NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Monday, February 23, 2015

Albino Wawaliza Maaskofu 10 na Mashehe 10 Katika Hospitali ya Bugando


Viongozi wa madhehebu ya dini jijini Mwanza, wakiwamo Maaskofu na Mashehe jana walijikuta wakibubujikwa na machozi baada ya kumtembelea Ester John, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Ester amelazwa  baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiofahamika, ambao walimteka mwanawe mwenye ulemavu wa ngozi  (albino), Yohana Bahati na kutokomea naye kusikojulikana.
 
Viongozi hao  wakiwemo maaskofu 10 na mashehe 10 walimtembelea Ester hospitalini hapo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kongamano kubwa la amani linalotarajiwa kufanyika Februari 28 mwaka huu kuiombea nchi amani na kulaani mauaji ya albino.
 
Mashehe na maaskofu hao walimuombea dua na sala Ester aweze kupona haraka na  walilaani kitendo cha kinyama, alichofanyiwa na wauaji hao.
 
Waliiomba Serikali ichukue hatua za haraka kukomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini.
 
Akizungumza hospitalini hapo huku akitokwa na machozi katika Wadi Namba 9 alikolazwa Ester, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa ya Viongozi wa Dini, Shehe Hassan Kabeke alisema wanaungana  kwa pamoja kulaani matukio mawili ya kinyama ya kuuawa kwa mtoto Yohana na kujeruhiwa vibaya mama yake mzazi.
 
“Maneno ya kusema yananiishia baada ya kumuona Ester, mimi nadhani hakuna sababu ya kuremba maneno dhidi ya ukatili huu wa kinyama, nasikia maumivu makali sana ndani ya moyo wangu kama kiongozi wa kiroho, tunaitaka serikali katika hili isiondoe adhafu ya kifo kwa kisingizio cha haki za binadamu”, alisema.
 
Aliongeza “Tunapozungumzia haki za binadamu, maana yake ni usawa, ukweli na haki kwa watu wote nchini, haiwezekani watu wengine waue watu halafu tunasingizia haki za binadamu, na wao wahukumiwe adhabu ya kifo, katika hili msimamo wetu kama viongozi wa dini tunaomba adhabu ya kifo isiondolewe”.
 
Pia, aliwataka majaji wanaosikiliza kesi za watu wenye ulemavu wa ngozi, kuzisikiliza kwa wakati ili kuondoa ucheleweshaji wa kesi hizo ili hukumu zitolewe kwa wakati.
 
“Nichukue fursa hii kwa niaba ya wenzangu kuwaomba waheshimiwa majaji waharakishe kusikiliza mashauri yaliyoko mahakamani yanayohusisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino)”, alisema.
 
Kwa upande wake, Katibu Mwenza wa Kamati hiyo ya Amani, Askofu Zenobius Isaya alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),  Ernest Mangu kulichukulia suala la mauaji ya albino kwa uzito wa kipekee kwa vile linagharimu maisha ya watu wasio na hatia katika jamii.
 
“Tunamuomba IGP Mangu alichukulie suala hili kwa uzito mkubwa, afanye uchunguzi wa kina ili aweze kukomesha mauaji haya ambayo yameipaka matope nchi yetu mbele ya Jumuiya ya Kimataifa”, alisema.
 
Akitoa salaam kwa Ester ambaye aliweza kukaa kitandani kwa muda, Isaya alisema shida iliyomkuta ni shida ya Watanzania wote wenye kupenda amani na kuchukia maovu.
 
“Shida iliyokukuta na taabu yako ni taabu yetu sisi sote wapenda amani ; na sisi wapenda amani kwa wingi wetu, kama unavyotuona, tunalaani tukio hili la kinyama, jambo hili ni la kinyama lakini tunakutia moyo uweze kupona haraka na Mungu akupe moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,” alisema.
 
Aliushukuru uongozi wa Hospitali ya Bugando kwa kufanya kazi kwa uvumilivu na kutanguliza upendo katika kumhudumia Ester tangu alipolazwa hospitalini hapo Februari 17 mwaka huu.
 
