NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Monday, August 10, 2015

Jiji la Dar Lasimama: Hapa Kuna Picha 8 za LOWASSA Akisindikizwa Ofisi za NEC na Maelfu ya Wananchi Kuchukua Fomu ya Urais

Picha  8  za  LOWASSA  Akisindikizwa  Ofisi  za  NEC  na  Maelfu  ya  Wananchi  Kuchukua  Fomu  ya  Urais







Friday, August 7, 2015

Wasomi Wampuuza Profesa Lipumba.......Wasema Amekurupuka



Wasomi mbalimbali nchini, wamepokea kwa mtazamo tofauti uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu wadhifa wake wa Mwenyekiti wa CUF Taifa wengine wakisema suala hilo si jipya bali ni aina ya changamoto zilizopo kwenye vyama vya siasa nchini.
 
Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti, wasomi hao pia walimshangaa Prof. Lipumba kwa uamuzi huo kwani alishiriki tangu mwanzo katika kumpokea mgombea urais aliyepitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Bw. Edward Lowassa, tangu alipohama CCM na kujiunga na CHADEMA.
 
Dkt. Lazaro Swai wa OUT
Akizungumzia uamuzi huo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Jamii katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dkt. Lazaro Swai, alisema anamshangaa Prof. Lipumba kwa uamuzi aliouchukua.
 
"Hizo ni aina ya changamoto zilizopo kwenye vyama vya siasa tangu vilipoanzishwa,  hilo ni shinikizo kutoka upande mmoja lakini si kutoka UKAWA wala CUF," alisema Dkt. Swai.
 
Aliongeza kuwa, hivi sasa katika vyama vya siasa kila mtu ana mvuto wa aina yake lakini kujiuzulu kwa Prof. Lipumba kutakuwa na mtikisiko kwa UKAWA na CCM kutokana na kuhama kwa Bw. Lowassa.
 
"Ujio wa Lowassa hauwezi kuipasua UKAWA, kujiuzulu kwa Lipumba kuna kitu ndani yake na kuleta mashaka kwa Watanzania, kwanini iwe sasa ndipo ajiondoe katika nafasi hiyo wakati alishiriki tangu mwanzo kumpokea Lowassa," alihoji.
 
Askofu Bagonza
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Karagwe, mkoani Kagera, Benson Bagonza, alisema kujiuzulu kwa Lipumba kunaashiria kuna jambo nyuma ya pazia, kwani wananchi hawataelewa.
 
"Tangu mwanzo alikuwa msingi imara kwenye UKAWA, ghafla anajiuzulu hiyo inashangaza watu wengi na sitaki kuamini kama amefikia uamuzi huo," alisema na kuongeza;
 
"Kutakuwa kuna jambo jingine limetokea nje ya UKAWA lakini swali la kujiuliza, kwanini alichelewa kuchukua uamuzi huo...huyo si Lipumba tunayemjua," alisema.
 
Dkt. Benson Bana
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Idara ya Sayansi ya Siasa ya Jamii, Dkt. Benson Bana, alisema kujiuzulu kwa Prof. Lipumba kulitarajiwa kutokana na mvutano uliokuwepo tangu awali.
 
"Ameona ni wakati mwafaka kuachia ngazi pia ni haki yake ya msingi kwani ndani ya muungano wa UKAWA, hauwezi kumpokea mtu wakati  huo huo akawa maarufu kushinda chama.
 
"Hilo ni pengo la kudumu ambalo haliwezi kuzibika kwa siku moja, uamuzi wa Lipumba na Slaa utakuwa wa halali kwani waliwekeza sana kwenye vyama vyao," alisema na kuongeza kuwa, kiongozi yeyote anapimwa kwa uadilifu na walikuwa tayari kujitoa kafara katika nyadhifa zao.
 
Julius Mtatiro
Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Bw. Julius Mtatiro, alisema hilo ni pigo kubwa kwa CUF na UKAWA hasa kipindi hiki cha kutafuta ushindi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa ujumbe wake alioutuma kwenye akaunti yake ya Facebook, Bw. Mtatiro alisema uamuzi huo ni mgumu kwani hajawahi kuusikia tangu awe mwanachama wa CUF miaka nane iliyopita.
 
Alisema kidemokrasia lazima kukubali matokeo na uamuzi binafsi wa mtu yeyote kwani mwisho wa siku, mtu hufanya uamuzi wake na tunalazimika kuyaheshimu ili maisha yaendelee.
 
 Aliongeza kuwa, si vizuri kumshutumu Prof. Lipumba kwenye mitandao na kwingineko bali akumbukwe kwa mchango wake mkubwa kisiasa ambapo jemedari anapoanguka vitani bunduki yake huchukuliwa na vita kuendelea.

