Wasomi mbalimbali nchini, wamepokea kwa mtazamo tofauti uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake wa Mwenyekiti wa CUF Taifa wengine wakisema suala hilo si jipya bali ni aina ya changamoto zilizopo kwenye vyama vya siasa nchini.
Wakizungumza
na mtandao huu kwa nyakati tofauti, wasomi hao pia walimshangaa Prof.
Lipumba kwa uamuzi huo kwani alishiriki tangu mwanzo katika kumpokea
mgombea urais aliyepitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Bw.
Edward Lowassa, tangu alipohama CCM na kujiunga na CHADEMA.
Dkt. Lazaro Swai wa OUT
Akizungumzia
uamuzi huo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Jamii katika Chuo Kikuu
Huria Tanzania (OUT), Dkt. Lazaro Swai, alisema anamshangaa Prof.
Lipumba kwa uamuzi aliouchukua.
"Hizo
ni aina ya changamoto zilizopo kwenye vyama vya siasa tangu
vilipoanzishwa, hilo ni shinikizo kutoka upande mmoja lakini si kutoka
UKAWA wala CUF," alisema Dkt. Swai.
Aliongeza
kuwa, hivi sasa katika vyama vya siasa kila mtu ana mvuto wa aina yake
lakini kujiuzulu kwa Prof. Lipumba kutakuwa na mtikisiko kwa UKAWA na
CCM kutokana na kuhama kwa Bw. Lowassa.
"Ujio
wa Lowassa hauwezi kuipasua UKAWA, kujiuzulu kwa Lipumba kuna kitu
ndani yake na kuleta mashaka kwa Watanzania, kwanini iwe sasa ndipo
ajiondoe katika nafasi hiyo wakati alishiriki tangu mwanzo kumpokea
Lowassa," alihoji.
Askofu Bagonza
Askofu
wa Kanisa Katoliki Jimbo la Karagwe, mkoani Kagera, Benson Bagonza,
alisema kujiuzulu kwa Lipumba kunaashiria kuna jambo nyuma ya pazia,
kwani wananchi hawataelewa.
"Tangu
mwanzo alikuwa msingi imara kwenye UKAWA, ghafla anajiuzulu hiyo
inashangaza watu wengi na sitaki kuamini kama amefikia uamuzi huo," alisema na kuongeza;
"Kutakuwa
kuna jambo jingine limetokea nje ya UKAWA lakini swali la kujiuliza,
kwanini alichelewa kuchukua uamuzi huo...huyo si Lipumba tunayemjua," alisema.
Dkt. Benson Bana
Naye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya
Siasa ya Jamii, Dkt. Benson Bana, alisema kujiuzulu kwa Prof. Lipumba
kulitarajiwa kutokana na mvutano uliokuwepo tangu awali.
"Ameona
ni wakati mwafaka kuachia ngazi pia ni haki yake ya msingi kwani ndani
ya muungano wa UKAWA, hauwezi kumpokea mtu wakati huo huo akawa maarufu
kushinda chama.
"Hilo
ni pengo la kudumu ambalo haliwezi kuzibika kwa siku moja, uamuzi wa
Lipumba na Slaa utakuwa wa halali kwani waliwekeza sana kwenye vyama
vyao," alisema na kuongeza kuwa, kiongozi yeyote anapimwa kwa uadilifu na walikuwa tayari kujitoa kafara katika nyadhifa zao.
Julius Mtatiro
Kwa
upande wake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Bw. Julius
Mtatiro, alisema hilo ni pigo kubwa kwa CUF na UKAWA hasa kipindi hiki
cha kutafuta ushindi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Kwa
mujibu wa ujumbe wake alioutuma kwenye akaunti yake ya Facebook, Bw.
Mtatiro alisema uamuzi huo ni mgumu kwani hajawahi kuusikia tangu awe
mwanachama wa CUF miaka nane iliyopita.
Alisema
kidemokrasia lazima kukubali matokeo na uamuzi binafsi wa mtu yeyote
kwani mwisho wa siku, mtu hufanya uamuzi wake na tunalazimika
kuyaheshimu ili maisha yaendelee.
Aliongeza
kuwa, si vizuri kumshutumu Prof. Lipumba kwenye mitandao na kwingineko
bali akumbukwe kwa mchango wake mkubwa kisiasa ambapo jemedari
anapoanguka vitani bunduki yake huchukuliwa na vita kuendelea.