NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Monday, February 23, 2015

Chenge, Tibaijuka Kikaangoni Baraza la Maadili Wiki hii


Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge Jumatano atasimama mbele ya Baraza la Maadili kujibu tuhuma za kukiuka maadili ya uongozi na kujipatia Sh bilioni 1.6 ambazo aligawiwa kutoka katika fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

Profesa Anna Tibaijuka ambaye alitimuliwa Uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi kutokana na kujipatia Sh bilioni 1.6 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira atajibu tuhuma hizo Alhamisi.
 
Ratiba iliyotolewa na Baraza la Maadili, jijini Dar es Salaam inaonesha kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, William Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, atasimama mbele ya Baraza hilo Jumatatu ijayo.
 
 Wengine watakaopanda kizimbani ni Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma atakayehojiwa Jumatatu ijayo.
 
Wengine ni  Mnikulu Shaban Gurumo atakayehojiwa  Machi 4, akifuatiwa na  Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip  Saliboko na  Machi 6 atahojiwa Naibu Kamishna  Upelelezi na Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania  (TRA), Loicy Appollo.
 
Ratiba hiyo inaonesha kuwa Machi 9 atahojiwa Mkurugenzi  Mdhibiti  Uchumi Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Dk Benedict Diu akifuatiwa na Meya wa Halmashauri ya  Manispaa ya Tabora, Gulam Remtullah.
 
Akizungumza Dar es Salaam,  Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Hamis Msumi alisema ratiba ya kuwahoji viongozi, ilitakiwa kuanza jana ikianza na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya  Korogwe, Mrisho Gambo. Hata hivyo, Gambo aliwasilisha barua kwamba anaumwa na atashindwa kuhudhuria.
 
Vievile,  Gambo aliwasilisha cheti cha daktari akitakiwa kupumzika kwa wiki mbili, jambo lililosababisha Baraza hilo kuahirisha kusikiliza shauri lake  hadi hapo litakapopanga kikao kingine.
 
Kutokana na kuanza kuwapandisha kizimbani watuhumiwa  wa sakata la Escrow, Baraza litatoa uamuzi wa ama wahusika hao wafikishwe mahakamani, au la, kulingana na hatia watakazokutwa nazo. 
 
Kashfa ya Escrow iliyonguruma mwaka jana bungeni, imesababisha baadhi ya watuhumiwa kujiuzulu nyadhifa zao na wengine kuvuliwa madaraka, akiwamo Profesa Tibaijuka aliyewekwa pembeni na Rais Jakaya Kikwete Desemba mwaka jana. 
 
Chenge alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na aliachia wadhifa huo hivi karibuni. Ngeleja aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mbunge wa Lupa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini , Victor Mwambalaswa, nao walijiuzulu hivi karibuni. 
 
Chenge na Profesa Tibaijuka kila mmoja alipata mgawo wa Sh bilioni 1.6 huku Ngeleja akipata Sh milioni 40.4 kutoka kwa James Rugemalira wa VIP Engineering and Marketing Limited, zikiwani mgawo wa Tegeta Escrow.
 
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2006 kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya tozo ya uwekezaji (capacity charges), zilizokuwa zinalipwa na  Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kabla hazijakabidhiwa kwa anayelipwa, ambaye ni Kampuni binafsi ya kufua umeme ya IPTL.
 
 Kabla ya hapo Tanesco ilikuwa inalipa moja kwa moja kwa IPTL.   Ilifunguliwa  ili kutoa nafasi kwa pande hizo mbili kumaliza tofauti zao kuhusu kiwango cha tozo hiyo.

Radi Yaua Mwalimu na Wanafunzi 6 Kigoma


Watu saba wakiwamo wanafunzi sita wa darasa la nne katika shule ya msingi Nyakasanda na Mwalimu wa shule hiyo, Anderson Kibada wamekufa baada ya kupigwa na radi huku watu wengine 11 akiwemo Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Laurence Sesegwa (42) wakijeruhiwa.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kigaga Daga alisema kuwa watu hao walifikwa na mauti hayo kufuatia mvua kubwa zilizonyesha zikiambatana na radi zilizoanza majira ya saa tano asubuhi zilizotokea katika kijiji cha Nyachenda wilaya ya Kasulu mkoani.
 
