NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Thursday, July 16, 2015

Wakenya kumpokea Obama wakiwa uchi ?


Kundi la Wakenya, limejiapiza kumkaribisha rais wa Marekani, Barack Obama, nchini kwao wakiwa hawajavaa nguo ili kuonesha kuwa hawajakubaliana na kitendo cha kuruhusu mapenzi ya jinsia moja.
 
Obama anatarajiwa kutembelea Kenya kwa mara ya kwanza tangu kuwa rais na kutegemea kuwa na mkutano na wafanyabiashara kuanzia Julai 24-26 mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa barua iliyosambazwa na kundi hilo la wakenya, imedai kuwa watafanya maandamano ya amani jijini Nairobi, Julai 22 na 23 mwaka huu kuanzia Uhuru kona.
 
Wamedai kuwa maandamano hayo yatafanywa na wanawake pia wanaume takriban 5,000 wakiwa watupu bila nguo yoyote kupinga Umoja wa nchi za Amerika kupitisha sheria ya mashoga kutambuliwa kisheria.
 
Wamesema lengo kuu la maandamano wakiwa uchi ni kumuonesha na kuelewesha rais Obama, utofauti uliopo kati ya wanawake na wanaume.
 
Wiki iliyopita, Wakenya hao walienda katika mitaa kuandamana wakimuonya rais Obama, kutothubutu kuzungumzia suala la haki za mashoga kwenye ziara yake ya kutembelea nchi hiyo.
 
Mbunge Charles Njagagua, pia aliwataka wabunge kumfukuza Obama, nje ya Bunge mara moja akigusia haki za mashoga.
 
Naye Makamu wa rais nchini Kenya, William Ruto, hivi karibuni alinukuliwa na vyombo vya habari akiwaambia wananchi wake kuwa wamesikia kuwa Marekani wameruhusu uhusiano wa mashoga na mambo mengine yasiyo na maadili na kuwataka viongozi wa dini kutetea nchi yao na kusimamia imani ya nchi yao.

Sunday, July 12, 2015

Nafasi ya Urais CCM........Magufuli Apata Ushindi wa Kishindo



Chama  cha  mapinduzi, CCM kimemteua  Dr .Magufuli  kuwa  mgombea  wa  Urais  2015.

Uteuzi wa  Dr. Magufuli  umetokana na  ushindi  wa  kishindo  alioupata  baada  ya  mkutano  mkuu  kukutana jana   usiku  kwa  ajili  ya  kupiga  kura  ili  kupata  jina moja  kati  ya  matatu  yaliyokuwa  yamependekezwa  na  Halmashauri  kuu  ya  CCM.
 Matokeo  ni  kama  ifuatavyo
1.Magufuli.....87%
2. Amina.......10%
3.Migiro......3%

Thursday, July 9, 2015

Dewji Atangaza Kutogombea Tena Ubunge Singida Mjini


Mbunge wa Singida Mjini (CCM) na mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji amewaliza baadhi ya wapigakura wake wakati akitangaza kutogombea tena nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa ya madai ya kubanwa na majukumu ya kifamilia na biashara. 
 
Dewji ambaye amekuwa mwakilishi wa jimbo hilo kwa awamu tatu mfululizo, alitangaza uamuzi wake huo kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi.
 
Alisema kuwa aliomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Singida Mjini mwaka 2000, hakuwa na familia na pia biashara zake hazikuwa kubwa kama ilivyo sasa.
 
Alisema katika kipindi chote cha uwakilishi wake, wakazi wa Singida Mjini wamempa heshima kubwa, ukarimu wa hali ya juu, wema uliotukuka na uvumilivu usio na kifani na kwa hali hiyo, hatawasahau kamwe na ataendelea kuwatumikia kupitia mfuko maalumu aliouanzisha.
 
Aliwataka wakazi hao kuendeleza moto wa maendeleo waliouwasha miaka 10 iliyopita kwa miaka mingine kama hiyo ijayo ili jimbo hilo lipige hatua zaidi.
 
“Kwa kutambua heshima mliyonipa na imani kubwa mliyonionyesha kwa vipindi vyote vya uongozi wangu, ingawa nina huzuni lakini sina budi niwaombe kuwa mwaka huu wa uchaguzi sigombei tena na ninatoa fursa kwa kada mwingine wa CCM anipokee kijiti hiki kuliongoza jimbo letu,” alisema kwa huzuni. 
 
Baada ya kutamka maneno hayo, wananchi wengi katika walipiga kelele kwa nguvu wakionyesha kutokubaliana na uamuzi wake. Huku moja ya sauti ikisikika... “Hatutaki mbunge mwingine ni wewe tu hadi tukuchoke.”
 
Awali, Dewji alitaja baadhi ya maendeleo yaliyofanyika katika vipindi vyake, kuwa ni pamoja na kujenga shule 15 za sekondari kutoka mbili zilizokuwapo.
 
Alisema kwa kutumia fedha zake alijenga na kuchimba visima 45 vya majisafi na salama.