“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana madaktari na wauguzi wetu kwa kuwa bega kwa bega na Ester kwa kumhudumia bila ya kuchoka, hii inaonyesha kuwa na mshikamano na Mungu awabariki”, alisema.
 
Awali, akiupokea ujumbe huo, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Hospitali ya Bugando, Leah Kagina aliwashukuru viongozi hao wa dini kwa kuamua kutenga sehemu ya muda wao kwa kwenda kumjulia hali.
 
Alisema hiyo ni mara ya kwanza kwa hospitali hiyo kupokea ujumbe huo mkubwa kwenda kumjulia hali Ester.
 
“ Tunawashukuru sana kwa ujio wenu,  ni kwa mara ya kwanza kwa hospitali kupokea ujumbe huu mzito wa viongozi wa kiroho kwa ajili ya kuja kumjulia hali Ester, hii inadhihirisha ni jinsi gani mlivyo na upendo kwa watu wote, rai yangu kwenu niwaombe mtumie ibada zenu katika kutoa elimu kwa jamii dhidi ya mauaji haya”, alisema.
 
Alisema kuwa viongozi wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya imani potofu, ambazo zimekuwa zikienezwa dhidi ya mauaji hayo na kuitaka serikali kuwachukulia hatua stahiki wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi.
 
Akizungumzia hali ya mgonjwa, Muuguzi wa Zamu katika wadi Namba 9, alikolazwa Esta, Adolphina Kishumba alisema hali ya Ester kwa sasa inaendelea vizuri na anajitahidi kula chakula.
 
“Kwa hivi sasa hali ya Ester inaendelea vizuri, ni tofauti na alivyokuwa mwanzo na sasa hivi anakula na anaanza kutembea kwenda chooni”, alisema.
 
Mama mzazi wa Ester ambaye anamuuguza hospitalini hapo, Tabu Mang’enyi aliwashukuru Watanzania kwa misaada yao ya hali na mali wakati wote, ambao amekuwa na mwanawe hospitalini hapo.
 
“Nawashukuru Watanzania wote kwa kumuombea mwanangu na kuendelea kumjulia hali. Kutokana na maombi yenu hali ya mwanangu inaendelea vizuri”, alisema.

Mbatia Aikosoa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ifundi......Asema huo ni mpango wa Serikali Kuwalaghai Wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu


Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Taifa, James Mbatia (kulia), akionesha kitabu cha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitoa tamko la chama hicho juu sera hiyo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosene Nyambabe na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Musa Kombo Musa.
 Hapa mkutano na waandishi wa habari ukiendelea.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
 Wanahabari wakiwa katika mkutano huo.
Wajumbe wa Halmshauri Kuu (NEC) ya chama hicho waliokuwepo kwenye mkutano huo. Kutoka kulia ni Honest Mombory, Katibu wa Wazee, Ernest Mwasada, Dk.Nderakindo Kessy ambaye pia pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Angelina Mutahiwa na Esther Komba.
 
*****
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia amesema kuwa uzinduzi wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ni mpango wa serikali kuwalaghai wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakao fanyika Oktoba mwaka huu.
 
Pia amesema hali ya elimu nchini ni kama mgonjwa aliyekuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, hivyo serikali isiwe inatoa majibu mepesi kwenye masuala magumu ambayo yanagusa maisha ya watanzania.
 
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitoa tamko la chama hicho kuhusu sera hiyo , Mbatia  alisema kuwa mnamo Januari 31 na Februari mosi mwaka 2013, aliwasilisha hoja bungeni kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu.
 
Alisema kuwa aliorodhesha athari mbalimbali za udhaifu wa wa elimu itolewayo nchini lakini suala hilo lilionekana kutawaliwa na siasa ambapo haikuwa lengo lake,lengo lilikuwa kuhakikisha kuwa sera mbalimbazi za elimu zinaboreshwa.
 
Mbatia aliongeza kuwa mnamo Februari 13, 2015 mwaka huu Rais Jakaya Kikwete, alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 lakini ikiwa haijajibu hoja alizokuwa amezitoa.
 