Mbali na Mwalimu Kibada aliyekufa hapo hapo, Mganga huyo Mkuu wa Wilaya aliwataja wanafunzi kuwa ni pamoja na Mary Steven (11), Severine Mussa (11) na Joseline Joseph (12). 
 
Aliwataja wanafunzi wengine waliofariki kuwa ni Joyness Simon (14), Nehemia Kepha (14) na Robin Gabriel (14).
 
Alisema kuwa hadi sasa wanafunzi wanne wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu ambao aliwataja kuwa Fadhila Emanuel (13), Matilda Moses (11), Bizimana Manjo (12) huku wanafunzi wengine saba wakiruhusiwa baada ya hali zao  kuwa nzuri.

Albino Wawaliza Maaskofu 10 na Mashehe 10 Katika Hospitali ya Bugando


Viongozi wa madhehebu ya dini jijini Mwanza, wakiwamo Maaskofu na Mashehe jana walijikuta wakibubujikwa na machozi baada ya kumtembelea Ester John, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Ester amelazwa  baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika, ambao walimteka mwanawe mwenye ulemavu wa ngozi  (albino), Yohana Bahati na kutokomea naye kusikojulikana.
 
Viongozi hao  wakiwemo maaskofu 10 na mashehe 10 walimtembelea Ester hospitalini hapo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano kubwa la amani linalotarajiwa kufanyika Februari 28 mwaka huu kuiombea nchi amani na kulaani mauaji ya albino.
 
Mashehe na maaskofu hao walimuombea dua na sala Ester aweze kupona haraka na  walilaani kitendo cha kinyama, alichofanyiwa na wauaji hao.
 
Waliiomba Serikali ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
 
Akizungumza hospitalini hapo huku akitokwa na machozi katika Wadi Namba 9 alikolazwa Ester, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa ya Viongozi wa Dini, Shehe Hassan Kabeke alisema wanaungana  kwa pamoja kulaani matukio mawili ya kinyama ya kuuawa kwa mtoto Yohana na kujeruhiwa vibaya mama yake mzazi.
 
“Maneno ya kusema yananiishia baada ya kumuona Ester, mimi nadhani hakuna sababu ya kuremba maneno dhidi ya ukatili huu wa kinyama, nasikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu kama kiongozi wa kiroho, tunaitaka serikali katika hili isiondoe adhafu ya kifo kwa kisingizio cha haki za binadamu”, alisema.
 
Aliongeza “Tunapozungumzia haki za binadamu, maana yake ni usawa, ukweli na haki kwa watu wote nchini, haiwezekani watu wengine waue watu halafu tunasingizia haki za binadamu, na wao wahukumiwe adhabu ya kifo, katika hili msimamo wetu kama viongozi wa dini tunaomba adhabu ya kifo isiondolewe”.
 
Pia, aliwataka majaji wanaosikiliza kesi za watu wenye ulemavu wa ngozi, kuzisikiliza kwa wakati ili kuondoa ucheleweshaji wa kesi hizo ili hukumu zitolewe kwa wakati.
 
“Nichukue fursa hii kwa niaba ya wenzangu kuwaomba waheshimiwa majaji waharakishe kusikiliza mashauri yaliyoko mahakamani yanayohusisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino)”, alisema.
 
Kwa upande wake, Katibu Mwenza wa Kamati hiyo ya Amani, Askofu Zenobius Isaya alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),  Ernest Mangu kulichukulia suala la mauaji ya albino kwa uzito wa kipekee kwa vile linagharimu maisha ya watu wasio na hatia katika jamii.
 
“Tunamuomba IGP Mangu alichukulie suala hili kwa uzito mkubwa, afanye uchunguzi wa kina ili aweze kukomesha mauaji haya ambayo yameipaka matope nchi yetu mbele ya Jumuiya ya Kimataifa”, alisema.
 
Akitoa salaam kwa Ester ambaye aliweza kukaa kitandani kwa muda, Isaya alisema shida iliyomkuta ni shida ya Watanzania wote wenye kupenda amani na kuchukia maovu.
 
“Shida iliyokukuta na taabu yako ni taabu yetu sisi sote wapenda amani ; na sisi wapenda amani kwa wingi wetu, kama unavyotuona, tunalaani tukio hili la kinyama, jambo hili ni la kinyama lakini tunakutia moyo uweze kupona haraka na Mungu akupe moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.
 
