Mbunge wa Kahama, James Lembeli ameiweka njia panda CCM baada ya kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
Uamuzi
wa Lembeli umekuja wakati wanachama kutoka sehemu mbalimbali
wakitangaza uamuzi wao wa kujiengua CCM na kujiunga na vyama vya
upinzani, hasa Chadema ambayo imesomba asilimia kubwa ya wahamaji hao.
Akizungumza jana baada ya kuzagaa kwa taarifa katika mitandao ya
kijamii kuwa amekihama chama chake na kuhamia Chadema, Lembeli alisema
taarifa hizo ni uvumi uliozagaa jimboni kwake, lakini hajajiunga na
chama chochote.
“Ni uvumi tu na uvumi wenyewe
umechangiwa na swali nililoulizwa leo na wananchi kwamba ‘mbona toka
mchakato wa kuchukua fomu umeanza hatujakuona’ na mimi nikawajibu kuwa
‘sitachukua fomu’,” alisema.
Lembeli (pichani) alisema
amechukua uamuzi huo kutokana na rafu inayoendelea jimboni humo na
maneno ya baadhi ya wanachama, wakiwemo viongozi kuwa hatakiwi na vigogo
ndani ya CCM.
Lembeli, mmoja wa wabunge waliokuwa
mstari wa mbele wakati wa kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow, alisema sababu za kutotakiwa huko zinatokana na dhana
potofu ya baadhi ya viongozi kwamba michango yake ndani na nje ya Bunge
inaivua nguo Serikali.
“Tangu mchakato wa uchukuaji wa
fomu umeanza baadhi ya wanachama wengi tu wameitwa kwenye vikao visivyo
halali karibu kata zote wakiwa na kadi zao na kuorodheshwa na kupewa
maagizo ya kunikataa kwenye kura ya maoni na wengine wanapewa Sh5,000,”
alisema
Lembeli alidai kuwa
mbaya zaidi ni kwamba zipo kadi mpya za CCM zinazotolewa kiholela bila
kufuata utaratibu na licha ya kulalamikia hali hiyo hakuna hatua
zilizochukuliwa.
Alisema kutokana na yote hayo, aliwahi
kusema kwenye mkutano wa hadhara kuwa kuna njama hizo, lakini badala ya
CCM kufanyia kazi madai hayo, wakamuita mbele ya Kamati ya Maadili.
“Kwenye
kamati ya maadili nilituhumiwa kuwa nakidhalilisha chama na kutakiwa
niwataje nani walioniambia sitakiwi. Niliwajibu, tena kwa maandishi na
kuwapa orodha, lakini mpaka leo kimya ina maana mimi bado ni mtuhumiwa,”
alidai.
“Mimi siyo mtoto mdogo. Naelewa nini
kinaendelea na ndiyo maana nimesema sitachukua fomu ya kugombea ubunge
kwa mazingira haya. Bado sijatangaza kuhama CCM”.
Wakati
Lembeli akisisitiza suala la kuhama kwake ni fununu tu, habari nyingine
zilidai huenda akagombea ubunge kwa tiketi ya Chadema kutokana na
kutokubaliana na mchakato huo anaodai ni batili.
Lembeli
anaonekana kuwa mwiba ndani ya Serikali ya CCM baada ya kuiongoza
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bunge katika uchunguzi wa
uendeshaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili na kuibuka na taarifa
iliyoonyesha kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Mawaziri hao ni Balozi Hamis Kagasheki, Dk. David Mathayo, Dk. Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na Ezekiel Maige.
Lembeli
pia nusura ajikute nje ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2010 wakati
alipopigiwa simu na katibu mkuu wa CCM wa wakati huo, akiambiwa achukue
fomu za kuwania ubunge wa jimbo jipya la Ushetu.
Wakati
huo, Lembeli alidokezwa siku ya mwisho na ofisa mmoja wa Tume ya
Uchaguzi kuwa hakukuwapo na jimbo hilo na kulazimika kufanya jitihada
katika muda mfupi kuchukua fomu kwenye Jimbo la Kahama na kufanikiwa
kushinda kiti hicho.
Hivi karibuni, Lembeli
alitofautiana na taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi
Ombeni Sefue ya kuwasafisha mawaziri na katibu wa wizara waliowajibika
kutokana na kashfa ya escrow na Operesheni Tokomeza.
Lembeli alisema kitendo cha kuwasafisha viongozi hao ni kuipeleka nchi gizani.
“Yuko
hapa (waziri mkuu wa zamani, Edward)Lowassa. Japo mimi sipendi wizi na
ufisadi, katika kashfa ya Richmond nilikuwa mmoja wa waliopiga kelele
awajibike. Lakini wengine wamesafishwa, kwanini naye asisafishwe,”
alisema baada ya taarifa hiyo ya Ikulu.
“Kama ni kusafishana tusafishwe wote, tuanze upya ndipo nchi hii itatawalika, vinginevyo huko mbele kuna giza nene.”