NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Friday, February 27, 2015

Mwanamke Auawa na Mumewe Kwa Kipigo na kisha Mwili wake Kufukiwa katika Zizi la Ng'ombe


Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Ubetu Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, amefariki dunia baada ya kupigwa na mume wake sehemu mbalimbali za mwili na kisha kuzika mwili wake kwenye boma la ng'ombe.
 
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo lilitokea Februari 25 mwaka huu saa 11:45 jioni.
 
Akieleza mazingira ya tukio hilo, Kamanda Kamwela, alisema siku ya tukio jirani na familia hiyo alipigiwa simu na mume wa marehemu na kumwambia ameuwa mkewe na kumtelekeza ndani ya bomala ng’ombe.
 
Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo aliyeuawa ametajwa kuwa ni Jenipher Peter (45). Alisema alikuwa akiishi na mume wake, Peter Mrosso (43) pamoja na watoto wao watatu. Alisema mwili wake ulifukiwa ndani ya boma la ng'ombe.
 
Kamanda alisema taarifa za mauaji ya mwanamke huyo ilitolewa baada ya jirani yake kupigiwa simu na mume wa marehemu, akimtaarifu kuwa amemuua mkewe na maiti ameifukia ndani ya boma la mifugo

Thursday, February 26, 2015

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Aua Mwanafunzi Mwenzake Darasani Wakati Wakigombania Daftari la Notes



Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Ilola iliyopo katika wilaya ya Shinyanga vijijini aitwaye Veronica Venance mwenye umri wa miaka 12 amefariki dunia kwa kupigwa na mwanafunzi mwenzake wakati wakigombania daftari darasani kwa ajili ya kuandika notes.

Walioshuhudia tukio hilo wamesema limetokea Februari 24 mwaka huu, saa 7 na nusu mchana katika darasa la tano katika Shule ya Msingi Ilola iliyopo katika Kata ya Ilola, Tarafa ya Itwangi, Wilaya ya Shinyanga.

Wamesema mwanafunzi huyo amefariki dunia baada ya kupigwa makofi na ngumi sehemu za kichwani na mwanafunzi mwenzake aitwaye Sophia Mathew (12).

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Andrew Chenge Agoma Kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma.....Adai kuna zuio la mahakama kuu, hatima yake kujulikana leo


MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Mtemi Andrew Chenge, jana ameonyesha utemi wake mbele ya Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, baada ya kusema haiwezi kumjadili kwa sababu kuna kesi mahakamani.
 
Alisema kuna zuio la Mahakama Kuu ambalo limevitaka vyombo vyote vya Serikali kutojadili suala la miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.
 
Tume hiyo inamtuhumu mbunge huyo kuwa alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitumia madaraka yake vibaya katika uuzaji wa hisa za Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwenda Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited.
 
Itakumbukwa wakati suala la Tegeta Escrow likijadiliwa bungeni, Chenge alidaiwa kupewa sh bilioni 16 na mmiliki wa VIP Engineering Tanzania Limited, James Rugemalira.
 
Jana, kabla ya Chenge kuieleza Tume ya Maadili kuwa haiwezi kumuhoji, Mwanasheria wa tume hiyo, Hassan Mayunga, alisoma mashtaka yanayomkabili.
 
“Mlalamikiwa akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwaka 1995 aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 wa kuongeza uzalishaji wa umeme na Kampuni ya IPTL.
 
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye Kampuni ya IPTL.
 
“Kitendo cha kuingia mkataba na Kampuni ya VIP ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(i) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha katika utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kwa masilahi binafsi,” alisema Mayunga.
 
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri wa Kampuni ya VIP huku akiwa na wadhifa wa ubunge, ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(e) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgogoro wa kimasilahi.
 
Mayunga alisema mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na VIP, ulimpatia masilahi ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume na kifungu cha 12(1)(e) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
 
“Mwaka 2014 mlalamikiwa aliingiziwa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 na kampuni hiyo katika Benki ya Mkombozi wakati hakutamka mapema kama aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali na kwamba ana masilahi binafsi na kampuni hiyo wakati alikuwa akijua kuwa Shirika la Umeme (Tanesco) lina mgogoro na IPTL,” alisema. Chenge
 
Baada ya kusomewa mashtaka, Chenge aliyakana na kuomba mwongozo kwa madai kuwa suala hilo lina zuio la Mahakama Kuu, hivyo basi tume hiyo haiwezi kujadili suala hilo hadi kesi ya msingi itakapokwisha.
 
