NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Wednesday, March 11, 2015

AJALI YA BASI LILILOANGUKIWA NA KONTENA IRINGA

Taarifa za awali kutoka jeshi la polisi mkoani Iringa zinaeleza kuwa basi la kampuni Majinja lenye usajili wa namba T438 CDE limelaliwa/kuangukiwa na Lori lilikuwa limebeba jumla ya watu 49, idadi hiyo ni pamoja na dereva na kondakta wa basi hilo.wengi wa watu hao wamefariki dunia idadi ya majeruhi haijajulikana bado. Taarifa hizo zinaeleza kuwa kwenye mizigo mingi ya abiria waliokuwa kwenye basi hilo kumepatikana madaftari mengi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam hivyo jeshi hilo linaendelea kufanya mawasoliano ma wamiliki wa gari hilo ili kujua kama lilikuwa limekodishwa kubeba wanafunzi wa chuo hicho ama ni mchanganyiko wa kawaida wa abiria.



Hivi ndivyo Basi la Majanja linavyo onekana mara baada ya kuondoa Lori lilikuwa limekandamiza basi hilo.
 
 Umati wa watu mbalimbali wakiwemo wasafiri wasafiri waliokuwa katika mabasi mengine wakiwa wamejaa kushuhudia Ajali hiyo.
Shughuli za uokoaji zikiwa zinaendelea

Muonekano wa Basi la Abiria na Lori yaliyo athirika kwa ajali hiyo

Mashuhuda
Basi la Abiria likiwa katika Hali mbaya baada ya ajali
Waokoaji wakiwa wanaendelea kufanya ushirikiano namna ya kuwasaidia watu waliopata ajali hiyo.
 
Miongoni mwa watu wakiwa wanatazama namna Magari hayo yalivyopata ajali



 
Askari wa usalama Barabarani wakiwa wanahakikisha watu mbalimbali waliodhurika katika ajali hiyo wanaweza  kupata msaada/huduma kwa haraka.

 Basi lililokuwa limebeba abiria waliokuwa wakitokea Mbeya kuelekea Dar es salaam  Lenye namba za usajili T438 CDE likiwa katika hali mbaya.

Albino Kukatwa Mkono: Waganga 10 Pamoja na Baba Mzazi Watiwa Mbaroni- NAFDA INAPINGA VIKALI UKATILI HUU


Polisi mkoani Rukwa inawashikilia watu 17 wakiwemo waganga wa jadi 10 wakihusishwa na tukio la kikatili katika kijijini cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga ambako mtoto mlemavu wa ngozi (albino), Baraka Cosmas (6) mwishoni mwa wiki alishambuliwa na kukatwa kiganja cha mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana.
 
Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni watu saba ambao wanatuhumiwa kushiriki katika kumkata kiganja mtoto huyo mlemavu wa ngozi akiwemo baba yake mzazi, Cosmas Yoram (32).
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Ferdinand Rwegasira amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao kufuatia msako mkali uliofanyika katika vijiji vinne vya wilaya za Sumbawanga na Nkasi.
 
Aliwataja waliokamatwa pamoja na baba mzazi wa mtoto huyo kuwa ni pamoja na Mwendesha William (30), Masunga Bakari (50), na Ngolo Masingija (47) wote kutoka kijiji cha Kaoze .
 
Wengine ni Paschal Jason (40), David Kiyenze (45) na Mageta Shimba (46), wote wakazi wa kikiji cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.
 
Kwa mujibu wa Rwegasira, katika msako huo pia walikamatwa waganga wapiga ramli chonganishi 10 akiwemo Sererino Kachingwe “Nakalango”(70), mkazi wa kijiji cha Miangalua wilayani humo ambaye pia alipatikana na bunduki aina ya Shot gun greener yenye namba G 73354 TZD,CAR 47478 ambayo anaimiliki isivyo halali .
 
“Mtuhumiwa huyu pia ni mganga wa kienyeji ambapo alikutwa na wanyama wawili aina ya Kalunguyeye wakiwa hai pamoja na dawa mbalimbali za miti shamba.
 