Wednesday, July 8, 2015

Mchungaji Mtikila Atangaza Kuwafikisha Mahakamani Wasaka Urais 6 wa CCM......Yumo Lowassa, Sumaye,Membe,January Wassira na Ngeleja


CHAMA cha Democratic Party (DP) kimetangaza kwenda mahakamani kukishtaki Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na makada wake sita kutokana na kukiuka sheria ya nchi, taratibu pamoja na kanuni za uchaguzi.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama hicho Mchungaji Christopher Mtikila, wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alisema makada hao pamoja na chama chao wamekiuka sheria za nchi pamoja na kanuni za uchaguzi.

Aliwataja makada ambao atawaburuta mahakamani kuwa ni Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa pamoja na Frederick Sumaye.
 
Wengine ni January Makamba, William Ngeleja, Stephen Wassira pamoja na Benard Membe. Alidai makada hao walivunja sheria za nchi pamoja na kanuni za uchaguzi kutokana na kuanza kampeni zao mapema.

Alisema  watakishtaki Chama Cha Mapinduzi kutokana na kushindwa kuwachukulia hatua na kuendelea kuwaweka katika mchakato wa kutafuta mgombea wa urais wa chama hicho wakati walishavunja sheria pamoja kanuni za uchaguzi, kwahiyo walitakiwa kukatwa mapema kabisa.

"Watu wameanza kampeni mapema na kwa kufuata sheria ya nchi taratibu  pamoja na kanuni za uchaguzi ni kwamba watu hao wamevunja Sheria kwa hiyo tunapeleka kesi mahakamani kuwashtaki wao pamoja na chama chao kwa kuvunja sheria," alisema Mtikila na kuongeza;

"Tunaenda mahakamani kuishtaki CCM iliyochezea uhuru wetu kwa miaka 54 pamoja na hawa watu wao kwani hawafai na hii nchi inapoelekea ni kubaya."

Alisema uchaguzi wa mwaka huu hautakuwa halali kama sheria hazitafuatwa na kudai kuwa vitu vinavyounyima uchaguzi wa mwaka huu uhalali ni pamoja na watu kuvunja sheria kwa kuanza kampeni mapema.

Alisema inashangaza kuona pesa zinatumika bure bila sababu ya msingi na kudai kuwa ni uhalifu mkubwa tena wa kimataifa. 
 
Alisema watu wanaotumia pesa wakiachwa kitatokea kitu kibaya nchini, hii ni mbaya sana kwani pesa zinazotumika kwa sasa lazima ijulikane zinatoka wapi.

Alisema fedha hizo zinazotumika ipo  siku zitakuja kurudi mahali pake kwa hao watu wanaozitoa.

Aliendelea kusema kuwa inashangaza kuona watu wanatumia pesa  kutafuta urais. Mtikila alimshukia moja kwa moja Lowassa akisema hastahili kupewa nafasi hiyo.

"Lowasa hastahili nafasi hiyo na wanasheria wetu wapo katika maandalizi ya kuandaa kesi kwa ajili ya kuwapeleka mahakamani," alisema Mtikila.

Alisema endapo wataona katika chama chochote kuna vitendo kama ambavyo havifai hawatasita kufuata utaratibu wa kwenda mahakamani endapo watakuwa na ushahidi wa kutosha. 
 
Alisema DP ipo kwenye maandalizi na wakati ukifika watu wote watafikishwa mahakamani.

Sunday, July 5, 2015

Wabunge 35 wa UKAWA Wafukuzwa Bungeni


Wabunge  35 wa kambi ya upinzani bungeni jana walitolewa nje ya ukumbi wa bunge na spika wa bunge  Anne Makinda na kupewa adhabu ya  kutokuhudhuria vikao vitano kwa madai ya kukiuka kanuni za bunge .
 
Mara baada ya kikao cha bunge kuanza spika wa bunge alinza kwa kuwakumbusha wabunge namna ya kufuata kanuni hasa pale wanapotaka kuondoa muswada wowote.
 
Hali ilibadilika ghafla Bungeni baada ya Mbunge Ezekiel Wenje kuomba Spika atoe ufafanuzi wa kwanini Mbunge Silinde hayuko kwenye list ya waliotajwa kusimamishwa lakini Askari wa Bunge wamemzuia asiingie kwenye Kikao?
Majibu ya Spika hayakuwaridhisha baadhi ya Wabunge, zikaanza tena kelele… ndipo spika aliamua  kuwatoa nje.
 
Hata hivyo baada ya vurugu zote kuisha miswada yote mitatu ambayo ni  ya sheria ya petroli, sheria ya usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi pamoja na sheria ya uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uchimbaji Tanzania iliwasilishwa Bungeni.
 