“Napata shida kujadili suala hili, mimi nikiwa kama mwanasheria linanisumbua kidogo, kutokana na umahiri wako jaji, ninaomba upitie zuio lililotolewa na Mahakama Kuu kwa kina ili uweze kuangalia kisheria, je inaruhusiwa kujadili au la,” alisema Chenge.
 
Baada ya majadiliano hayo, Mwanasheria Mayunga alisema amri ya mahakama haihusiani na kazi za baraza kwani katika oda ya mahakama, hakuna kipengele cha kuzuia kujadili suala hilo.
 
“Ibara ya 132 ya sheria ya mwaka 1987, ibara ndogo ya kwanza ambayo inaeleza kuwa kutakuwa na sekretarieti ya maadili ya utumishi wa umma ya kuchunguza mienendo ya viongozi na watumishi wa umma.
 
“Taasisi hii ni huru na kwamba inafanya kazi endapo kuna taarifa ya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi katika suala la rushwa au kutumia madaraka yao vibaya,” alisema Mayunga.
 
Baada ya kusema hayo, Mwenyekiti wa barza hilo, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alihairisha shauri hilo na kusema watapitia zuio la mahakama hiyo ili waweze kuangalia kama ni kweli linaweza kuwazuia kufanya kazi zao au la na leo waweze kutoa uamuzi.
 
“Tumeomba muda kidogo ili tuweze kuipitia hii oda ya mahakama na kuiangalia kwa umakini kama ni kweli inatuzuia tusijadili suala hili au la, leo tutatoa uamuzi kamili,” alisema Jaji Msumi.
 
Aliongeza kutokana na hali hiyo, baraza hilo linapitia hoja ya mlalamikiwa na mlalamikaji ili kuangalia mambo ya kisheria yanayohusu kujadili au kutokujadili suala hilo.
 
Chenge akiwa nje ya Ukumbi wa Karimjee ambako mashauri hayo yanasikilizwa, waandishi walitaka kusikia maoni yake juu ya suala hilo na yeye akawajibu: “Andikeni kama mlivyoona na kusikia.”
 
Mbunge huyo alifika katika viwanja vya Karimjee saa 3:00 asubuhi kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri lake saa 3:15 baada ya jopo la majaji na mwenyekiti wa baraza hilo kuwasili.
 
Baraza hilo pamoja na kutolea uamuzi wa shauri la Chenge wa kusikilizwa au kutosikilizwa leo, pia linatarajia kumuhoji Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kwa siku mbili – leo na kesho.
 
KASHFA ZA CHENGE
Chenge ametajwa kuhusika katika kashfa mbalimbali, zikiwamo za rada, ajali iliyoua watu wawili na uchotwaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Rada
Chenge alitajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada, ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri.
 
Rada hiyo ilinunuliwa kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa dola milioni 40 mwaka 2001, kiwango kilicholistua Bunge la Uingereza.
 
Katika uchunguzi wa suala hilo, ilibainika kuwa Chenge alikuwa na akaunti kwenye Kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya dola milioni 1 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.8) hali iliyofanya ashinikizwe kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa miundombinu.
 
Ajali iliyoua wawili
Wakati kashfa ya rada ikiendelea, Chenge alihusika katika ajali iliyoua wanawake wawili mmoja akitajwa kuwa mtu wake wa karibu.
 
Baada ya ajali hiyo, alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha gari kizembe na bila kuwa na bima.
 
Alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 700,000 ambazo alilipa.
 
Tegeta Escrow
Mwaka jana alijikuta kwenye kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambapo alidaiwa kuchotewa Sh bilioni 1.6.
 
KAULI TATA
1. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.8 za rada, alisema ‘Ni vijisenti’.
 
2. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.6 za Escrow, alikuja na kauli mbili: “Mimi ni tumbili, hata kwenye hii (kashfa ya Escrow)” na “Mimi ni nyoka wa makengeza, nawatafutia wananchi fedha.”
 
3. Wakati wa kelele za kumtaka Chenge na wenzake kujivua gamba, mbunge huyo alisema: “Gamba limevuka limeishia kiunoni”.
 
4.Ashauri waliohusika na kashfa ya Escrow, mamlaka ya uteuzi (Rais) iwashughulikie na wapinzani wakaungana naye, lakini CCM wakagoma.
 
NYADHIFA ALIZOWAHI KUSHIKA
2014: Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya.
2006/15: Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.
2006/08: Waziri wa Miundombinu.
2006: Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
1993-05: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1991-93: Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1972-73: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM

Waliomuiba Mtoto Albino Pendo Wakamatwa Jijini Mwanza


Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, amesema watu wote waliohusika ‘kuiba’ mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino) Pendo Emmanuel (4) katika kijiji cha Ndami wilayani Kwimba, Mwanza, wamekamatwa.

Akizungumza wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya wa mkoa huo jana, Manju Msambya (Misungwi), Zainab Rajab (Sengerema) na Pili Moshi (Kwimba), Mulongo alisema watu wote waliohusika wamekamatwa na hivi sasa bado hawafahamu kama mtoto huyo yupo hai ama mfu.
 
“Wezi wale baada ya kumuiba mtoto Pendo walimleta katika hoteli moja hapa jijini Mwanza, kisha kuwakabidhi watu walionekana wanunuzi, lakini wote hao wamekamatwa akiwamo mmiliki wa hoteli hiyo,” alisema Mulongo.
 
Alisema serikali ipo kazini wakati wote, ndiyo maana inafanya kazi usiku na mchana kuwasaka watu wote waovu mkoani Mwanza ambao hawawezi kusalimika kwa kile watakachokifanya.
 
Hata hivyo, alisema watu hao waliofanya uhalifu huo akiwamo baba wa mtoto huyo, Emmanuel Shilinde, wanashikiliwa na polisi huku mtu wa mwisho aliyetoweka na mtoto huyo toka hotelini hapo akiendelea kutafutwa.
 
Mulongo hata hivyo hakuweza kuitaja hotel wala mmiliki wake na wangine waliohusika na tukio hilo lilitokea Desemba 27 mwaka jana, lakini Shilinde akituhumiwa kuhusika zaidi na tukio hilo kutokana na kuamua kufanya hivyo kwa sababu alikuwa ana watoto wawili albino.
 
Mkuu wa mkoa huyo aliwataka wakuu wa wilaya wapya, kuhakikisha kushughulikia changamoto za wapiga ramli, kuangalia utoaji wa vibali kwa waganga wa jadi ili kudhibiti matukio ya utekaji na mauaji ya albino.
 
Hata hivyo, alishangazwa na maneno yanayotolewa na watu kuhusiana na mauaji hayo kuwa yanatokana na masuala ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu.
 
Katibu wa chama cha maalbino mkoa wa Mwanza, Mashaka Tuju, aliishutumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua stahili tangu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yalipoanza miaka tisa iliyopita.
 
Amesema kwa miaka tisa serikali inahangaika na kudai inachukua hatua lakini hakuna hatua yoyote inayoonekana mpaka sasa huku albino wengi wakiwa wanaishi vijijini katika nyumba zisizo na ulinzi thabiti, lakini utakuta viongozi wa serikali wanaenda huko pale linapotokea tatizo la mauaji ya watu hao.
 
Tuju amewashambulia mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza, Antony Diallo, naibu waziri wa nishati na madini, Charles Kitwanga na mbunge wa Magu, Dk. Festus Limbu, kwa kushindwa kufanya juhudi zozote za kuwalinda na kuwatetea albino.
 
Katika kipindi cha miezi miwili, watoto Pendo Emmanuel wa Kwimba na Yohana Bahati (mwaka mmoja) wa kijiji cha Ilelema Chato, walitekwa na watu wasiojulikana.