"Pia katika msako huo amekamatwa mganga mwingine wa kienyeji , Eliza Malongo mwenye umri wa miaka 36 mkazi wa kijiji cha Kamnyalila akiwa na nyara za Serikali, “ alieleza.
 
Aliongeza Eliza alikutwa na ngozi ya chui, wanyama wanne waliokaushwa aina ya Kalunguyeye na nywele zinazodhaniwa kuwa za binadamu pamoja na mfupa wa swala.
 
Waganga wengine waliokamatwa katika msako huo ni pamoja na Sodeli Malimbo ‘Chuchi” (69) mkazi wa kijiji cha Miangalua, Akobo Chinzwe (50), Leonard Samson (59) na Engelbert Kasinde (45) , wote wakazi wa kijiji cha Kamyalila.
 
Katika orodha hiyo wapo Boniface halya (49) na Julius Simbamwene (40) wote wakiwa wakazi wa kijiji cha Mpui .
 
“Watuhumiwa hawa walikutwa na vifaa mbalimbali vya kupigia ramli vikiwemo vioo viwili, pembe moja, ndege na wanyama ambao hawakuweza kutambulika mara moja, mizizi ya aina mbalimbali na dawa mbalimbali za kienyeji,“ alieleza Rwegasira.
 
Akifafanua zaidi, Rwegasira alidai kuwa msako huo pia ulifanyika wilayani Nkasi ambako alitiwa nguvuni mganga wa kienyeji aitwae Charles Misalaba (47) , mkazi wa kijiji cha Kacheche ambapo alikutwa na yai la mbuni , kucha za chui , pembe ya korongo , ngozi ya paka pori na kobe aliyekaushwa.
 
Amesisitiza kuwa msako huo bado unaendelea na kwamba watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara tu baada ya upelelezi wa awali wa shauri lao kukamilika.
 
Kwa mujibu wake msako huo unafuatia watu wasiojulikana kumshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita, Baraka Cosmas na kisha kutokomea nacho kusikojulikana usiku wa kuamkia Machi 08, mwaka huu.
 
Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas Yoram (32) na Prisca Shaaban pamoja na watoto wengine wawili ambao nao ni albino wakiwa na umri wa miaka nane na minne.
 
Alisema tukio hilo ni la saa nane usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo.
 
Akielezea zaidi, Kaimu Kamanda Rwegasira alisema usiku huo kikundi cha watu wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi, Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
 
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumjeruhi vibaya …
 
“Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojulikana,” alibainisha.

Tundu Lissu Atangaza Rasmi Kuwa Zitto Kabwe Si Mwanachama wa CHADEMA


Mwanasheria mkuu wa chama cha upinzani nchini CHADEMA, Tundu Lissu leo ametangaza kuvuliwa uanachama kwa mbunge wa Kigoma Kasikani Zitto Kabwe baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi la mbunge huyo la kuzuia asijadiliwe.

"Kwa mujibu wa katiba ya chama cha CHADEMA, mwanachama yoyote anapofungua kesi mahakamani dhidi ya chama chake, endapo atashindwa katika kesi hiyo atakuwa amejiondoa uanachama wake, kwahiyo natangaza rasmi rasmi Zitto Kabwe sio mwanachama tena wa Chadema." Amesema  Tundu  Lissu

Kwa upande wake Zitto Kabwe amesema hawakuwa na wito wa mahakamani leo na Jaji wa kesi kahamishiwa Tabora na hawana taarifa ya Jaji Mpya, pia kaongeza kuwa Mwanasheria anafuatilia na atatoa taarifa rasmi

Wednesday, March 4, 2015

MAKAHABA, MATEJA WAMPONZA GWAJIMA!