Majina ya Wabunge waliotimuliwa  ni,
  1. Ezekiel Wenje
  2. Mussa Kombo
  3. Masoud Abdallah Salim
  4. Rebecca Ngodo
  5. Sabrina Sungura
  6. Khatib Said Haji
  7. Dr. Anthony Mbassa
  8. Maulidah Anna Valerian Komu
  9. Kulikoyela Kahigi
  10. Cecilia Pareso 
  11. Joyce Mukya
  12. Mariam Msabaha 
  13. Grace Kiwelu
  14. Israel Natse 
  15.  Mustapha Akonaay
  16. Konchesta Rwamlaza
  17. Suleiman Bungura 
  18. Rashid Ali Abdallah 
  19. Ali Hamad
  20. Riziki Juma
  21. Rukia Kassim Ahmed
  22. Azza Hamad
  23. Khatibu Said Haji
  24. Kombo Khamis Kombo
  25. Ali Khamis Seif
  26. Haroub Mohammed Shamisi 
  27. Kuruthum Jumanne
  28. Mchuchuli
  29. Amina Mwidau
  30. Mkiwa Kimwanga
  31. Salum Baruhani 
  32. Marry Stellah Malaki
  33. Rashid Ally Omary
  34. Mwanamrisho Abama
  35. Lucy Owenya

Saturday, July 4, 2015

ACT yailalamikia CHADEMA kuhujumu mikutano yake


CHAMA cha Alliance for Change and Transparency(ACT), kimebaini kuwepo kwa mipango inayoratibiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kuhusika kuhujumu mikutano yake mbalimbali.
 
Hujuma hizo zimebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Mipango na Mikakati Taifa  wa ACT Habibu Mchange, aliyesema kuwa chama hicho kimekuwa kikihangaikia ACT na kusahau kushughulikia matatizo ya watanzania.
 
“Chadema wamekuwa wakitufuatilia kila mahali tunapofanya mkutano na hilo wamekuwa wakifanya kwa sababu ya kutuhofia. Kwa mfano tulipokuwa na mkutano Mwanza na wao wakatangaza kufanya tukawashinda, kesho tumetangaza kufanya mkutano na wao wametangaza kufanya Kawe.
 
“Chadema tunawaonea huruma kwa kuwa tutawafanya kitu ambacho hawatasahau katika historia ya siasa za tanzania kwa sababu njia nyingi wanazotumia ni zile tulizoziratibu wakati tukiwa huko,”alisema Mchange.
 
Katika hatua nyingine Mchage alisema baada mbalimbali mikoani hivi sasa ACT kupitia viongozi wake  wa kitaifa wameandaa kufanya mkutano mkubwa kesho jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga.
 
“Mkutano huo utatoa fursa ya kuzindua Ilani ya jiji la Dar es salaam, itakayotokana na ilani Kuu  ya chama ili kukabiliana na kero mbalimbali za jiji.
 
“mkutano huo utatoa fursa ya ACT kuwataka watanzania kuishi katika misingi ya haki, undugu, umoja na mshikamano kwa kutumia azimio la Tabora lilozinduliwa na chama hicho likiwa limewisha azimio la Arusha,”alisema.
 
Chama hicho kinatarajia kusimamisha madiwani, wabunge na nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
 
Akizungumzia tuhuma hizo msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema chama hicho hakina muda wa kuzungumzia tuhuma ambazo hazina mashiko.

Thursday, July 2, 2015

Urais 2015: UKAWA Waahidi Neema Kwa Wachimbaji


SERIKALI itakayoundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) imeahidi kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogowadogo ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo katika shughuli za uchimbaji wa madini huku ikihakikisha kuwa kampuni kubwa za uwekezaji zikilipa kodi stahiki ya Serikali.
 
Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahimu Lipumba, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Kahama katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja CDT mjini hapa.
 
Lipumba alisema kuwa kwa sasa Serikali imekuwa haiwajali wachimbaji wadogowadogo wa madini hususani wa madini ya dhahabu ambapo wamekuwa wakigundua maeneo yenye madini kisha baadaye huondolewa na Serikali kwa kile kinachodaiwa kuwa hawana leseni za kumiliki maeneo hayo.
 
Alisema kuwa wachimbaji hao wamekuwa waathirika kila wanapoibua maeneo ya mgodi kwani hutolewa badala ya Serikali kuwajengea uwezo wa uchimbaji pamoja na kuwaongezea mitaji hali ambayo ingesaidia kupunguza kukosekana kwa ajira tatizo ambalo ni kubwa kwa vijana nchini.
 
Aidha Lipumba aliitaka Serikali kutokuwakumbatia wawekezaji wakubwa hasa wa madini na kuwasahau wale wadogo ambao ndio chanzo cha kupatikana kwa maeneo ya uchimbaji na kuwa chanzo cha kukua kwa miji midogo katika maeneo ya uchimbaji wa madini.
 
Pamoja na mambo mengine Lipumba alisisitiza kwa Serikali kuwatafutia wakulima wa zao la tumbaku na pamba masoko ya uhakika yatakayoleta tija kwa wakulima na kuondokana na malalamiko yaliyopo kwa wakulima wa mazao hayo kwa sasa katika Kanda ya Ziwa.
 
Pia Lipumba alisema Ukawa itakapoingia madarakani haitatoa nafasi kwa kampuni kubwa kusamehewa kodi kwani kwa kufanya hivyo kunarudisha nyuma maendeleo ya taifa na kukosekana pato ambalo linaweza kuwasaidia wajasiriamali wadogo ambao hawana kipato kwa sasa.