Tuesday, February 24, 2015

Warioba Ashutumu Ubinafsi wa Vyama vya Siasa Katika Mchakato wa Kura ya Maoni


Waziri Mkuu mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba amevitaka  vyama vya siasa kuzingatia matakwa ya wananchi katika suala zima la Kura ya Maoni  ya Katiba Inayopendekezwa na badala ya kuwagawa.

Aidha, Warioba amesema anaamini baadhi ya vipengele vilivyokataliwa katika Rasimu ya Katiba, ipo siku  vitafanyiwa kazi kuondoa migongano huku akisisitiza, kisheria kura ya maoni  siyo mwisho wa mchakato.
 
Warioba alisema kwa  sasa,  badala ya kuwaweka wananchi  pamoja na kukubaliana wanachotaka , upo mvutano huku wengine wakitaka Katiba Iliyopendekezwa ikubaliwe na wengine wakitaka wananchi waikatae.
 
“Kwa suala hili la kundi la Ukawa kuwasihi wafuasi wake kutoshiriki katika upigaji kura ya maoni, inaonyesha dhahiri hakuna maridhiano na wananchi kwani badala ya kujua matakwa yao,  vyama vya siasa vinawagawa wananchi katika suala hilo jambo ambalo linaonyesha vyama hivyo vinajitazama vyenyewe,” alisema.
 
Alikuwa akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.
 
Alisema suala la kupiga kura ya maoni ni kuangalia maridhiano na wananchi na si vyama vya siasa. Alisema hata katika mchakato wa awali,  waliangalia maridhiano ya  wananchi na walihakikisha maoni yao yanaingia kwenye Katiba pendekezwa.
 
Alisema vyama vya siasa vinataka maridhiano yao bila  kuangalia matakwa ya wananchi na kukubaliana jambo, alilosema ni tatizo.
 
Alisisitiza kwamba anaamini baadhi ya vipengele vilivyokataliwa, ipo siku vitafanyiwa kazi kuondoa migongano.
 
Alisema katika Katiba Inayopendekezwa, suala la mgawanyo wa madaraka halijaainishwa lakini anavyoona maendeleo katika dunia  na matatizo, ipo siku lazima madaraka yatenganishwe, kwani kutakuwa na migongano kati ya Serikali na Bunge.
 
Alisema ingawa masuala hayo hayajaingizwa katika Katiba Inayopendekezwa, kama ilivyokuwa kwenye rasimu iliyoandaliwa na Tume aliyokuwa akiiongoza,  anaamini kutakuwa na mabadiliko kabla ya kura ya maoni au baada kwa kuwa hayaepukiki.
 
 “Matatizo haya ya wazi ya masuala kama ya mgongano wa madaraka na Muungano yatafanywa kabla au baada ya kura ya maoni kwani kuna mambo katika Katiba pendekezwa hayawezi kutekelezwa na hayazungumziki,” alisema.
 
Akizungumzia suala la maadili,Warioba alisema sheria ya maadili ipo, lakini haina nguvu kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine.  Alitoa mfano wa Ufilipino akisema walikuwa na sheria hiyo lakini wakaweka kwenye katiba iwe rahisi kutekelezwa. Alitaja pia  Namibia  na  Kenya.
 
Alisema suala la mgawanyo wa madaraka bado ni muhimu kwani kwa kutenganisha, kunaweza kusaidia katika uwajibikaji . Alitoa mfano wa sakata la  Tegeta Escrow bungeni na kusema Bunge na Serikali ziliingiliana madaraka badala ya  serikali kuwa na kauli moja.
 
“Hebu angalia suala la Bunge kumfukuza Katibu Mkuu, hii siyo kazi yake, lilichanganya madaraka, kama Bunge haliridhiki na mwenendo wa serikali haliwezi kwenda kufukuza watumishi wa serikali. Bunge linatakiwa kusema kutokuwa na imani na serikali na siyo kufurahia kusema fulani afukuzwe. Siyo utaratibu mzuri,” alisema.
 
Waziri Mkuu huyo mstaafu alisema kazi ya Bunge ni kusimamia serikali na siyo kufukuza watu, kwani wakati mwingine kunakuwa na suala la visasi na kufukuza watumishi ambao hawahusiki.
 
