NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Wednesday, February 11, 2015

Serikali Yaiagiza TANESCO Kushusha bei ya Umeme na SUMATRA nao Waagizwa Kushusha bei za Nauli


Baada ya kushuka kwa bei ya mafuta nchini, wakati wowote kuanzia leo Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) linatarajiwa kutangaza bei mpya za umeme ambazo zitakuwa na unafuu kwa wananchi.

Kutangazwa kwa bei hiyo ni agizo la Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene la kuwataka kuangalia uwezekano wa kushusha gharama za umeme ili kushuka kwa mafuta kuwaguse moja kwa moja wananchi wa kawaida.
 
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) nayo imetakiwa kuangalia namna itakavyoweza kushusha bei za nauli ili kushuka kwa gharama za mafuta, kuendane sambamba na kuwagusa wananchi.
 
Simbachawene alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano wa pamoja kati ya wadau na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na wizara hiyo.
 
Alisema, ingawa matumizi ya mafuta katika kuzalisha umeme yamepungua, lakini kwa mitambo na kiasi kinachotumika katika kuzalisha umeme lazima ionekane kushuka kwa bei ya umeme.
 
"Tanesco waangalie ni kwa kiasi gani gharama za uzalishaji, kwa sababu hizo gharama za uzalishaji wa umeme ndiyo zinazotumika kupanga bei ya umeme.
 
”Hivyo lazima tuoneshe Ewura wanapotangaza zile bei, aidha imepanda basi kiasi kile ambacho wananchi huwa wanajisikia vibaya sasa wajisikie raha kwamba tunaona bidhaa hii ya mafuta imeshuka bei, kwa hiyo uzalishaji wa umeme nao unashuka gharama yake," alisema.
 
Alisema ni lazima bei hizo zishuke hata kama ni kwa gharama ndogo kutokana na mitambo mingi inatumia maji na gesi, lakini kiwango hicho ni lazima kionekane kushuka.
 
Aidha, alisema angependa kuona kila shughuli inayogusa nishati ya mafuta ikiwemo mashine za kusaga zinazotumia nishati hiyo zinashusha gharama zake tofauti na hapo wananchi hawataona kushuka huko na lawama zitaelekezwa kwa serikali.
 
Akizungumzia kuhusu suala la usafiri, aliiomba Sumatra iweze kuchukua hatua za haraka za kutangaza bei mpya za nauli ambazo zitakuwa chini tofauti na ilivyo sasa.
 
Awali akijibu maswali na hoja za wadau  hao, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema kusimamishwa kwa ufuatiliaji wa uchakachuaji na wanaokwepa kodi kwa umwagaji wa mafuta ya nje  nchini, itarudisha hali ya miaka ya nyuma, ambapo alisema ni vyema mradi huo ukaendelea kutokana na kuisaidia serikali kukusanya mapato mengi.
 
Mkutano huo ulikuwa unalenga kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu sekta hiyo, ikiwemo changamoto wanazokumbana nazo.
 
Tangu kuanza kwa mwaka huu, bei ya bidhaa za petroli zimekuwa zikishuka bei kutokana na kushuka kwa bei katika soko la dunia. Tayari unafuu umeanza kuonekana kwa watumiaji wa petroli, dizeli na mafuta ya taa, bidhaa ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu ya Sh 2000, lakini sasa zimeshuka na kuwa chini ya Sh 1,800.
 
Kutokana na hali hiyo, wadau wamekuwa wakihimiza kuangaliwa kwa uwezekano wa nafuu hiyo ya bei kugusa pia maisha ya kila siku ya mwananchi, ikiwa ni pamoja na kupunguza nauli katika vyombo vya usafiri.

Monday, February 9, 2015

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE KUTANGAZWA JUMAPILI YA WIKI HII TAREHE 15.01.2015


Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne nchini ya mwaka 2014, yanatarajiwa kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Jumapili wiki hii.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde (pichani), alitoa ahadi hiyo kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa mkoani Dodoma, kufuatia ajali ya moto iliyotokea Januari  20, mwaka huu na kuteketeza mali zote zilizokuwa kwenye bweni la wasichana 64 wa kidato cha tano na cha sita.

Dk. Msonde alikuwa miongoni mwa viongozi walioongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu), Kassim Majaliwa, kwenye ziara ya kutoa pole katika shule hiyo.

