NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Thursday, August 13, 2015

JE TRAFIKI ANARUHUSIWA KUKUNYANG”ANYA LESENI ?




Kumekuwepo na sintofahamu nyingi kwa madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya usafiri. Sintofahamu hii imekuwa ikiletwa na baadhi ya mambo ambayo hayaeleweki sawasawa katika suala zima la usalama barabarani na sheria zake. Wadau wa barabarani wamekuwa wakilaumiana, madereva wakiwalaumu askari wa barabarani kwa uonevu huku askari wa barabarani wakiwalaumu madereva kwa ukorofi na ukosefu wa utii wa sheria bila shuruti. Lakini swali hapa ni kwanini iwepo mivutano na hali kuna sheria. Sheria inasemaje kwa kila jambo ambalo wadau hawa wanatofautiana?.
1.UBABE WA ASKARI WA BARABARANI.
Baadhi ya askari wa barabarani wamekuwa ni wababe sana. Wanahoji mambo ambayo si wajibu wao kuyahoji na hawataki dereva aulize lolote kuhusu kuhoji kwao mambo hayo. Wanataka kila wanachosema dereva atii hata kama anaona hakipo kwa mujibu wa sheria. Matokeo yake mtu anaandikiwa faini za makosa mengi ilimradi tu kumkomoa. Askari wengine wamefikia hatua ya kuwapiga madereva vibao. Binafsi nimewahi kushuhudia askari wa usalama barabarani akimnasa kibao dereva wa daladala. Ni ubabe uliovuka mipaka na hakika ni uvunjaji wa sheria uliopitiliza.


2. JE TRAFIKI ANARUHUSIWA KUMNYANGANYA DEREVA LESENI.
Masuala ya usalama barabarani yanaainishwa ndani ya Sheria ya Usalama barabarani ( The Road Traffic Act) ambayo ndio hueleza wajibu na haki za kila mdau na mtumiaji wa barabara. Katika sheria hii hakuna pahala pameandikwa kuwa trafiki achukue leseni ya dereva kwa kuwa dereva ametenda kosa fulani. Maana fupi ya hili ni kuwa trafiki haruhusiwi kuchukua leseni ya dereva. Anachoweza kufanya trafiki ni kile kilichoainishwa na kifungu cha 17 cha sheria hiyo ya usalama barabarani. Kifungu hicho kinampa trafiki mamlaka ya kukagua na kujiridhisha na uhalali wa leseni ya dereva. Hakisemi aichukue. Kinasema aikague basi. Kukagua na kuchukua ni mambo mawili tofauti.
Kama hivyo ndivyo basi yafaa kueleweka kuwa kitendo cha askari kumsimamisha dereva na kisha kumpokonya leseni yake ni kinyume cha sheria.
Dereva anao wajibu wa kulinda haki hii kwa kulikataa hili na kuhakikisha trafiki hamfanyii kitendo hiki. Kumbuka kuwa wakati askari wa barabarani akitekeleza wajibu wake wa kisheria na wewe dereva unayo haki ya kutetea haki zako za kisheria. Hakuna aliye juu ya mwingine kwani anatekeleza wajibu nawe unalinda haki.
3. SAID MWEMA AKATAZA KUNYANGANYWA LESENI.
Mkuu wa jeshi la polisi mstaafu ndugu Saidi Mwema aliwahi kuandika kukemea hatua ya madereva kunyanganywa leseni. Katika kijarida alichokiita UMESIMAMISHWA NA POLISI UKIWA UNAENDESHA ?, ZIJUE HAKI NA WAJIBU WAKO, ndugu mwema ameandika akisema kuwa ofisa wa polisi hana haki ya kuchukua leseni ya dereva.
4. HAIRUHUSIWI KUBANDUA BIMA/ AU KIBANDIKO( STICKERS) KINGINE CHOCHOTE.
Wakati mwingine askari wa barabarani huamua kubandua bima au vibandiko vingine ( stickers) kwa lengo la kumfanya dereva amfuate au malengo mengine yoyote. Hili nalo ni kosa kwakuwa haliainishwi popote katika sheria. Jambo ambalo halikuruhusiwa na sheria kulitenda kwake ni kosa. Ieleweke kuwa askari wa barabarani haruhusiwi kubandua stika yoyote katika gari lako wala kuichukua.
5. UKIONEWA NA ASKARI WA BARABARANI CHUKUA HATUA HIZI.
Ili uweze kumchukulia hatua vizuri askari ni vema ukijua jina lake, cheo chake, na kituo anachotokea. Katika kuyajua haya ni lazima watu wajue kuwa ni haki yako kumuuliza askari taarifa hizi. Sio dhambi wala kosa ila ni haki kumuuliza askari taarifa hizi. Na kwa askari ni wajibu kukueleza taarifa hizi. Haijalishi mmeshatofautiana wala nini isipokuwa ni wajibu akupe taarifa hizi. Lakini ushauri ni kuwa ni vema zaidi askari anapokusimamisha tu kabla ya kujadili lolote kumuuliza au kumuomba ajitambulishe ili hata mkishatofautiana mbeleni iwe rahisi kwako kuchukua hatua.
Kiutaratibu inatakiwa askari ajitambulishe kwako bila wewe kumuuliza na kabla ya kuzungumza lolote lakini kwakuwa hawafanyi hivyo ndio maana wewe unalazimika kumuuliza. Baada ya kupata taarifa hizo peleka malalamiko yako kwa mkuu wa kituo anachotokea halafu fuatilia. Atachukuliwa hatua wala huna haja ya kulihofi hilo. Jeshi la polisi ni sehemu ambako nidhamu inazingatiwa kuliko pahali pengine popote hivyo unapomripoti askari ni lazima ashughulikiwe.
Kwa taarifa yako askari wanaogopa sana kuripotiwa kwa wakubwa zao kuliko watumishi wengine wowote wa umma unaowajua, hili nakupa. Na askari yoyote mwenye kujitambua akijua unalenga kumripoti ni lazima akubali myamalize. Basi usiishie kulalamika kwani kulalamika hakusaidii chukua hatua ili iwe funzo kwa wengine kesho na mbeleni.
MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com