleka maombi Mahakama Kuu kuzuia utekelezaji wa hukumu wakidai kampuni hiyo ilikuwa ikiishtaki Serikali ya Libya.

Kampuni hiyo ilidai walifungua kesi ya madai No. 110/2010 hivyo amri ya Mahakama Kuu ikitekelezwa na kumpa fedha hizo mwekezaji, wangekosa mahali pa kukazia hukumu waliyoitarajia katika kesi yao kwa Serikali ya Libya ambapo maombi yao yalisikilizwa na kutolewa maamuzi stahiki.

"Kampuni ya Mohamed Enterprises Limited haikuridhika na uamuzi wa Mahakama Kuu hivyo walipeleka shauri Mahakama ya Rufaa kupitia maombi No. 2/2011 ambayo nayo yalisikilizwa na kutolewa maamuzi.

"Mwisho wa yote, maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa katika mchakato huu, mwekezaji alikuwa na haki ya kupewa fedha za mradi wa Kiwanda cha Saruji mkoani Lindi kama ilivyoainishwa katika mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Libya," alisema Bw. Membe.

Alisema ni wazi kuwa, mgogoro huu ulichujwa na mahakama hadi ngazi ya juu kwa nyakati tofauti, mbele ya Majaji wa Mahakama Kuu na Rufaa ambapo katika Taifa linaloongozwa kikatiba, chini ya utawala wa sheria kama Tanzania, Mahakama ndicho chombo kilichopewa mamlaka ya mwisho kuamua juu ya haki za raia na Serikali.

Aliongeza kuwa, si rahisi na hatakuwa sahihi kwa mtu yeyote kuhoji uhalali wa mchakato huo ulivyoongozwa, kuelekezwa, kuamuliwa na mahakama, bali sheria inatoa mwanya wa kurudi mahakamani kwa mtu ambaye hajaridhika au anayetaka kuhoji maamuzi haya.

Bw. Membe alisema kwa mtu yeyote mwenye kutazama masilahi ya nchi ni dhahiri kuwa suala  la utekelezaji mikataba ya kubadilishana madeni ni jambo lenye manufaa kwa Tanzania na fursa inapotokea itekelezwe.


"Nchi wafadhili, wanapotoa fursa za kutupunguzia mzigo wa madeni katika utaratibu wenye manufaa kama huu, tutaonekana wa ajabu tukiendelea kulumbana badala ya kuchangamkia fursa ya maendeleo.

"Mimi kama Mbunge kutoka mkoani Lindi na Waziri mwenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, nalifuatilia kwa karibu suala hili kwa sababu kuu mbili; moja mradi huu utawanufaisha wapiga kura wangu na Watanzania kwa kuinua uchumi wao, kuongeza ajira kwenye mikoa ya Kusini ambayo imeachwa nyuma," alisema.

Alisema utafiti unaonesha kuwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ina utajiri mkubwa wa malighafi ya saruji na upo uhakika wa kupata saruji bora na kwa bei nafuu sana...sababu ya pili suala hili linagusa uhusiano wa nchi mbili; hivyo lazima wizara yangu ilisimamie kwa nguvu, umahiri na kwa  umakini wote.

"Fedha hizi ambazo ni mkopo zilizotolewa kwa amri ya Mahakama na hazikuchukuliwa kama zile za EPA au Escrow, bali ni mkopo ambao ulitolewa kwa Kampuni ya Meis kulingana na mkataba wa makubaliano yenye masharti ya kibenki na ikishindwa kuulipa, itafilisiwa mali zake na TIB itarudishiwa fedha zake," alisema.

Bw. Membe alisema yeye hana kampuni nchini, hana ubia na kampuni yoyote ikiwemo ya Meis na hana hisa katika kampuni hiyo, hajafaidika na mkopo huo ambao unasimamiwa na TIB.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa kiwanda hicho unaendelea vizuri na mitambo yote inayotakiwa katika ujenzi tayari imewasili ambapo asilimia 45 ya ujenzi wa kiwanda hicho, umekamilika na matarajio ya kampuni husika ni kiwe kimekamilika ifikapo Desemba, mwaka huu.

Alisema kama kuna mtu anahitaji taarifa zaidi awe huru kuihoji kampuni ya Meis, TIB ambayo imetoa mkopo huo, kwenda kwa Msajili wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa ambazo zote ziliamua kampuni hiyo ipewe mkopo kwa mujibu wa sheria za kibenki.

Bw. Membe aliwataka wagombea wenzake wa nafasi ya urais ndani ya CCM, kukubali matokeo; lakini suala la mgombea kujiaminisha kuwa jina lake haliwezi kukatwa si la kiungwana.

"Jina langu likikatwa nitawaunga mkono mgombea ambaye atapita, lengo letu ni ushindi, mwanasiasa aliyekomaa hawezi kusema jina lake haliwezi kukatwa," alisema Bw. Membe.