“Zawadi niliyowaandalia ni taarifa kwamba Februari 15, mwaka huu, tutatangaza matokeo ya mitihani iliyofanywa na watahiniwa wa kidato cha nne nchini. Nasema ni zawadi kwa sababu sijaitoa mahali kokote, nyie ndiyo wa kwanza kuipata,” alieleza Msonde.

Watahiniwa waliotarajiwa kufanya mtihani huo Novemba, mwaka jana ni 297,488 huku watanihiwa 245,030 wakiwa wa shule na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 52,448. Watahiniwa wa shule walioandikishwa ni wavulana 132,244 (asilimia 53.97) na wasichana 112,786 (asilimia 46.03).

Kupitia ziara hiyo, Serikali imepeleka vitanda 64 ambapo magodoro 64 yalitolewa na Mbunge wa Kibakwe ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.

Pamoja na misaada hiyo, aliahidi kupeleka madaftari, mikebe ya vifaa vya hisabati, kalamu na kumpa kila mwanafunzi aliyekuwa akiishi kwenye bweni lililoteketea fedha taslim ili anunue vifaa binafsi ambavyo havikupatikana kwenye misaada iliyotolewa na wasamaria wema.

Aliongeza kuwa shule hiyo itapelekewa vitabu vya aina zote kwa kiwango cha kila mwanafunzi kuwa na kitabu chake, vitakavyonunuliwa kutokana na Sh. bilioni 27 ambazo zimepatikana kutoka kwenye ‘chenji’ ya ununuzi wa rada.

Pamoja na misaada ya mahitaji binafsi ya wanafunzi inayopelekwa na watu binafsi, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, misaada mingine inayoendelea kupelekwa ni vifaa vitakavyowezesha kujengwa kwa bweni mbadala.

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (LAPF), umepeleka mabati 92 yenye thamani ya Sh. milioni mbili.

SIASA:Mbowe Azindua Mafunzo ya vijana 200 wa Red Brigade na Wacheza Kareti


Chama  Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kimejipanga kuhakikisha katika uchaguzi Mkuu hawaibiwi kura.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freemon Mbowe  wakati akizindua mafunzo ya Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha chama hicho (Red Brigade), kwa vijana 200 wa  Kanda ya Kati pamoja na Kikosi maalum cha Karate.

“Katika  uchaguzi huu hatutaki  kulalamika tena kwamba tumeibiwa kura na tutahakikisha  tutaomba  kura kwa wananchi na tutazilinda,” alisema Mbowe.

Alisema endapo watakubali kuibiwa kura maana yake hawapo tayari kuongoza.

Mbowe aliwataka  vijana hao wa Brigade kutokukilinda chama peke yake bali pia kiwe chachu ya ulinzi kwa jamii inayowazunguka kwenye maeneo yao.

Alibainisha kuwa Chadema  kitaendelea kutoa mafunzo ya ulinzi kwa vijana nchi nzima.

"Vijana  hawa lazima wajenge moyo wa kujitolea, chama kilijengwa na watu wenye moyo huo ambao baadhi walipata madhara mbalimbali ikiwamo kupoteza maisha,” alisema Mbowe.

Alisema wajenge sifa ya kuwa wakombozi wa Taifa na  malipo mengine siyo lazima walipwe hapa duniani bali  watapata  kwa Mungu.

Awali akisoma risala kwa niaba ya kikosi hicho, mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Anatoly Isidory, alisema kikosi hicho kinachojumuisha mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida, kina jumla ya vijana 4,271.

Alisema kati ya hao, 200 wamepewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha kulinda chama na mali zake, viongozi pamoja na kura katika Uchaguzi Mkuu.

“Hadi sasa yapo mafanikio mengi ambayo tumeyapata, ikiwamo kulinda mikutano ya chama pamoja na kuwalinda viongozi wetu katika mikutano hiyo,” alisema Isidory.

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AZINDUA MPANGO WA KITAIFA WA WA KUKUZA STADI ZA KUSOMA, KUANDIKA NA KUHESABU(KKK)


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amezindua Mpango wa Kitaifa wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) unaolenga kukuza viwango vya uelewa kwa watoto wa darasa la kwanza na la pili kwa nchi nzima.