Aliushukuru uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kufanya kazi kwa uvumilivu na kutanguliza upendo katika kumhudumia Ester tangu alipolazwa hospitalini hapo Februari 17 mwaka huu.
 
“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana madaktari na wauguzi wetu kwa kuwa bega kwa bega na Ester kwa kumhudumia bila ya kuchoka, hii inaonyesha kuwa na mshikamano na Mungu awabariki”, alisema.
 
Awali, akiupokea ujumbe huo, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Hospitali ya Bugando, Leah Kagina aliwashukuru viongozi hao wa dini kwa kuamua kutenga sehemu ya muda wao kwa kwenda kumjulia hali.
 
Alisema hiyo ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kupokea ujumbe huo mkubwa kwenda kumjulia hali Ester.
 
“ Tunawashukuru sana kwa ujio wenu,  ni kwa mara ya kwanza kwa hospitali kupokea ujumbe huu mzito wa viongozi wa kiroho kwa ajili ya kuja kumjulia hali Ester, hii inadhihirisha ni jinsi gani mlivyo na upendo kwa watu wote, rai yangu kwenu niwaombe mtumie ibada zenu katika kutoa elimu kwa jamii dhidi ya mauaji haya”, alisema.
 
Alisema kuwa viongozi wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya imani potofu, ambazo zimekuwa zikienezwa dhidi ya mauaji hayo na kuitaka serikali kuwachukulia hatua stahiki wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi.
 
Akizungumzia hali ya mgonjwa, Muuguzi wa Zamu katika wadi Namba 9, alikolazwa Esta, Adolphina Kishumba alisema hali ya Ester kwa sasa inaendelea vizuri na anajitahidi kula chakula.
 
“Kwa hivi sasa hali ya Ester inaendelea vizuri, ni tofauti na alivyokuwa mwanzo na sasa hivi anakula na anaanza kutembea kwenda chooni”, alisema.
 
Mama mzazi wa Ester ambaye anamuuguza hospitalini hapo, Tabu Mang’enyi aliwashukuru Watanzania kwa misaada yao ya hali na mali wakati wote, ambao amekuwa na mwanawe hospitalini hapo.
 
“Nawashukuru Watanzania wote kwa kumuombea mwanangu na kuendelea kumjulia hali. Kutokana na maombi yenu hali ya mwanangu inaendelea vizuri”, alisema.

Mbatia Aikosoa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ifundi......Asema huo ni mpango wa Serikali Kuwalaghai Wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu


Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Taifa, James Mbatia (kulia), akionesha kitabu cha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitoa tamko la chama hicho juu sera hiyo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosene Nyambabe na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Musa Kombo Musa.
 Hapa mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Wanahabari wakiwa katika mkutano huo.
Wajumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) ya chama hicho waliokuwepo kwenye mkutano huo. Kutoka kulia ni Honest Mombory, Katibu wa Wazee, Ernest Mwasada, Dk.Nderakindo Kessy ambaye pia pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Angelina Mutahiwa na Esther Komba.
 
*****
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia amesema kuwa uzinduzi wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ni mpango wa serikali kuwalaghai wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakao fanyika Oktoba mwaka huu.
 
Pia amesema hali ya elimu nchini ni kama mgonjwa aliyekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, hivyo serikali isiwe inatoa majibu mepesi kwenye masuala magumu ambayo yanagusa maisha ya watanzania.
 
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitoa tamko la chama hicho kuhusu sera hiyo , Mbatia  alisema kuwa mnamo Januari 31 na Februari mosi mwaka 2013, aliwasilisha hoja bungeni kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu.
 
Alisema kuwa aliorodhesha athari mbalimbali za udhaifu wa wa elimu itolewayo nchini lakini suala hilo lilionekana kutawaliwa na siasa ambapo haikuwa lengo lake,lengo lilikuwa kuhakikisha kuwa sera mbalimbazi za elimu zinaboreshwa.
 
Mbatia aliongeza kuwa mnamo Februari 13, 2015 mwaka huu Rais Jakaya Kikwete, alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 lakini ikiwa haijajibu hoja alizokuwa amezitoa.
 
Alifafanua kuwa wakati Rais akihutubia alisema kuwa sera hiyo ilitumia miaka saba kukamilika, lakini Mwenyekiti huyo alisema baada ya kuipitia alibaini sera hiyo kuwa na lugha ngumu huku ikiwa na makosa mengine mengi.
 