Alifafanua kuwa wakati Rais akihutubia alisema kuwa sera hiyo ilitumia miaka saba kukamilika, lakini Mwenyekiti huyo alisema baada ya kuipitia alibaini sera hiyo kuwa na lugha ngumu huku ikiwa na makosa mengine mengi.
 
Mbatia alisema anachokiona kwa serikali kuzindua sera hiyo mwaka huu ni mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu,kwani yaliyomo ndani ya sera hiyo yamelenga kuwalaghai wapiga kura.
 
Aidha alisema mambo hayo ni pamoja na kutangaza kuwa elimu ya msingi kutolewa bure bila karo na lugha iliyotumika inawachanganya watanzania hivyo ni vigumu kwa wananchi wa vijijini ambao wengi wao hawana elimu kutambua yaliyoandikwa ndani ya sera hiyo.
 
"Mfano sera mpya ina matamko mawili ambayo  inawachanganya watanzania kuhusu lugha ya kufundishia,moja inatamka Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia ngazi zote za elimu,na ya pili inatamka kuwa Kingereza kitatumka kama lugha ya kufundishia katikan ngazi zote za elimu.
 
"Matamko haya mawili, kwanza yanakwepa lawama zinazotokana na malumbano ya muda mrefu kuhusiana na lugha gani inafaa kufundishia, pili imehalalisha mifumo miwili ya elimu ndani ya nchi moja" alisema Mbatia kwa msisitizo 
 
Hivyo alisema serikali ilipaswa kutengeneza sera ambayo inazungumza kwa uhakika kuhusu suala la lugha ya kufundishia, kuliko kutoa tamko la sera lisilo na msimamo.
 
Aliweka wazi kuwa wanapendekeza iundwe tume ya kudumu ya elimu nchini itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine kuhakikisha ubora wa elimu unapatikana nchini.
 
Vilevile alisema wanaiomba serikali kupitia upya sera hiyo kabla haijaanza kutumika ili kuepusha taifa na madhara ambayo yameonesha dalili za kutokea hata kabla haijaanza kutumiaka.

Saturday, February 21, 2015

Mwanamke Amkata Mpwa Wake Sehemu za Siri Huko Ruvuma


Mtu mmoja wa Kijiji cha Majimaji Ruvuma, Patrick Vitus amekatwa sehemu zake za siri  na kuachwa zikining’inia. 
 
Ofisa Mtendaji Wa Kijiji hicho Hussein Mkali amesema Partick alikatwa sehemu zake za siri na mpwa wake Zainabu Saidi baada ya kumkatalia kwenda kumfuata mume wake anayeitwa Musa Said ambaye alikuwa kwa mke mdogo.
 
Baada ya kufanya tukio hilo Ofisi ya Kijiji ilimkamata Zainabu na kumpeleka katika kituo cha Polisi, huku Patrick akipelekwa Hospitali ya Tunduru kwa ajili ya matibabu.

Thursday, February 19, 2015

Uteuzi wa Paul Makonda Kuwa Mkuu wa Wilaya Wapingwa Kila Kona.....Anatuhumiwa Kumpiga Warioba na Kumtusi Lowassa Hadharani


Uteuzi wa Makonda ambao umefanywa na Rais Kikwete, unaonesha kuwashitua wengi; hali ambayo imefanya watu wengi kumbeza hasa kupitia mitandao ya kijamii.
 
Baadhi ya wanaobeza, wanadai kwamba Makonda hana sifa ya kuongoza wilaya kubwa kama Kinondoni, ambayo ina changamoto na migogoro mingi ya ardhi.
 
Makonda ambaye ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM, jina lake limekuwa kubwa hivi karibuni baada ya kutuhumiwa kumpiga  Jaji Warioba wakati wa  mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
 
Pia, kujitokeza kwake hadharani kumpinga Edward Lowassa, kuliongeza jina hilo kuwa maarufu.