Kuhusu Muungano, alisema,  “Hili jambo ni ‘serious’(nyeti) lazima kufika wakati kuwa na nchi moja na hata kuangalia jinsi ya kuweka sawa suala la muundo wa serikali.”
 
Alisisitiza  msimamo wake kwamba yeye ni muumini wa Muundo wa serikali mbili kwenda moja na siyo muumini wa serikali tatu. Alipendekeza kwenda hatua kwa hatua hata baada ya miaka 100 kupata serikali moja.
 
Warioba alisema  siku ya  kupiga kura ya maoni, inaweza kubadilishwa kwani haiko kisheria na haitaathiri mchakato wa kupata Katiba mpya.
 
Alisema tarehe ya kupiga kura, imewekwa na wanaohusika na inaweza kuahirishwa kwa kadri wanavyoona maandalizi yamekamilika katika kuandikishwa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wanajeshi 6 wa JTK Waliotaka Kuandamana Wafikishwa Mahakamani Chini ya Ulinzi Mkali

Wanajeshi 6 wa JTK Waliotaka Kuandamana Wafikishwa Mahakamani Chini ya Ulinzi Mkali


Wahitimu sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko usio halali.

Washitakiwa hao ni Mwenyekiti wa Umoja wa wahitimu hao George Mgoba, Makamu Mwenyekiti Parali Kiwango, Katibu Linus Steven na wahitimu wengine Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob Mang’wita.
 
Wote walikana mashitaka  na kurudishwa rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi yao.
 
Walifikishwa mahakamani hapo asubuhi na kupandishwa kizimbani saa 10 kasoro jioni, wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali na kushawishi wenzao kutenda kosa la jinai.
 
Wakili wa Serikali,  Nassoro Katuga akisaidiwa na Tumaini Kweka, Hellen Moshi, Janethroza Kitali na Inspekta Jackson Chidunda,  alidai mbele ya Hakimu Mkazi,  Frank Moshi kuwa Februari 15 mwaka huu katika eneo la Msimbazi Centre, Ilala Dar es Salaam, washitakiwa walipanga njama za kutenda kosa.
 
Alidai siku hiyo katika eneo hilo, walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kuandamana kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na lingesababisha uvunjifu wa amani.
 
Katika mashitaka yanayomkabili Mgoba, Kiwango na Steven, wanadaiwa siku hiyo katika eneo hilo, walishawishi wahitimu wenzao wa mafunzo ya JKT, kufanya maandamano kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi wa umma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
 
Walikana  mashitaka yanayowakabili na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika. DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya washitakiwa hao, chini ya kifungu cha 148 (4) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
 
Hakimu Moshi alisema washitakiwa watarudi rumande hadi Machi 6 kesi itakapotajwa kwa kuwa DPP amefunga dhamana yao kwa muda mpaka atakapoona inafaa, hivyo Mahakama haiwezi kutoa masharti ya dhamana.
 
Awali, Makamu Mwenyekiti wa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Parali Kiwango (25) mkazi wa Temeke Mikoroshini alijisalimisha Makao Makuu ya Polisi, kwa Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi.
 
Amri ya kumtaka kiongozi huyo kujisalimisha ilitolewa juzi na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova

Bunduki ya kivita na risasi 524 zakamatwa Kibondo


Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma ACP Jafari Mohamed amesema, risasi 524  na bunduki moja  ya kivita aina ya SMG zimekamatwa katika eneo la kijiji cha Nduta baada ya polisi katika kizuizi cha Nduta kufanya ukaguzi ndani ya basi.
 
Wakati kazi hiyo ikiendelea  mtu anayesadikiwa kumiliki begi lililokuwa na risasi na bunduki alitoroka, ambapo amesema vizuizi vya barabarani vilivyowekwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kigoma vimesaidia kukamata wahalifu na silaha zinazosafirishwa mara kwa mara.
 
Pia ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali wilayani Kibondo kwa kutoa pikipiki tatu kwa jeshi la polisi.

Kwa upande wake aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kibondo Venance Mwamoto, ambaye amehamishiwa wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, amewataka wananchi kutoa ushirikiano na kuisadia serikali kuimarisha ulinzi kwa kuwa jukumu la ulinzi ni la wananchi wote.