Mpango huo wa miaka mitatu ulioanza kutekelezwa 2014/2015 hadi 2016/2017 umelengwa kuwahusisha watoto wenye umri wa miaka mitano hadi 13 walio kwenye mfumo rasmi wa elimu na usio rasmi (MEMKWA).
 
Akizungumza na wadau wa elimu, walimu na wanafunzi walioshiriki uzinduzi huo juzi jioni (Jumamosi, Februari 7, 2015) Waziri Mkuu Pinda alisema mpango huo ni mkubwa na umeandaliwa mahsusi kujibu changamoto zilizojitokeza miaka ya nyuma.
 
Aliwataka watekelezaji wakuu wa mpango ambao ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuhakikisha kuwa wanazishirikisha asasi zisizo za Kiserikali ambazo zinajihusisha na masuala ya elimu.
 
“Kuna mashirika mengi yasiyo za kiserikali ambayo ni chachu ya kuhimiza elimu nchini... jaribuni kuwashirikisha sababu wao ni wadau wazuri sana wa suala hili. Pangeni utaratibu wa kukaa na hawa wadau na kuwapa mrejesho wa mpango huu mzima,” alisema Waziri Mkuu.
 
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka wahusika wakuu wa mpango waangalie mgawanyo wa mikoa iliyoingizwa kwenye mpango huo kwa kuzingatia kanda ili kuleta matokeo ya mtawanyiko badala ya hali ilivyo sasa. 
 
“Nimeangalia jinsi mlivyogawa mikoa yenu, inanipa taabu kidogo... kuna mikoa inahitaji msukumo wa pekee, mikoa ya wadugaji, mikoa iliyoko pwani ya bahari na maziwa, yote inahitaji msukumo wa tofauti,” alisema.
 
Katika taarifa yao, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilisema mpango huo wa KKK au LANES (Literacy and Numeracy Support Programme) unafadhiliwa na Ushirika wa Kimataifa wa Maendeleo ya Elimu (Global Partnership for Education – GPE) na wahisani wengine.
 
Wahisani hao ni pamoja na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) kupitia mradi wa EQUIP-T unaotekelezwa katika mikoa saba ya Kigoma, Shinyanga, Mara, Simiyu, Lindi, Dodoma na Tabora; Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Elimu kwa Mtoto (UNICEF) wanaofadhili utelekezaji wa Mpango wa LANES katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe; na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia Mradi wa TZ-21 unaotekelezwa katika mkoa wa Mtwara.
 
Mapema, akisoma taarifa ya mpango huo mbele ya Waziri Mkuu, Kamishna wa Elimu nchini, Prof. Eustella Bhalalusesa alisema mpango huo umelenga kuongeza ufanisi katika stadi za KKK, kurahisisha kazi ya walimu wanaofundisha watoto wa darasa la kwanza na la pili pamoja na kuongeza ushiriki wa jamii katika kuboresha elimu na hasa ujifunzaji wa stadi za KKK.
 
Alisema mpango huo utachangiwa sh. bilioni 150 ambazo zitaingizwa moja kwa moja kwenye mfuko wa elimu kupitia Wizara ya Fedha.
 
Alisema maandalizi yote ya utekelezaji wa mpango huu yamekamilika ikiwa ni pamoja na mtaala wa darasa la kwanza na darasa la pili, muhtasari wa KKK kwa darasa la I & II, pamoja na Mwongozo wa Mwalimu wa kufundisha kusoma , kuandika na kuhesabu.

Saturday, February 7, 2015

RIPOTI YA REPOA: Polisi Yaongoza kwa Rushwa.....TRA, Mahakama na TAKUKURU Nao Wamo


Baadhi ya watendaji wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), pamoja na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), ni miongoni mwa watendaji wa taasisi nne ambao wametajwa katika utafiti kuwa wamekithiri kwa kupokea rushwa.

Takukuru na TRA zimetajwa kuwa na kadhia hiyo katika ripoti ya Taasisi ya Afro Barometer iliyofanywa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupunguza Umasikini (Repoa).
 
Kwenye  ripoti  hiyo, Polisi bado wanaongoza kwa kupokea rushwa wakifuatiwa na TRA, Mahakama na Takukuru inashika nafasi ya nne, jambo ambalo limewashitua watu wengi waliohudhuria kwenye mkutano huo.
 
Akiwasilisha ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya wadau mbalimbali, mtafiti wa Repoa, Rose Aiko alisema maofisa wa serikali za mitaa, maofisa serikalini na baadhi ya wabunge na wananchi wamewataja kuwa wanashiriki kwenye vitendo vya rushwa.
 
Ripoti hiyo imeeleza kuwa asilimia 67 ya watu waliohojiwa ambao ni 2,386 walikiri kuwa vitendo vya rushwa vimeongezeka kuanzia mwaka 2013 hadi 2014; licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali za kuajiri maofisa wengi wa kupambana na rushwa katika taasisi ya Takukuru.
 
“Habari kwamba rushwa imeongezeka, imeongelewa na watu wa kawaida mijini, wanaume, wasomi na wakazi wengi wa Zanzibar,” ilieleza ripoti hiyo.
 
Miongoni mwa walihojiwa, asilimia 50 waliitaja polisi kukithiri kwa rushwa, TRA (asilimia 37), Mahakama asilimia 36, Takukuru asilimia 29 wakati maofisa wa Serikali za mitaa ni asilimia 25.
 
Hata hivyo, utafiti huo umebaini kuwa miongoni mwa watu watatu ambao wanaenda kupata huduma Polisi na mahakamani, mmoja kati ya watu hao anadaiwa rushwa.
 
Mtazamo wa wananchi ambao ni asilimia 53, wanaona kwamba wananchi wa kawaida wanaweza kusaidia katika mapambano ya rushwa, huku asilimia 33 wakisema wananchi wa kawaida hawawezi. Pia utafiti huo ulibaini kuwa wananchi wengi hawatoi taarifa kwa mamlaka husika hata pale wanapodaiwa rushwa.
 
Watu wanane kati ya 10 ambao walihojiwa ambao tayari walishatoa rushwa, walikiri kuwa hawakutoa taarifa mahali popote licha ya kutoa rushwa. 
 
Pia utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 34 ya wahojiwa, walitoa rushwa wakati wanatafuta haki mahakamani na wengine asilimia 34 walitoa rushwa kwa kuepuka usumbufu wa Polisi.
 
Pia utafiti huo wa Repoa ulisisitiza kuwa, ili jamii iondokane na tatizo la rushwa, ni lazima watu wakatae kutoa rushwa na wengine wawaripoti kwenye mamlaka zinazohusika wale wote ambao wanawaomba rushwa.
 
Sababu ya watu kutoripoti matukio ya rushwa kwenye mamlaka zinazohusika, utafiti uliainisha kuwa ni mazingira magumu ya upatikanaji wa ushahidi kwa kuwa watuhumiwa wengi wamekuwa rahisi kukataa kuhusika na vitendo vya rushwa.
 
Pia mamlaka zinazohusika na kupambana na rushwa, zimetajwa kuwa ziko mbali, jambo ambalo linawafanya wengi wanaokutwa na janga la kuombwa rushwa, wasiripoti kwa kuepuka gharama za kwenda huko.
 
Pia utafiti huo ulibaini kuwa watu wanaamini bila kutoa rushwa, hawawezi kupata huduma na kwamba mtu ambaye amekusaidia baada ya kupewa rushwa sio vizuri kumripoti Takukuru.
 
“Kubwa hapa ni kwamba jamii haina uelewa wa kutosha kwa maana mtu anaamini kwamba hawezi kupata huduma wakati mwingine atakapokuwa na shida iwapo ataripoti tukio la rushwa Takukuru au Polisi,” alisema Rose.
 
Hata hivyo, wananchi wengi walipongeza vyombo ya habari kwa kuwa mstari wa mbele kutangaza vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya maofisa wa Serikali katika taasisi mbalimbali.
 
Naye Ofisa wa Takukuru, Mary Mosha alipochangia kuhusu ripoti hiyo, alisema Takukuru imekuwa na mpango mkakati   uliowahusisha wadau mbalimbali wa namna ya kuielimisha jamii ielewe juu ya madhara ya rushwa.
 
Alisema pia kuwa juhudi nyingi zimefanywa na Serikali kuziba mianya ya rushwa; “Bahati mbaya ni kwamba juhudi hazionekani na watu wanataka kuona watu wanapelekwa mahakamani."
 
Mosha aliwataka wadau wote kuendelea kushirikiana na Takukuru kupambana na rushwa na akasisitiza kuwa kuna mabadiliko miongoni mwajamii.
 