Mbatia alisema anachokiona kwa serikali kuzindua sera hiyo mwaka huu ni mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu,kwani yaliyomo ndani ya sera hiyo yamelenga kuwalaghai wapiga kura.
 
Aidha alisema mambo hayo ni pamoja na kutangaza kuwa elimu ya msingi kutolewa bure bila karo na lugha iliyotumika inawachanganya watanzania hivyo ni vigumu kwa wananchi wa vijijini ambao wengi wao hawana elimu kutambua yaliyoandikwa ndani ya sera hiyo.
 
"Mfano sera mpya ina matamko mawili ambayo  inawachanganya watanzania kuhusu lugha ya kufundishia,moja inatamka Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia ngazi zote za elimu,na ya pili inatamka kuwa Kingereza kitatumka kama lugha ya kufundishia katikan ngazi zote za elimu.
 
"Matamko haya mawili, kwanza yanakwepa lawama zinazotokana na malumbano ya muda mrefu kuhusiana na lugha gani inafaa kufundishia, pili imehalalisha mifumo miwili ya elimu ndani ya nchi moja" alisema Mbatia kwa msisitizo 
 
Hivyo alisema serikali ilipaswa kutengeneza sera ambayo inazungumza kwa uhakika kuhusu suala la lugha ya kufundishia, kuliko kutoa tamko la sera lisilo na msimamo.
 
Aliweka wazi kuwa wanapendekeza iundwe tume ya kudumu ya elimu nchini itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine kuhakikisha ubora wa elimu unapatikana nchini.
 
Vilevile alisema wanaiomba serikali kupitia upya sera hiyo kabla haijaanza kutumika ili kuepusha taifa na madhara ambayo yameonesha dalili za kutokea hata kabla haijaanza kutumiaka.

Saturday, February 21, 2015

Mwanamke Amkata Mpwa Wake Sehemu za Siri Huko Ruvuma


Mtu mmoja wa Kijiji cha Majimaji Ruvuma, Patrick Vitus amekatwa sehemu zake za siri  na kuachwa zikining’inia. 
 
Ofisa Mtendaji Wa Kijiji hicho Hussein Mkali amesema Partick alikatwa sehemu zake za siri na mpwa wake Zainabu Saidi baada ya kumkatalia kwenda kumfuata mume wake anayeitwa Musa Said ambaye alikuwa kwa mke mdogo.
 
Baada ya kufanya tukio hilo Ofisi ya Kijiji ilimkamata Zainabu na kumpeleka katika kituo cha Polisi, huku Patrick akipelekwa Hospitali ya Tunduru kwa ajili ya matibabu.

Thursday, February 19, 2015

Uteuzi wa Paul Makonda Kuwa Mkuu wa Wilaya Wapingwa Kila Kona.....Anatuhumiwa Kumpiga Warioba na Kumtusi Lowassa Hadharani


Uteuzi wa Makonda ambao umefanywa na Rais Kikwete, unaonesha kuwashitua wengi; hali ambayo imefanya watu wengi kumbeza hasa kupitia mitandao ya kijamii.
 
Baadhi ya wanaobeza, wanadai kwamba Makonda hana sifa ya kuongoza wilaya kubwa kama Kinondoni, ambayo ina changamoto na migogoro mingi ya ardhi.
 
Makonda ambaye ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM, jina lake limekuwa kubwa hivi karibuni baada ya kutuhumiwa kumpiga  Jaji Warioba wakati wa  mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
 
Pia, kujitokeza kwake hadharani kumpinga Edward Lowassa, kuliongeza jina hilo kuwa maarufu.

Wananchi wakizungumza kwa nyakati  tofauti, baadhi ya wasomaji wa mitandao mbali mbali, wamedai kuwa uteuzi huo wa Rais ni mzuri ila  alikosea kumweka wilaya ya  Kinondoni yenye matatizo chungu mzima ya kiutendaji ikiwemo migogoro ya mipaka, ardhi, wafanyabiashara ndogondogo na mambo mengine ya ndani.

“Tunampongeza Rais kwa kuteua wakuu wapya wa wilaya, ila kwa huyu Paul Makonda kumweka Kinondoni, ameteleza. Hii wilaya inahitaji mtu mwenye uzoefu mkubwa katika uongozi na uadilifu” alisema Sued Musa.