Profesa Lipumba Aondoka Nchini Akiwa Chini ya Ulinzi



Saa chache baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutangaza kujiuzulu wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), ametoweka nchini.

Hata hivyo, haikufahamika mara moja amekwenda nchi gani na atakaa kwa muda gani.

Profesa Lipumba aliondoka nchini baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari katika Hoteli ya Peacok jijini Dar es Salaam, ambako alitangaza kujiondoa katika chama chake na katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Taarifa zilizopatikana, baada ya kumaliza mkutano na waandishi, alielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), na aliondoka nchini kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda (Rwanda Air).

Awali kiongozi huyo ambaye alivaa suti ya ‘dark blue’ na shati jeupe alikuwa apande ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) 485, lakini alibadili mwelekeo baada ya kufika uwanjani na kuamua kupanda Rwanda Air kuelekea Kigali saa 9 alasiri.

Chanzo cha uhakika kutoka uwanjani hapo, kilieleza  kuwa Profesa Lipumba, alifika saa 7:00 mchana akiwa na vijana wawili wa kiume ambao walionekana kama walinzi wake.

Katika muda huo ambao Profesa Lipumba alikuwa katika taratibu za kuondoka, palikuwapo na ndege nne tu za kwenda nje ya nchi.

Vijana hao ambao hawakujulikana majina yao, walikuwa wakifuatilia kila hatua ya kile alichokuwa akikifanya Profesa Lipumba, huku yeye akionekana mwenye wasiwasi na msongo mkubwa wa mawazo.

“Profesa Lipumba anaonekana hayuko katika hali ya kawaida, anaonekana ni mtu mwenye msongo wa mawazo, na pia ana wasiwasi kama vile kuna jambo linamsumbua.

“Macho yake yalionekana ni mekundu mithili ya mtu aliyekuwa akilia kwa muda mrefu, huku uso wake ukionekana hauna furaha,” kilisema chanzo chetu.

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amelazimika kukatisha shughuli za kiserikali alizokuwa nazo Zanzibar na kwenda jijini Dar es Salaam kunusuru hali ya sintofahamu ndani ya chama hicho.

“Ndiyo hivyo imeshatokea, lakini tayari katibu mkuu amekuja bara kuhakikisha mambo yanakaa sawa na chama hakiyumbi,” alisema kiongozi wa CUF ambaye hakupenda kutajwa jina

Friday, July 31, 2015

LOWASSA Aahidi Kuishinda CCM Uchaguzi Mkuu 2015


Waziri mkuu wa Zamani Edward  Lowassa  amewaahidi wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema pamoja na wale wa umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika oktoba 25 mwaka 2015.

Lowassa alisema hayo jana mara baada ya kukabidhiwa fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Demkorasia na Maendeleo ambayo itampa ridhaa ya kugombea urais kupitia umoja wa Katiba ya wananchi ukawa unaundwa na vyama vinne vya siasa nchini Tanzania ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, Cuf na NLD.

Aidha, Lowassa aliyekabidhiwa fomu na Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Freeman Mbowe katika ofisi za Chadema makao makuu yaliyopo Kinondoni jijini Dar es salaam jana,alichangiwa kiasi kadhaa cha pesa kitakachomsaidia katika yake ya matumaini iliyofufukia Ukawa. Katika hafla hiyo  Lowassa aliongozana na Mkewe pamoja na wana familia na ndugu wengine mbalimbali.

Mwanasheria mkuu wa Chadema Tundu Lissu alisema kwamba  ili mgombea ameweze kuwania urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ni lazima awe mwanachama wa chama chochote cha Siasa nchini Tanzania, hivyo Lowassa ni mwanachama halali wa Chadema pia amechaguliwa na vikao mbalimbali vya kamati kuu ya chama hicho iliyoketi hadi usiku wa manane.

Uamuzi wa Lowassa kugombea Urais ulipokelewa kwa shangwe na umati wa wananchi uliohudhuria hafla hiyo makao makuu ya Chadema kinondoni jijini Dar es salaam.

Mwanasiasa huyo Mkongwe atapambana  na Mgombea kutoka chama cha Mapinduzi Dk.John Magufuli katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu utakaokuwa wa aina yake  mwaka huu wa 2015

Lembeli ashinda kura za maoni Chadema, Bulaya almanusura.......Viti maalumu vyamuokoa


Wabunge wawili waliohama CCM hivi karibuni, James Lembeli na Ester Bulaya wamepitishwa katika kura za maoni kuwania ubunge kupitia chama chao kipya.

Wakati Lembeli akipitishwa kwa kura za kishindo kuwania ubunge katika Jimbo la Kahama Mjini, Bulaya alishinda katika nafasi ya viti maalumu baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha Jimbo la Bunda Mjini.