NI msala! Kupigwa notisi ya kutakiwa kuhamisha kanisa kwa  Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kumeelezwa kusababishwa na baadhi ya makahaba, wavuta bangi na wengineo, Amani limeambiwa.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Mapema wiki iliyopita, Gwajima amepewa  notisi na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ikimtaka kuhamisha kanisa lake kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar ifikapo Machi 9, mwaka huu.
Taarifa zilizodakwa na gazeti hili zinasema kuwa, barua mbili za NHC zilipelekwa kwa makanisa  mawili likiwemo la Ngurumo ya Upako la Nabii George David ‘Geor Dave’ (Amani lina nakala).
Amani lilifika kwenye viwanja  hivyo mwanzoni mwa wiki hii na kuzungumza na wenyeji wa eneo hilo ambao walisema hata wao wanasikia mchungaji huyo anatakiwa kuondoka eneo  hilo lakini kwa ajili ya kupisha ujenzi wa nyumba za NHC.
Katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mzimuni, Amani lilizungumza na mwenyekiti wake,  Hassan Faraji Nganyani ambapo alikiri kupata kopi ya barua hiyo.
“Ni kweli ndugu waandishi kopi ya barua kutoka Shirika la Nyumba la Taifa tumepata, inawataka viongozi wa  makanisa  hayo mawili kuhama ifikikapo Machi 9, mwaka huu,” alisema kiongozi  huyo.
Kiongozi huyo alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, kuhamisha makanisa hayo ili kujenga nyumba za shirika ni sahihi lakini tatizo jingine ni kwamba, siku ambazo waumini hao hawakeshi  kanisani hapo, kuna  makundi  ya watu hufika eneo hilo na kufanya ukahaba, wengine  kutupa vichanga baada ya kutoa mimba achilia mbali wahuni wanaovuta bangi na mateja mbalimbali ‘wabwia unga’.
Mzee mmoja ambaye alisema ni mstaafu wa serikali alisema kuwa, alishapeleka maombi kwenye shirika la nyumba akitaka eneo hilo lidhibitiwe baada ya baadhi ya watu, ukiacha makanisa kulitumia vibaya.
“Ni kweli siku kukiwa hakuna ibada, wahuni, m****** wavuta bangi na watumia madawa ya kulevya wanageuza maskani yao. Nadhani NHC walizingatia pia maombi yangu na ya wengine,” alisema mstaafu huyo.
Waandishi walifakiwa kuongea na baadhi ya watu wanaoabudu  katika Kanisa la Gwajima ambapo walisema eneo hilo lilikuwa  limezoeleka kwa kila mtu aliyekuwa  akiabudu hapo.Baadhi yao walisema uwanja huo ulikuwa  unatosheleza  umati  uliokuwa ukifika kusikia Neno la Mungu lakini baada  ya kupata  notisi hawajui  watapata wapi  kiwanja  kikubwa kama hicho.
Juhudi za kumpata Mchungaji Gwajima hazikufua dafu baada ya simu yake kuita muda mrefu bila kupokelewa. Amani lilipofika kanisani kwake ilidaiwa yuko safarini.
Mchungaji Gwajima alihamia katika viwanja hivyo mwaka 2008 akitokea Ubungo Chai Bora, Dar ambako kulionekana kutokidhi idadi ya watu.Nabii Geor Dave naye alipotafutwa na Amani kwa njia ya simu hakupatikana hewani hadi gazeti linakwenda mitamboni.
chanzo cha habari:
Global publishers.

Friday, February 27, 2015

Mwanamke Auawa na Mumewe Kwa Kipigo na kisha Mwili wake Kufukiwa katika Zizi la Ng'ombe


Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Ubetu Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, amefariki dunia baada ya kupigwa na mume wake sehemu mbalimbali za mwili na kisha kuzika mwili wake kwenye boma la ng'ombe.
 
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo lilitokea Februari 25 mwaka huu saa 11:45 jioni.
 
Akieleza mazingira ya tukio hilo, Kamanda Kamwela, alisema siku ya tukio jirani na familia hiyo alipigiwa simu na mume wa marehemu na kumwambia ameuwa mkewe na kumtelekeza ndani ya bomala ng’ombe.
 
Kwa mujibu wa kamanda, mwanamke huyo aliyeuawa ametajwa kuwa ni Jenipher Peter (45). Alisema alikuwa akiishi na mume wake, Peter Mrosso (43) pamoja na watoto wao watatu. Alisema mwili wake ulifukiwa ndani ya boma la ng'ombe.
 