Naye  Albert Chenza  wa  Dar  alikuwa  na  haya ya  kusema: "Ma-DC kama Makonda wapo kwa ajili ya CCM kutetea maslahi ya CCM au wapo kwa ajili ya wananchi kuwasaidia wananchi?
 
"Ikumbukwe DC ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na DSO akiwa katibu wake, sasa mtu kama Makonda ambaye yupo tayari kufanya vurugu yoyote kutetea maslahi ya CCM leo kupewa u-DC wa Kinondoni tutegemee nini uchaguzi mkuu wa Oct 2015?
 
"Ikitegemea kuna mvutano kati ya wapinzani na CCM ambao vyombo vya usalama vinatakiwa kuleta haki na amani, wapinzani wategemee kupata haki au NGUVU zao ndo itakuwa haki yao? Hakika nuru ya amani inafifia Tanzania.
 
"Hii ni kama tupo disco la kukesha ambalo inatolewa CD hii inawekwa ile na zote unahitaji unywe panadol kuzisikiliza." Alisema  Albert  na  kuongeza:

"Ni dhahiri sasa Mzee Warioba na Taasisi ya Mwalimu Nyerere wamemjua adui yao halisi ni nani. Aliyekua mstari wa mbele kumshambulia na kumfanyia fujo Mzee Warioba amepongezwa rasmi  kwa  kupewa  ukuu  wa  wilaya.
 
"Pia imeendelea kujidhihirisha sasa kuwa Ukitaka U-DC wewe mtukane Lowassa kama Nape Nnauye, Mrisho Gambo na Makonda  walivyofanya.
 
"Na pengine atakayekua jasiri vya kutosha na kumchapa angalao vibao viwili usoni anaweza kupata Ukuu wa Mkoa au Ubalozi kabisa"
  
Sailas Kassa Edward  yeye  anamaoni  tofauti  kidogo, na hapa  anaanza  kwa kumpongeza Makonda: "Siku ya jana (juzi) Rais kikwete alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya ambapo moja ya wateule ni paul Makonda. 
 
"Inanishangaza sana kutoka jana(juzi) mpaka leo(jana) watanzania wamekuwa wakilalamika kupitia mitandao ya kijamii wakikosoa uteuzi wa ndgu makonda. 
 
"Mimi binafsi nampongeza kwa nafasi aliyopata nadhani katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania haijampa rais mamlaka ya kuwatenga watu bali kila mtu ana haki ya kuongoza na pia kuongozwa. 
 
"Kwa watanzania itafika hatua kila mtu mwenye intrest za chama cha mapinduzi hamtaki apate nafasi je nani ana haki na nani hana?
 
"Nimejaribu kuchunguza haya yote yanatoka wapi mpaka makonda anakuwa gumzo mtaani nikagundua kuwa wapenzi wa Edward Lowassa wameumia sana kuona makonda anakuwa mkuu wa wilaya hasa ukizingatia anafichua mbinu na hila za Lowassa na makundi yake. "

BASI LA ABIRIA KIDIA ONE LAUA KWA KUGONGANA USO KWA USO NA LORI ENEO LA CHAMWINO DODOMA


Watu wawili wamekufa papo hapo huku wengine 45 wakijeruhiwa baada ya basi la abiria lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kugongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Vikonje wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 7.05 mchana wakati basi la Kidia lenye namba za usajili T663 AXL kugonga lori lenye namba za usajili T 496 CFG na trela lenye namba za usajili T576 AZX Scania.
 
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea  Dar es Salaam kwenda Mwanza wakati lori lilikuwa likitokea Dodoma kwenda  Dar es Salaam.
 
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa lori, Fadhili Said (36) na utingo wa basi, Chogo Chigunda.
 
Kamanda Misime alisema ajali hilo ilitokea wakati dereva wa basi la Kidia, Adam Robert (34) alipokuwa akilifuata gari lililokuwa likilipita gari la mbele yake.
 
Alisema dereva wa basi baada ya kushindwa kulipita gari lililo mbele yake alikutana na lori lililokuwa likija mbele yake na kusababisha ajali hiyo.
 
Alisema Jeshi la Polisi wanamfuatilia dereva wa basi ambaye anatibiwa majeraha katika moja ya hospitali mjini hapa.
 
Pia alisema majeruhi hao bado walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na wengine wameruhusiwa kurejea nyumbani