Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema katika majaribio ya uandikishaji
wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, mfumo mpya wa
uandikishaji wa 'Biometric Voter Registration Kit' (BVR), umefanikiwa
kwa asilimia kubwa licha ya changamoto kadhaa, na ina uhakika mfumo huo
utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika daftari hilo bila
matatizo.
Aidha,
Tume hiyo imebadilisha tarehe ya kuanza rasmi uandikishaji wa wananchi
katika daftari la kudumu uliokuwa uanze Februari 16, katika mkoa wa
Njombe, hadi Februari 23, mwaka huu, ili kutoa nafasi kwa wadau kuweza
kujiandaa vyema.
Pamoja
na hayo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wameonesha wasiwasi juu
ya utaratibu mzima wa uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu
kupitia BVR, kuwa kama utafanyika na kumalizika kwa wakati, kutokana na
tume hiyo kuchelewa kufanya mambo mengi, ikiwemo elimu ya uraia na kutoa
ratiba ya uandikishaji.
Akifungua
mkutano ulioandaliwa na tume hiyo kwa ajili ya kukutana na vyama vya
siasa kujadili uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura,
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, alisema tume hiyo ilianza
utaratibu wa majaribio ya uandikishaji kwa kutumia mfumo huo katika
mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro na Katavi.
“Kwa
ujumla uandikishaji ulifanyika vizuri na kwa mafanikio katika maeneo
yote, idadi ya watu walioandikishwa pia katika maeneo hayo iliongezeka
na kuvuka lengo ambalo tume iliweka kwa zaidi ya asilimia 100 licha ya
kuwepo kwa changamoto kadhaa, hii ni dalili nzuri kwamba mfumo huu
utafanikiwa,” alisema Jaji Lubuva.
Alisema
tume hiyo katika eneo la Kawe mkoani Dar es Salaam ililenga kuandikisha
wananchi 14,312, lakini waliandikishwa wananchi 15,123 sawa na asilimia
105.67, Kilombero mkoani Morogoro waliandikishwa wananchi 19,188 wakati
lengo la Tume lilikuwa wananchi 17,290 sawa na asilimia 110.9.
“Pia
katika mkoa wa Katavi, wilayani Mlele, tuliweka lengo la kuandikisha
wananchi 11,104 lakini kupitia mfumo huu wa BVR ambao katika kila kituo
tulitumia BVR kit 80, tuliandikisha wananchi 11,210,” alisisitiza.
Aliwahakikishia
wanasiasa hao kuwa, kutokana na majaribio ya mfumo huo katika mikoa
hiyo, pamoja na kubaini changamoto kadhaa, tume hiyo ina uhakika mfumo
huo ni imara na unaweza kutumika kuandikishia Watanzania wote katika
muda uliopangwa bila matatizo.
Hata
hivyo, alisema tume hiyo imebadilisha muda wa kuanza uandikishaji
kutoka Februari 16 hadi 23, mwaka huu, ambapo katika mkoa wa Njombe
pekee wanatarajia kutumia vifaa vya BVR takribani 250 huku vifaa vingine
7,050 vikisubiriwa kuwasili nchini kwa ajili ya uandikishaji kuendelea
maeneo mengine.
“Suala
la ratiba tunalifahamu na tutaitoa muda wowote, tayari Serikali
imeshatoa fedha kwa ajili ya vifaa hivi ambavyo vinatokea China, awamu
ya kwanza vifaa takribani 2,000 vitawasili wiki ya kwanza ya mwezi
Machi, napenda nitoe wasiwasi, Tume iko huru, wazi na haina chochote
inachokificha wala kutumika na mtu,” alisema.
Aidha,
Jaji Lubuva, alisema kutokana na taarifa za sensa, tume hiyo imeongeza
vituo vya uandikishaji wapiga kura kutoka vituo 24,919 vya zamani hadi
vituo 36,109.
Naye
Mkurugenzi wa tume hiyo, Julius Malaba, alisema katika majaribio ya
mfumo huo wa BVR, changamoto kadhaa zilijitokeza ikiwemo mfumo mzima wa
BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na programu zinazotumiwa na mfumo
huo pamoja na maeneo ya uendeshaji uandikishaji huo.
“Changamoto
zote hizi tumezifanyia kazi kwa kuzirekebisha. Katika BVR
zitakazotumika mkoani Njombe nazo zimefanyiwa marekebisho kutokana na
changamoto zilizojitokeza, ila tumechukua tahadhari za uhakika ili
kuhakikisha utaratibu mzima unafanyika bila tatizo,” alisema Malaba.
Wakitoa
maoni yao kuhusu mada hiyo, wengi wa viongozi wa vyama vya siasa
walionesha wasiwasi na kutokuwa na imani na tume hiyo kwa kushindwa
kuwasilisha ratiba nzima ya uandikishwaji nchi nzima ikiwa ni pamoja na
utaratibu huo kuanza huku vifaa vingi vikiwa bado havijawasili.
Mwenyekiti
wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, alisema
bado kuna masuala mengi yenye utata ambayo tume hiyo haijayafafanua
likiwemo suala la programu zipi zinazotumiwa na mfumo huo, lini vifaa
vyote vitawasili na kwanini mpaka sasa hakuna ratiba ya uandikishwaji
wapiga kura.
“Tunaomba
ratiba kamili ya uandikishwaji, mnasema mmeongeza muda ili tujipange na
kutoa mawakala, sasa tutajipangaje wakati hata hatujui ratiba yenyewe,
lakini pia bado elimu ya uraia iliyotolewa hasa juu ya BVR kwa wananchi
na watendaji watakaoendesha uandikishaji haitoshi, tuna wasiwasi, naomba
jambo hili baadaye lisivuruge nchi,” alisisitiza Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba.
Hata
hivyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye, aliitaka NEC kutokukaa kimya na kujibu hoja mbalimbali
zinazojitokeza ili kuondoa utata na dhana potofu zinazosambazwa na
baadhi ya watu kuhusu mfumo huo ambazo endapo hazitojibiwa kiuhakika
wananchi huziamini.
“Kuweni
wawazi, msichoke kuwafafanulia watu na kumbukeni kuwa zoezi hili ni
muhimu lisipofanyika vizuri tunaweza kujuta mambo yakiharibika.
“Nasema hivi kwa kuwa siku zote mambo yakiharibika au uongo ukisambazwa na kuaminiwa bila majibu, lawama zote huiangukia CCM,” alihadharisha.
Akijibu
changamoto zilizotolewa na viongozi wa vyama vya siasa, Lubuva alisema
watazifanyia kazi, huku akiongeza kuwa suala la ratiba itatolewa hivi
karibuni, lakini akadokeza kuwa, baada ya uandikishaji kuanza Njombe,
itafuatia mikoa mingine huku Zanzibar na Dar es Salaam zitakuwa za
mwisho.