“Ila tu matukio kama haya ya Escrow wakati mwingine ndio yameifanya jamii ione kuwa tatizo hili bado ni kubwa,” alisema.
 
 Mkurugenzi wa Masuala ya Uchumi wa Repoa, Dk Donald Mmari alisema kuitaja Takukuru ni kuwapa fursa viongozi wa taasisi hiyo kumulika watu wake ili taasisi hiyo isije ikapoteza imani miongoni mwa wananchi.
 
“Sisi ndio maana tumemwita hapa ofisa wa Takukuru na kuitaja kwenye utafiti sio jambo baya, tunataka kumwonesha kinachofanywa na watu wa ofisi yake na wachukue hatua kuanzia sasa,” alisema Mmari.
 
Lakini Dk Benson Bana, alikuwa na mtazamo tofauti kuwa utafiti huo ni mzuri lakini kuitaja Takukuru hadharani, kutakatisha watu tamaa.
 
“Watu wanajenga imani mbaya kwamba mwizi hawezi kumkamta mwizi mwenzake,” alisema Dk Bana.

Lowassa asema hana Haja ya Kutumia Pesa Kumnadi Mtu, Apangua tuhuma za Kuwahonga Milioni 10 Makada wa CCM




WAZIRI Mkuu wa Zamani Edward Lowassa, amekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki iliyosema “Lowassa apanga safu”, akisema hana haja ya kufanya hivyo wala kutumia fedha kumnadi mgombea yeyote.
 
Taarifa iliyotolewa na ofisi yake  ilisema habari hiyo ilijengwa na taswira ya uongo kwamba kuna mpango wa kupanga nani atagombea ubunge katika Jimbo la Monduli baada ya Lowassa kumaliza muda wake.
 
“Taarifa hiyo potofu ilikuwa na lengo la kumshushia Lowassa hadhi kwa wananchi wake,” ilisema taarifa hiyo.
 
Kwa mujibu wa taaifa hiyo, Lowassa anatarajia kupeleka malalamiko rasmi kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Idara ya Habari (Maelezo) ili ukweli ujulikane.
 
Ilisema habari hiyo ilidai kuwa Lowassa amewahonga makada kadhaa wa CCM wilayani humo ambao wameonyesha au wana nia ya kuwania kiti hicho, Sh millioni 10 kila mmoja ili wamuunge mkono Mbunge wa Viti Maalum, Namelok Sokoine.
 
Taraifa hiyo ilimnukuu Lowassa akisema, “Huu ni muendelezo wa habari za uongo na uzushi dhidi yangu ambao gazeti hili limekuwa likiufanya kwa muda mrefu sasa. Gazeti hili limekuwa likitumika kama chombo cha propaganda dhidi yangu,” alisema Lowassa na kuongeza:
 
“Kwa muda mrefu sasa gazeti hili limekuwa likizusha habari za uongo dhidi yangu. Mfano ni taarifa potofu na ovu ya mimi kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kongosho nchini Ujerumani jambo ambalo ni uongo”.
 
Alisema inasikitisha kuona gazeti lenye waandishi na wahariri makini kama hilo linaweza kuacha kufuata maadili ya uandishi wa habari na kuamua kuandika habari ambazo hazina hata chembe ya ukweli.
 
“Lazima watambue kwamba wananchi wamekwisha kuelewa uovu na uonevu wa gazeti hili dhidi yangu,” alisema.

Wednesday, February 4, 2015

Rais Kikwete Afichua SIRI Kipigo cha Lipumba


SIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake kupigwa na polisi, Rais Jakaya Kikwete amesema tukio hilo limetokea kwa sababu nchi inaongozwa kwa sheria na atakayekiuka atakumbana na mkono wa sheria.
 
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo ya faragha na mgeni wake, Rais wa Ujerumani, Joachim Gauck, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tano.
 
Kabla ya Rais Kikwete kutoa kauli hiyo, Rais Gauck aliimwagia sifa Tanzania kutokana na namna inavyofuata utawala wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na kulinda haki za binadamu.
 
Baada ya viongozi hao kuzungumza mbele ya waandishi wa habari juu ya ziara hiyo, waandishi walipewa fursa ya kuuliza maswali na ndipo mmoja wa wanahabari kutoka Ujerumani, alipotaka kauli ya Rais Kikwete na Rais Gauck, juu ya msingi wa uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu nchini, wakati hivi karibuni gazeti la The East African lilifungiwa na wanachama wa CUF kupigwa na polisi walipotaka kuandamana.
 