Kamanda alisema taarifa za mauaji ya mwanamke huyo ilitolewa baada ya jirani yake kupigiwa simu na mume wa marehemu, akimtaarifu kuwa amemuua mkewe na maiti ameifukia ndani ya boma la mifugo

Thursday, February 26, 2015

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Aua Mwanafunzi Mwenzake Darasani Wakati Wakigombania Daftari la Notes



Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Ilola iliyopo katika wilaya ya Shinyanga vijijini aitwaye Veronica Venance mwenye umri wa miaka 12 amefariki dunia kwa kupigwa na mwanafunzi mwenzake wakati wakigombania daftari darasani kwa ajili ya kuandika notes.

Walioshuhudia tukio hilo wamesema limetokea Februari 24 mwaka huu, saa 7 na nusu mchana katika darasa la tano katika Shule ya Msingi Ilola iliyopo katika Kata ya Ilola, Tarafa ya Itwangi, Wilaya ya Shinyanga.

Wamesema mwanafunzi huyo amefariki dunia baada ya kupigwa makofi na ngumi sehemu za kichwani na mwanafunzi mwenzake aitwaye Sophia Mathew (12).

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Andrew Chenge Agoma Kuhojiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Umma.....Adai kuna zuio la mahakama kuu, hatima yake kujulikana leo


MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Mtemi Andrew Chenge, jana ameonyesha utemi wake mbele ya Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma, baada ya kusema haiwezi kumjadili kwa sababu kuna kesi mahakamani.
 
Alisema kuna zuio la Mahakama Kuu ambalo limevitaka vyombo vyote vya Serikali kutojadili suala la miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.
 
Tume hiyo inamtuhumu mbunge huyo kuwa alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitumia madaraka yake vibaya katika uuzaji wa hisa za Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwenda Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited.
 
Itakumbukwa wakati suala la Tegeta Escrow likijadiliwa bungeni, Chenge alidaiwa kupewa sh bilioni 16 na mmiliki wa VIP Engineering Tanzania Limited, James Rugemalira.
 
Jana, kabla ya Chenge kuieleza Tume ya Maadili kuwa haiwezi kumuhoji, Mwanasheria wa tume hiyo, Hassan Mayunga, alisoma mashtaka yanayomkabili.
 
“Mlalamikiwa akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mwaka 1995 aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 wa kuongeza uzalishaji wa umeme na Kampuni ya IPTL.
 
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya VIP Engineering Tanzania Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye Kampuni ya IPTL.
 
“Kitendo cha kuingia mkataba na Kampuni ya VIP ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(i) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha katika utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake kwa masilahi binafsi,” alisema Mayunga.
 
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri wa Kampuni ya VIP huku akiwa na wadhifa wa ubunge, ni ukiukwaji wa kifungu cha 6(e) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgogoro wa kimasilahi.
 
Mayunga alisema mkataba ambao mlalamikiwa aliingia na VIP, ulimpatia masilahi ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume na kifungu cha 12(1)(e) cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
 
“Mwaka 2014 mlalamikiwa aliingiziwa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 na kampuni hiyo katika Benki ya Mkombozi wakati hakutamka mapema kama aliwahi kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali na kwamba ana masilahi binafsi na kampuni hiyo wakati alikuwa akijua kuwa Shirika la Umeme (Tanesco) lina mgogoro na IPTL,” alisema. Chenge
 
Baada ya kusomewa mashtaka, Chenge aliyakana na kuomba mwongozo kwa madai kuwa suala hilo lina zuio la Mahakama Kuu, hivyo basi tume hiyo haiwezi kujadili suala hilo hadi kesi ya msingi itakapokwisha.
 
“Napata shida kujadili suala hili, mimi nikiwa kama mwanasheria linanisumbua kidogo, kutokana na umahiri wako jaji, ninaomba upitie zuio lililotolewa na Mahakama Kuu kwa kina ili uweze kuangalia kisheria, je inaruhusiwa kujadili au la,” alisema Chenge.
 
Baada ya majadiliano hayo, Mwanasheria Mayunga alisema amri ya mahakama haihusiani na kazi za baraza kwani katika oda ya mahakama, hakuna kipengele cha kuzuia kujadili suala hilo.
 
“Ibara ya 132 ya sheria ya mwaka 1987, ibara ndogo ya kwanza ambayo inaeleza kuwa kutakuwa na sekretarieti ya maadili ya utumishi wa umma ya kuchunguza mienendo ya viongozi na watumishi wa umma.
 
“Taasisi hii ni huru na kwamba inafanya kazi endapo kuna taarifa ya ukiukwaji wa maadili kwa viongozi katika suala la rushwa au kutumia madaraka yao vibaya,” alisema Mayunga.
 
Baada ya kusema hayo, Mwenyekiti wa barza hilo, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alihairisha shauri hilo na kusema watapitia zuio la mahakama hiyo ili waweze kuangalia kama ni kweli linaweza kuwazuia kufanya kazi zao au la na leo waweze kutoa uamuzi.
 
“Tumeomba muda kidogo ili tuweze kuipitia hii oda ya mahakama na kuiangalia kwa umakini kama ni kweli inatuzuia tusijadili suala hili au la, leo tutatoa uamuzi kamili,” alisema Jaji Msumi.
 
Aliongeza kutokana na hali hiyo, baraza hilo linapitia hoja ya mlalamikiwa na mlalamikaji ili kuangalia mambo ya kisheria yanayohusu kujadili au kutokujadili suala hilo.
 
Chenge akiwa nje ya Ukumbi wa Karimjee ambako mashauri hayo yanasikilizwa, waandishi walitaka kusikia maoni yake juu ya suala hilo na yeye akawajibu: “Andikeni kama mlivyoona na kusikia.”
 
Mbunge huyo alifika katika viwanja vya Karimjee saa 3:00 asubuhi kabla ya kuanza kusikilizwa kwa shauri lake saa 3:15 baada ya jopo la majaji na mwenyekiti wa baraza hilo kuwasili.
 
Baraza hilo pamoja na kutolea uamuzi wa shauri la Chenge wa kusikilizwa au kutosikilizwa leo, pia linatarajia kumuhoji Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kwa siku mbili – leo na kesho.
 
KASHFA ZA CHENGE
Chenge ametajwa kuhusika katika kashfa mbalimbali, zikiwamo za rada, ajali iliyoua watu wawili na uchotwaji fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Rada
Chenge alitajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada, ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri.
 
Rada hiyo ilinunuliwa kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa dola milioni 40 mwaka 2001, kiwango kilicholistua Bunge la Uingereza.
 
Katika uchunguzi wa suala hilo, ilibainika kuwa Chenge alikuwa na akaunti kwenye Kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya dola milioni 1 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.8) hali iliyofanya ashinikizwe kujiuzulu wadhifa wake wa uwaziri wa miundombinu.
 
Ajali iliyoua wawili
Wakati kashfa ya rada ikiendelea, Chenge alihusika katika ajali iliyoua wanawake wawili mmoja akitajwa kuwa mtu wake wa karibu.
 
Baada ya ajali hiyo, alishtakiwa kwa makosa ya kuendesha gari kizembe na bila kuwa na bima.
 
Alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 700,000 ambazo alilipa.
 
Tegeta Escrow
Mwaka jana alijikuta kwenye kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ambapo alidaiwa kuchotewa Sh bilioni 1.6.
 
KAULI TATA
1. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.8 za rada, alisema ‘Ni vijisenti’.
 
2. Alipopata kashfa ya kuchota Sh bilioni 1.6 za Escrow, alikuja na kauli mbili: “Mimi ni tumbili, hata kwenye hii (kashfa ya Escrow)” na “Mimi ni nyoka wa makengeza, nawatafutia wananchi fedha.”
 
3. Wakati wa kelele za kumtaka Chenge na wenzake kujivua gamba, mbunge huyo alisema: “Gamba limevuka limeishia kiunoni”.
 
4.Ashauri waliohusika na kashfa ya Escrow, mamlaka ya uteuzi (Rais) iwashughulikie na wapinzani wakaungana naye, lakini CCM wakagoma.
 
NYADHIFA ALIZOWAHI KUSHIKA
2014: Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya.
2006/15: Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti.
2006/08: Waziri wa Miundombinu.
2006: Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
1993-05: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1991-93: Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
1972-73: Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM