NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Thursday, August 13, 2015


OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU YATANGAZA MATOKEO YA TAKWIMU ZA PATO LA TAIFA
                     


X1
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam wakati akitangaza matokeo ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 ambayo yameonyesha kuwa thamani ya Pato la imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.
X3
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke wakati akitangaza matokeo ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 ambayo yameonyesha kuwa thamani ya Pato la imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.
Matokeo ya takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka ya kwanza yaani kuanzia mwezi Januari – Machi, 2015 yameonyesha kuwa thamani ya Pato la Taifa imekua na kufikia shilingi trilioni 21.9 ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 ya robo mwaka ya kwanza ya mwaka 2014.(VICTOR)

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke amesema takwimu hizo zimetayarishwa kwa kuzingatia marekebisho ya Takwimu za Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2007.
“Pato la Taifa kwa bei za mwaka 2007 katika kipindi cha robo mwaka ya kwanza linaonyesha kuwa na jumla ya thamani ya shilingi trilioni 10.6 kwa mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi trilioni 9.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2014”, amefafanua Oyuke.
Oyuke amesema kuwa, Pato hili la Taifa limeongezeka kwa kasi ya asilimia 6.5 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Aidha, Oyuke amesisitiza kuwa utayarishaji wa takwimu za Pato la Taifa hujumuisha shughuli zote za kiuchumi na hivyo hutumika katika kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha sera za kiuchumi.
Baadhi ya shughuli hizo za uchumi ni kilimo na mifugo ambazo zilikua kwa kasi ya asilimia 2.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 3.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli za Uvuvi ziliongezeka kwa asilimia 0.9 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 2.3 kipindi kama hicho mwaka 2014. Ukuaji huu ulitokana na jitihada za Serikali kuwasaidia wakulima kwa kutoa ruzuku na maelekezo ya Ma-ofisa Ugani kwa wakulima kama vile kuchagua mbegu bora yaliyosaidia kuongeza uzalishaji.
Shughuli za Uchimbaji Madini, Mawe na Kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 0.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya ukuaji wa asilimia 19.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli za Uzalishaji bidhaa Viwandani zilikua kwa kasi ya asilimia 5.7 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.2 kipindi kama hicho mwaka mwaka 2014. Kasi ya ukuaji ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa bidhaa za vyakula, vinywaji, tumbaku, nguo, simenti na bidhaa za kemikali na madawa.
Shughuli nyingine ni pamoja na Uzalishaji nishati ya umeme na maji ambazo zilikua kwa kasi ya asilimia 10.7 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 10.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2014. Kuongezeka kwa ukuaji wa nishati ya umeme kulitokana na kuongezeka kwa umeme uliozalishwa kutoka kwenye mitambo inayotumia, maji, mafuta na gesi asilia.
Shughuli za Fedha na Bima katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ziliongezeka kwa asilimia 9.1 ikilinganishwa na asilimia 11.2 kipindi kama hicho mwaka 2014.
Shughuli za Ujenzi (ambazo zinajumuisha ujenzi wa nyumba za makazi na zisizo za makazi; barabara na madaraja; na shughuli nyingine za uhandisi) katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2015 ziliongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na asilimia 21.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2014.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu ina jukumu la kutayarisha na kusambaza takwimu rasmi nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za Pato la Taifa kwa robo Mwaka ambazo hupimwa kwa kuangalia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini katika vipindi vya miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari – Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba – Desemba.