Wanasiasa hao sasa wanasubiri uteuzi wa Kamati Kuu ya Chadema utakaofanyika Agosti 5 na 6.

Ushindi wa Lembeli
Katika uchaguzi huo wa juzi, mbunge huyo wa zamani wa Kahama aliwabwaga wenzake 13 aliogombea nao akipata kura 168 kati ya 262 zilizopigwa, akifuatiwa na John Katibu aliyepata kura 45, Peter Shita (17) na Emmanuel Madoshi aliyepata kura 10.

Wengine ni Muta Nyerere (4), Felician Maige (4), Zacharia Obadia (3), Tadeo Mwati (2), Arnold Mtajwaka (2), Prosper Denga (2), Deusdedit Madinda (1), Reuben Macheyeki (1). Victor Mbwana na Richard Makingi waliambulia patupu. Katika uchaguzi wa viti maalumu, Winfrida Mwinula alishinda kwa kura 34 akifuatiwa na Salome Makamba aliyepata kura 30.

 Bulaya
Kama isingekuwa ni kura za maoni za viti maalumu zilizomfuta machozi, Bulaya alikuwa tayari ametupwa nje baada ya kuanguka katika Jimbo la Bunda Mjini.

Bulaya aliyekuwa miongoni mwa makada saba wa chama hicho waliokuwa wanawania kuliwakilisha jimbo hilo, alipata kura 37 kati ya 182 zilizopigwa akiwa nyuma ya Pius Masururi aliyeibuka mshindi kwa kura 65 na  Magembe Makoye aliyepata kura 40.

Baadaye katika mkutano wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), uliofanyika baadaye usiku, Bulaya alipata kura 71 kati ya 110 zilizopigwa na kuwabwaga Godliver Masamaki aliyepata kura 31, Joyce Sokombi (4), Minza Shani (3), Dk Jane Nyamsenda (1) na Alice Wandya aliyeambulia patupu.

Awali, Bulaya alikwaa kisiki baada ya jina lake kuwa miongoni mwa waliokatwa na kamati ya utendaji inayosimamia majimbo hayo wakidaiwa ni wageni katika chama; wapenda fujo na matabaka, akiwa pamoja na Chacha Nyamhanga, Sulemani Daudi lakini walirudishwa kundini baada ya kikao cha viongozi na watiania.

Katika Jimbo la Bunda Vijijini, Sulemani Daudi aliibuka mshindi kwa kura 84 kati ya 127 zilizopigwana kuwashinda John Masenza aliyepata kura 14, Dk Lucas Webiro (11), Frank Mongateko (8), Edgar Chibura (5) na Mathias Bandio aliyepata kura moja.

Tuesday, July 28, 2015

Hatupo tayari kuungana na chama kingine - TLP


Chama cha TLP kimesema hakipo tayari kuungana na chama kingine chochote kile kwa makubaliano ya kumsimamisha mgombea mmoja badala yake kitasimamisha mgombea wake makini ambaye ataingia katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya urais.

Kauli hiyo imetolewa na naibu katibu mkuu wa chama cha TLP taifa Dominata Rwechungura wakati akiongea na wananchi wa kata ya Kishogo wilayani Bukoba ambapo amewataka watanzania kuendelea kuwa na imani na chama hicho huku akiwasisitiza wananchi kutowasikiliza wanasiasa wanaopanda kwenye majukwaa na kuwarubuni.

Rwechungura ametoa tahadhari kwa watanzania ili wasikubali kununuliwa kwa gharama nafuu na wanasiasa wanaopitisha pesa kwa wananchi ili waweze kuchaguliwa hali ambayo inaweza kusababisha kupata viongozi wabovu wasio na sifa ya kuliongoza taifa.

Katika hatua nyingine naibu katibu mkuu wa TLP Dominata Rwechungura amelaani vikali juu ya wanasiasa wanao jilimbikizia pesa za walipakodi ambazo zilitakiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi huku makamu mwenyekiti wa TLP taifa Bw. Joas Kayura akiwataka watanzania kutofanya makosa katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutochagua viongozi wabovu badala yake wawe makini na kuchangua viongozi wazalendo wenye sifa za kuliongoza taifa kwa umakini

Wednesday, July 22, 2015

Ajali Mbaya ya Basi la Simiyu Express Yaua Watu Wengi Dodoma Usiku wa Kuamkia Leo


Taarifa kutoka mkoani Dodoma zinasema watu  zaidi  ya 10  wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo , huku zaidi ya abiria 40 wakijeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya SIMIYU EXPRESS walilokua wakisafiria kutoka Mwanza kwenda DSM kupasuka tairi na kuacha njia na kugonga mbuyu na kisha kupinduka.
 
Taarifa zinasema ajali hiyo ni mbaya sana kuwahi kutokea mkoani Dodoma.Majeruhi wamekimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu.