NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Friday, August 14, 2015

JWTZ YAKANUSHA KUWANYANG'ANYA KADI ZA KUPIGIA KURA MAOFISA NA ASKARI WAKE
Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Ngemela Lubinga (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi wakati akikanusha jeshi hilo kuwanyang'anya kadi za kupigia kura maofisa na askari wake kama ilivyodaiwa na kiongozi mmoja wa chama cha siasa. Kulia ni Msaidizi wa Kanali Lubinga, Meja Joseph Masanja na kushoto ni Kapteni Swaleh Omari.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale

JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ), limekanusha kuwanyang'anya kadi za kupigia kura maofisa na askari wake kama ilivyodaiwa na mmoja wa viongozi wa chama kimoja cha siasa na kutolewa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.


Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Kanali Ngemela Lubinga alisema madai hayo siyo ya kweli na  kuwa jeshi hilo halijafanya hivyo na wala haliwezi kufanya hivyo.

"Wanajeshi hawaruhusiwi kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa na kuwa mwanajeshi haruhusiwi kuwa shabiki wa chama chochote cha kisiasa.
Lubinga alisema Jeshi la Wananchi Tanzania linafanya kazi zake kama 'professional state organ duniani na kuwa mwanajeshi anayekiuka huchukuliwa hatua za kinidhamu za kijeshi wala si za kiraia. Alisema Jeshi la Wananchi Tanzania limesikitishwa na kauli hiyo iliyotolewa na kiongozi huyo.

"Wananchi na viongozi wa kisiasa mnaombwa mfanye kazi zenu za kisiasa na zisianzishwe hoja nje ya maeneo hayo ya kisiasa kwani lugha hizo za upotoshaji zinaweza kuleta hofu, ukakasi na wasiwasi kwa wananchi" alisema Kanali Lubinga.

Kanali Lubinga alisema jeshi hilo linaendelea na shughuli zake kama kawaida halipendi litolewe kauli za upotoshaji, kusikoeleweka ufuatwe utaratibu wa kuuliza kupata majibu ya uhakika kwani wananchi wanaimani na jeshi lao.