Wananchi wakizungumza kwa nyakati  tofauti, baadhi ya wasomaji wa mitandao mbali mbali, wamedai kuwa uteuzi huo wa Rais ni mzuri ila  alikosea kumweka wilaya ya  Kinondoni yenye matatizo chungu mzima ya kiutendaji ikiwemo migogoro ya mipaka, ardhi, wafanyabiashara ndogondogo na mambo mengine ya ndani.

“Tunampongeza Rais kwa kuteua wakuu wapya wa wilaya, ila kwa huyu Paul Makonda kumweka Kinondoni, ameteleza. Hii wilaya inahitaji mtu mwenye uzoefu mkubwa katika uongozi na uadilifu” alisema Sued Musa.

Naye  Albert Chenza  wa  Dar  alikuwa  na  haya ya  kusema: "Ma-DC kama Makonda wapo kwa ajili ya CCM kutetea maslahi ya CCM au wapo kwa ajili ya wananchi kuwasaidia wananchi?
 
"Ikumbukwe DC ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na DSO akiwa katibu wake, sasa mtu kama Makonda ambaye yupo tayari kufanya vurugu yoyote kutetea maslahi ya CCM leo kupewa u-DC wa Kinondoni tutegemee nini uchaguzi mkuu wa Oct 2015?
 
"Ikitegemea kuna mvutano kati ya wapinzani na CCM ambao vyombo vya usalama vinatakiwa kuleta haki na amani, wapinzani wategemee kupata haki au NGUVU zao ndo itakuwa haki yao? Hakika nuru ya amani inafifia Tanzania.
 
"Hii ni kama tupo disco la kukesha ambalo inatolewa CD hii inawekwa ile na zote unahitaji unywe panadol kuzisikiliza." Alisema  Albert  na  kuongeza:

"Ni dhahiri sasa Mzee Warioba na Taasisi ya Mwalimu Nyerere wamemjua adui yao halisi ni nani. Aliyekua mstari wa mbele kumshambulia na kumfanyia fujo Mzee Warioba amepongezwa rasmi  kwa  kupewa  ukuu  wa  wilaya.
 
"Pia imeendelea kujidhihirisha sasa kuwa Ukitaka U-DC wewe mtukane Lowassa kama Nape Nnauye, Mrisho Gambo na Makonda  walivyofanya.
 
"Na pengine atakayekua jasiri vya kutosha na kumchapa angalao vibao viwili usoni anaweza kupata Ukuu wa Mkoa au Ubalozi kabisa"
  
Sailas Kassa Edward  yeye  anamaoni  tofauti  kidogo, na hapa  anaanza  kwa kumpongeza Makonda: "Siku ya jana (juzi) Rais kikwete alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya ambapo moja ya wateule ni paul Makonda. 
 
"Inanishangaza sana kutoka jana(juzi) mpaka leo(jana) watanzania wamekuwa wakilalamika kupitia mitandao ya kijamii wakikosoa uteuzi wa ndgu makonda. 
 
"Mimi binafsi nampongeza kwa nafasi aliyopata nadhani katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania haijampa rais mamlaka ya kuwatenga watu bali kila mtu ana haki ya kuongoza na pia kuongozwa. 
 
"Kwa watanzania itafika hatua kila mtu mwenye intrest za chama cha mapinduzi hamtaki apate nafasi je nani ana haki na nani hana?
 
"Nimejaribu kuchunguza haya yote yanatoka wapi mpaka makonda anakuwa gumzo mtaani nikagundua kuwa wapenzi wa Edward Lowassa wameumia sana kuona makonda anakuwa mkuu wa wilaya hasa ukizingatia anafichua mbinu na hila za Lowassa na makundi yake. "

BASI LA ABIRIA KIDIA ONE LAUA KWA KUGONGANA USO KWA USO NA LORI ENEO LA CHAMWINO DODOMA


Watu wawili wamekufa papo hapo huku wengine 45 wakijeruhiwa baada ya basi la abiria lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza kugongana uso kwa uso na lori katika kijiji cha Vikonje wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 7.05 mchana wakati basi la Kidia lenye namba za usajili T663 AXL kugonga lori lenye namba za usajili T 496 CFG na trela lenye namba za usajili T576 AZX Scania.
 
Alisema basi hilo lilikuwa likitokea  Dar es Salaam kwenda Mwanza wakati lori lilikuwa likitokea Dodoma kwenda  Dar es Salaam.
 
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa lori, Fadhili Said (36) na utingo wa basi, Chogo Chigunda.
 
Kamanda Misime alisema ajali hilo ilitokea wakati dereva wa basi la Kidia, Adam Robert (34) alipokuwa akilifuata gari lililokuwa likilipita gari la mbele yake.
 
Alisema dereva wa basi baada ya kushindwa kulipita gari lililo mbele yake alikutana na lori lililokuwa likija mbele yake na kusababisha ajali hiyo.
 
Alisema Jeshi la Polisi wanamfuatilia dereva wa basi ambaye anatibiwa majeraha katika moja ya hospitali mjini hapa.
 
Pia alisema majeruhi hao bado walikuwa wakitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na wengine wameruhusiwa kurejea nyumbani

Kortini kwa tuhuma za kununua "Malaya wa Buguruni Rozana"


WATU wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Jiji kwa tuhuma za kununua machangudoa katika eneo la Buguruni Rozana jijini Dar es Salaam. Watuhumiwa hao waolifikishwa Jumanne ya wiki hii katika mahakama hiyo ni Antidius Severian (25), Yaham Mihamed (24), Ally Hassan (35) na Mohamed Hamis (27).
  
Wakisomewa mashtaka na wakili wa Serikali, Ramadhan Kalinga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Bernard Mpepo, alidai kuwa Februari 14, mwaka huu katika eneo la Buguruni Rozana watuhumiwa hao walikamatwa na askari mwenye namba E.7882D/CPL wakifanya manunuzi ya madada poa hao huku wakijua ni kosa kisheria.
 
Hata hivyo, washtakiwa hao walikana kosa hilo, ambapo Hakimu Mpepo, alisema dhamana kwa watuhumiwa hao ipo wazi ambapo aliwataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini dhamana ya Sh 200,000.
 
Watuhumiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi Februari 24, mwaka huu kesi itakapotajwa tena.

Majina ya Wakuu wa Wilaya Wapya walioteuliwa na Rais Kikwete yako hapa.......12 Wamesimamishwa na 64 Wamebadilishiwa Vituo

Paul Makonda, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni

RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya Wakuu wa Wilaya kwa kuwateua Wakuu wapya 27, kuwahamisha vituo vya kazi 64 na wengine 42 amewabakisha kwenye vituo vyao vya kazi vya zamani. 
 
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa OWM TAMISEMI jana mchana (Jumatano, Februari 18, 2015) Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema mabadiliko hayo yamesababishwa na kuwepo kwa nafasi wazi 27 ambazo zilitokana na wakuu wa wilaya watatu kufariki dunia; kupandishwa cheo wakuu wa wilaya watano, kupangiwa majukumu mengine wakuu wa wilaya saba na kutenguliwa kwa uteuzi wa wakuu wa wilaya 12. 
 
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema, Rais Kikwete amewabadilisha vituo vya kazi wakuu wa wilaya 64 na kuwabakiza kwenye vituo vyao vya zamani wakuu wa wilaya 42.

Wakuu wa Wilaya ambao uteuzi wao umetenguliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo umri, afya na nyinginezo ni hawa hapa;
  1. James Kisota Ole Millya- Longido
  2. Elias Wawa Lali- Ngorongoro
  3. Alfred Ernest Msovella- Kongwa
  4. Dany Beatus Makanga- Kasulu
  5. Fatma Losindilo Kimario- Kisarawe
  6. Elibariki Emanuel Kingu- Igunga
  7. Dr. Leticia Moses Warioba- Iringa
  8. 8. Evarista Njilokiro Kalalu- Mufindi
  9. Abihudi Msimedi Saideya- Momba
  10. Martha Jachi Umbula- Kiteto
  11.  Khalid Juma Mandia- Babati
  12. Eliasi Goroi Boe Boe Goroi – Rorya
Wakuu wa Wilaya walioteuliwa;
  1. Mariam Ramadhani Mtima- Ruangwa
  2. Dkt. Jasmine B. Tiisike- Mpwapwa
  3. Pololeti Mgema- Nachingwea
  4. Fadhili Nkurlu- Misenyi
  5. Felix Jackson Lyaniva- Rorya
  6. Fredrick Wilfred Mwakalebela- Wanging’ombe
  7. Zainab Rajab Mbussi- Rungwe
  8. Francis K. Mwonga- Bahi
  9. Col. Kimiang’ombe Samwel Nzoka- Kiteto
  10. Husna Rajab Msangi- Handeni
  11. Emmanuel Jumanne Uhaula- Tandahimba
  12. Mboni Mhita- Mufindi
  13. Hashim S. Mngandilwa- Ngorongoro
  14. Mariam M. Juma- Lushoto
  15. Thea Medard Ntara- Kyela
  16. Ahmad H. Nammohe- Mbozi
  17. Shaban Kissu- Kondoa
  18. Zelote Stephen- Musoma
  19. Pili Moshi- Kwimba
  20. Mahmoud A. Kambona- Simanjiro
  21. Glorius Bernard Luoga- Tarime
  22. Zainab R. Telack- Sengerema
  23. Bernard Nduta- Masasi
  24. Zuhura Mustafa Ally- Uyui
  25. Paulo Makonda- Kinondoni
  26. Mwajuma Nyiruka- Misungwi
  27. Maftah Ally Mohamed- Serengeti
 Wakuu wa Wilaya Waliobadilishwa vituo vya kazi
  1. Nyerembe Deusdedit Munasa- Ametoka Arumeru amehamishiwa Mbeya
  2. Jordan Mungire Obadia Rugimbana- Ametoka Kinondoni amehamishiwa Morogoro
  3. Fatma Salum Ally- Ametoka Chamwino amehamishiwa Mtwara
  4. Lephy Benjamini Gembe- Ametoka Dodoma Mjini amehamishiwa Kilombero
  5. Christopher Ryoba Kangoye- Ametoka Mpwapwa amehamishiwa Arusha
  6. Omar Shaban Kwaang’- Ametoka Kondoa amehamishiwa Karatu
  7. Francis Isack Mtinga- Ametoka Chemba amehamishiwa Muleba
  8. Elizabeth Chalamila Mkwasa- Ametoka Bahi amehamishiwa Dodoma
  9. Agnes Elias Hokororo (Mb)- Ametoka Ruangwa amehamishiwa Namtumbo
  10. Regina Reginald Chonjo- Ametoka Nachingwea amehamishiwa Pangani
  11. Husna Mwilima- Ametoka Mbogwe amehamishiwa Arumeru
  12. Gerald John Guninita- Ametoka Kilolo amehamishiwa Kasulu
  13. Zipporah Lyon Pangani- Ametoka Bukoba amehamishiwa Igunga
  14. Issa Suleimani Njiku- Ametoka Missenyi amehamishiwa Mlele
  15. Richard Mbeho- Ametoka Biharamulo amehamishiwa Momba
  16. Lembris Marangushi Kipuyo- Ametoka Muleba amehamishiwa Rombo
  17. Ramadhani Athuman Maneno- Ametoka Kigoma amehamishiwa Chemba
  18. Venance Methusalah Mwamoto- Ametoka Kibondo amehamishiwa Kaliua
  19. Gishuli Mbegesi Charles- Ametoka Buhigwe amehamishiwa Ikungi
  20. Novatus Makunga- Ametoka Hai amehamishiwa Moshi
  21. Anatory Kisazi Choya- Ametoka Mbulu amehamishiwa Ludewa
  22. Christine Solomoni Mndeme- Ametoka Hanang’ amehamishiwa Ulanga
  23. Jackson William Musome- Ametoka Musoma amehamishiwa Bukoba
  24. John Benedict Henjewele- Ametoka Tarime amehamishiwa Kilosa
  25. Norman Adamson Sigalla- Ametoka Mbeya amehamishiwa Songea
  26. Michael Yunia Kadeghe- Ametoka Mbozi amehamishiwa Mbulu
  27. Crispin Theobald Meela- Ametoka Rungwe amehamishiwa Babati
  28. Magreth Ester Malenga- Ametoka Kyela amehamishiwa Nyasa
  29. Said Ali Amanzi- Ametoka Morogoro amehamishiwa Singida
  30. Antony John Mtaka- Ametoka Mvomero amehamishiwa Hai
  31. Elias Choro John Tarimo- Ametoka Kilosa amehamishiwa Biharamulo
  32. Francis Cryspin Miti- Ametoka Ulanga amehamishiwa Hanang’
  33. Hassan Elias Masala- Ametoka Kilombero amehamishiwa Kibondo
  34. Angelina Lubalo Mabula- Ametoka Butiama amehamishiwa Iringa
  35. Farida Salum Mgomi- Ametoka Masasi amehamishiwa Chamwino
  36. Wilman Kapenjama Ndile- Ametoka Mtwara amehamishiwa Kalambo
  37. Ponsian Damiano Nyami- Ametoka Tandahimba amehamishiwa Bariadi
  38. Mariam Sefu Lugaila- Ametoka Misungwi amehamishiwa Mbogwe
  39. Mary Tesha Onesmo- Ametoka Ukerewe amehamishiwa Buhigwe
  40. Karen Kemilembe Yunus- Ametoka Sengerema amehamishiwa Magu
  41. Josephine Rabby Matiro- Ametoka Makete amehamishiwa Shinyanga
  42. Joseph Joseph Mkirikiti- Ametoka Songea amehamishiwa Ukerewe
  43. Abdula Suleiman Lutavi- Ametoka Namtumbo amehamishiwa Tanga
  44. Ernest Ng’wenda Kahindi- Ametoka Nyasa amehamishiwa Longido
  45. Anna Rose Ndayishima Nyamubi- Ametoka Shinyanga amehamishiwa Butiama
  46. Rosemary Kashindi Kirigini (Mb)- Ametoka Meatu amehamishiwa Maswa
  47. Abdallah Ali Kihato- Ametoka Maswa amehamishiwa Mkuranga
  48. Erasto Yohana Sima- Ametoka Bariadi amehamishiwa Meatu
  49. Queen Mwanshinga Mulozi- Ametoka Singida amehamishiwa Urambo
  50. Yahya Esmail Nawanda- Ametoka Iramba amehamishiwa Lindi
  51. Manju Salum Msambya- Ametoka Ikungi amehamishiwa Ilemela
  52. Saveli Mangasane Maketta- Ametoka Kaliua amehamishiwa Kigoma
  53. Bituni Abdulrahman Msangi- Ametoka Nzega amehamishiwa Kongwa
  54. Lucy Thomas Mayenga- Ametoka Uyui amehamishiwa Iramba
  55. Majid Hemed Mwanga- Ametoka Lushoto amehamishiwa Bagamoyo
  56.  Muhingo Rweyemamu- Ametoka Handeni amehamishiwa Makete
  57.  Hafsa Mahinya Mtasiwa- Ametoka Pangani amehamishiwa Korogwe
  58. Dr. Nasoro Ali Hamidi- Ametoka Lindi amehamishiwa Mafia
  59. Festo Shemu Kiswaga- Ametoka Nanyumbu amehamishiwa Mvomero
  60.  Sauda Salum Mtondoo- Ametoka Mafia amehamishiwa Nanyumbu
  61.  Seleman Mzee Seleman- Ametoka Kwimba amehamishiwa Kilolo
  62.  Esterina Julio Kilasi- Ametoka Wanging’o mbe amehamishiwa Muheza
  63.  Subira Hamis Mgalu- Ametoka Muheza amehamishiwa Kisarawe
  64. Jacqueline Jonathan Liana-Ametoka Magu amehamishiwa Nzega