NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Tuesday, July 28, 2015

Hatupo tayari kuungana na chama kingine - TLP


Chama cha TLP kimesema hakipo tayari kuungana na chama kingine chochote kile kwa makubaliano ya kumsimamisha mgombea mmoja badala yake kitasimamisha mgombea wake makini ambaye ataingia katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya urais.

Kauli hiyo imetolewa na naibu katibu mkuu wa chama cha TLP taifa Dominata Rwechungura wakati akiongea na wananchi wa kata ya Kishogo wilayani Bukoba ambapo amewataka watanzania kuendelea kuwa na imani na chama hicho huku akiwasisitiza wananchi kutowasikiliza wanasiasa wanaopanda kwenye majukwaa na kuwarubuni.

Rwechungura ametoa tahadhari kwa watanzania ili wasikubali kununuliwa kwa gharama nafuu na wanasiasa wanaopitisha pesa kwa wananchi ili waweze kuchaguliwa hali ambayo inaweza kusababisha kupata viongozi wabovu wasio na sifa ya kuliongoza taifa.

Katika hatua nyingine naibu katibu mkuu wa TLP Dominata Rwechungura amelaani vikali juu ya wanasiasa wanao jilimbikizia pesa za walipakodi ambazo zilitakiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi huku makamu mwenyekiti wa TLP taifa Bw. Joas Kayura akiwataka watanzania kutofanya makosa katika uchaguzi mkuu ujao kwa kutochagua viongozi wabovu badala yake wawe makini na kuchangua viongozi wazalendo wenye sifa za kuliongoza taifa kwa umakini

Wednesday, July 22, 2015

Ajali Mbaya ya Basi la Simiyu Express Yaua Watu Wengi Dodoma Usiku wa Kuamkia Leo


Taarifa kutoka mkoani Dodoma zinasema watu  zaidi  ya 10  wamefariki dunia usiku wa kuamkia leo , huku zaidi ya abiria 40 wakijeruhiwa vibaya baada ya basi la kampuni ya SIMIYU EXPRESS walilokua wakisafiria kutoka Mwanza kwenda DSM kupasuka tairi na kuacha njia na kugonga mbuyu na kisha kupinduka.
 
Taarifa zinasema ajali hiyo ni mbaya sana kuwahi kutokea mkoani Dodoma.Majeruhi wamekimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa ajili ya matibabu.

Mbowe Asema UKAWA Wana Mgombea Makini.......Asema Atajulikana hivi punde


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe amesema pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika Ukawa, lakini wanajitahidi kumpata mgombea mmoja.
 
Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika jijini Mwanza, ambapo pia aliwatambulisha wabunge waliohamia Chadema kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge wa Kahama, James Lembeli na mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mara, Ester Bulaya.
 
Mbowe alisema viongozi wanaounda Ukawa, wanaendelea kushirikiana ingawa kuna changamoto kadhaa. Lakini, watatumia kila mbinu kuhakikisha anapatikana mgombea mmoja kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
 
“Tunaendelea kushirikiana lakini kuna changamoto, kama viongozi tutatumia kila mbinu tuwe na mgombea mmoja wa Ukawa na mazungumzo yoyote yanahitaji uvumilivu, kuheshimiana na kushirikiana,” alisema Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai.
 
Hata hivyo, Mbowe alisema umoja huo hautatangaza mgombea wao kwa haraka, kama ambavyo wananchi wanatarajia, kwa sababu tu CCM wamekwisha kumtangaza wao, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
 
“Tutamtangaza mgombea wetu kwa muda muafaka na watanzania wote watafurahi…hatuwezi kutangaza kwa sababu tu CCM wametangaza mgombea wao,” alisema Mbowe.

Tuesday, July 21, 2015

Mbunge wa Kahama Kupitia CCM, James Lembeli Atangaza Kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na CHADEMA


2015 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu Tanzania, kila siku stori za Siasa zimekuwa kwenye headlines nyingi kuanzia Magazetini, kwenye TV,  mitandaoni  na Radioni .

Mbunge James Lembeli alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili.. kuna habari za baadhi ya Wabunge wametangazwa kuhama Vyama vyao, Lembeli kathibitisha kuhama CCM kwa maneno yake mwenyewe.

"Nimetafakari, nimezungumza na mama yangu kwa zaidi ya saa kumi.. mke wangu na watoto wangu, na kwa kusikia kilio cha wananchi wa Jimbo la zamani la Kahama nimeamua kutangaza kuanzia leo kwamba natangaza kujiondoa uanachama wangu ndani ya CCM" - James Lembeli.

"Nilikipenda lakini nimelazimika kuchukua uamuzi huu, najua nawakera wengi lakini nawaomba waangalie hali ambayo Viongozi wa CCM Wilaya ya Kahama wamesababisha niamue uamuzi huu mgumu.

"Kuanzia leo najiunga na CHADEMA… Namshukuru Rais Kikwete, nafikiri atakuwa mtu wa kwanza kuamini haya ninayosema, mwaka 2010 mizengwe iliyofanyika lengo lake ilikuwa kukata jina langu, kila mtu anafahamu Rais mwenyewe aliwahi kuniambia lakini Rais Kikwete ndiye aliyerudisha jina langu… Ninaahidi nitaendelea kufanya kazi nae mahali popote, na MUNGU naomba anisaidie niweze kuvuka salama katika haya"- James Lembeli.

Monday, July 20, 2015

MAJAMBAZI WALIOVAMIA STAKISHARI, WAKAMATWA

Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limefanikiwa kuwakamata majambazi watano wanaodaiwa kuhusika na tukio la uvamizi katika kituo cha polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema Majambazi hao wamekamatwa Mbagala ambapo katika tukio hilo pia wamekamata pia fedha shilingi milioni 170 na bunduki 16 miongoni mwao ni zile zilizoibiwa katika kituo cha Stakishari.
East Africa Television (EATV)'s photo.

ESTHER BULAYA AITOSA CCM



Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Chama Cha CCM, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Esther Bulaya mbunge machachari , kuitosa CCM kwa kutangaza uamuzi wake wa kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho
CHANZO CHA HABARI ..... EAST AFRICA TELEVISION

Benard Membe Atangaza Kuachana Na Siasa.......Asema Hatagombea Wadhifa Wowote Mwaka Huu


Waziri wa Mambo ya Nje na  ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe, amesema hatogombea wadhifa wowote kwenye uchaguzi mkuu wa  mwaka huu na kwamba anapanga kujishughulisha na masuala yake ya kibinafsi.

Membe ambaye alikuwa akitafuta tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania urais mwezi Oktoba lakini akashindwa kufikia lengo hilo, amesema kuwa, hatotafuta nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtama.

Hata hivyo amesema ataendelea kukiunga mkono chama chake cha CCM na atampigia debe mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Bw. John Magufuli.

Awali kulikuwa na tetesi kwamba Membe angegombea ubunge baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Huku hayo yakijiri, chama cha Mapinduzi  (CCM) kinaendelea kupata pigo baada ya baadhi ya wabunge wake kutangaza kuwa hawatogombea tena nafasi zao kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Tayari madiwani 20 wa CCM katika jimbo la Monduli wametangaza kuhamia Chadema na kumtaka mbunge wao, Edward Lowassa kufuata mkondo huo.