Akijibu swali hilo, Rais Kikwete alisema: “Tuna sheria zinazoongoza mambo hayo, huwezi kuamka tu ukaamua kuandamana, tuna taratibu zetu za vyama vya siasa kukusanyika, wala hatubani haki na uhuru wa wapinzani, ukivunja sheria hiyo utawajibishwa.
 
“Na hapa wapinzani ndio wanafanya mikutano mingi kuliko chama tawala, ikitokea hawajafuata taratibu, hatuwezi kuwaacha waendelee kuvunja sheria,” alisema Rais Kikwete.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Profesa Lipumba alisema walifuata sheria zote na pia kutii amri ya polisi ya kuwataka kuacha kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara.
 
CUF walipanga kuandamana na kufanya mkutano wa hadhara kukumbuka wenzao waliouawa mwaka 2001.
 
Kuhusu kufungiwa kwa gazeti la kila wiki la The East African linalochapishwa nchini Kenya na Kampuni ya Nation Media Group (NMG) na kusambazwa Tanzania, Rais Kikwete alisema halijafungiwa bali lilibainika kusambazwa nchini bila kuwa na kibali.
 
Alisema baada ya kubainika hilo, kampuni inayochapisha gazeti hilo ilitakiwa kutoendelea kulisambaza nchini hadi kibali cha kufanya hivyo kitakapopatikana.
 
Rais Kikwete alisema kwa sasa utaratibu wa kutoa kibali hicho unaendelea.
 
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani ambazo zinajali uhuru wa vyombo vya habari, na hata sasa kuna magazeti mengi yaliyosajiliwa na yanachapishwa kila siku.
 
Akizungumzia kuhusu hali ya usalama na tishio la ugaidi, Rais Kikwete alisema hawezi kusema kuwa Tanzania iko salama asilimia 100, lakini kutokana na hatua zinazochukuliwa za kulinda amani na usalama, hali iko shwari.
 
“Tunashirikiana vizuri na vyombo vya usalama vya kimataifa, tunadabilishana taarifa kila inapobidi, siwezi kusema kuwa sisi tuko salama kwa asilimia 100, kwamba hatuwezi kuguswa kutokana na mikakati ya kulinda amani, hali kwetu ipo shwari,” alisema.
 
Katika hatua nyingine, aliiomba Ujerumani kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini, ikiwamo gesi, viwanda na biashara.
 
Alisema Tanzania baada ya kugundua gesi asilia, pamoja na mambo mengine itatumika kwa matumizi ya nyumbani kwani kwa sasa zaidi ya tani 40 za mkaa hutumika Dar es Salaam pekee kila mwaka, hivyo kiasi kikubwa cha miti huteketea.
 
Kwa upande wake, Rais Gauck, alisema Ujerumani iko tayari kuendeleza ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi na Tanzania na ndiyo maana katika msafara wake ameongozana na wadau mbalimbali wa sekta za kiuchumi, wakiwamo wafanyabiashara wakubwa na waziri husika kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa za uwekezaji.
 
Alisema anaridhishwa na jinsi Tanzania inavyosimamia haki za binadamu na kasi ya kushughulikia tatizo la rushwa, umoja wa kitaifa na maendeleo, na kwamba Ujerumani itaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo na Tanzania.
 
Rais Gauck alisema nchi hizi mbili zimekuwa na ushirikiano wa kihistoria tangu mwaka 1961, na ndiyo maana kuna miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii iliyotekelezwa, na kwamba Ujerumani inaisaidia kiuchumi Tanzania.
 
Aliipongeza pia Tanzania kutokana na kushiriki katika kutuliza migogoro ya kikanda, ikiwa ni pamoja na kutafuta amani Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
 
Alisema Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa jinsi inavyojituma kupeleka majeshi yake katika mataifa yenye machafuko, kwani kwa kufanya hivyo inajilinda yenyewe.
 
Rais Gauck anatarajiwa pia kutembelea Zanzibar, Bagamoyo, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na ameomba akae Arusha kwa muda kabla ya kurejea Ujerumani, kwani mji huo una sifa ya kipekee duniani.