NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Monday, February 16, 2015

Rais Kikwete aongoza maziko ya Chifu Abdul Mkwawa ambapo Mwanafunzi wa Miaka 13 Ametawazwa kuwa Chifu Mpya wa Wahehe, akirithi nafasi ya baba yake


Mwanafunzi wa Darasa la Saba, Adam Abdul Sapi (13) ametawazwa kuwa Chifu mpya wa Wahehe, akirithi nafasi ya baba yake, aliyefariki na kuzikwa mkoani Iringa.

Rais  Jakaya Kikwete alishiriki maziko ya Chifu huyo wa Wahehe, Abdul Sapi Mkwawa (66)  yaliyokwenda sanjari na hafla ya kumsimika mtoto huyo kushika wadhifa huo wa kimila.
 
Maziko ya kiongozi  huyo aliyefariki Februari 14, mwaka huu, yalifanyika katika kijiji cha Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa ndani ya makumbusho yaliyowekwa  fuvu la babu yake,Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa.
 
Mbali na Rais Kikwete, wengine waliohudhuria maziko hayo ambayo taratibu zake zilitumia takribani saa 2.30 kuanzia saa 7 mchana ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania Bara, Phillip Mangulla, wakuu wa mikoa ya Iringa na Mbeya na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa.
  
Kabla ya kifo chake kilichosababishwa na maradhi ya sukari na figo, Abdul Sapi Mkwawa aliyekuwa mtoto wa tatu wa Spika wa kwanza mweusi nchini, Adam Sapi Mkwawa, alikuwa akifanyakazi katika kiwanda cha maji Afrika cha Kidamali, Iringa.
 
Amewahi pia kufanyakazi katika Chama cha Wazalishaji Tumbaku Iringa na Shirika la Elimu Supplies.
 
Alizaliwa Mei 4, 1949 katika kijiji cha Kalenga na kupata elimu ya msingi katika shule za Kalenga na Tosamaganga kati ya mwaka 1956 na 1963.
 
Mwaka 1964 hadi 1970 alijiunga na shule ya sekondari Iyunga na Mkwawa, ambako alipata elimu ya kawaida na ya juu ya sekondari kabla ya kujiunga na elimu ya juu ya biashara na utawala 1971 hadi 1973.
  
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Hussein Sapi alisema mpaka umauti unamkuta, Abdul Sapi Mkwawa alikuwa mtwa (chifu);  alisimikwa mwaka 1999 baada ya kifo cha baba yake, Adam Sapi Mkwawa aliyefariki Juni 25, 1999.
 
Kabla ya maziko ya Chifu huyo, wazee wa kabila la Wahehe walimsimika Adam ambaye ni mtoto wake wa tano kuwa chifu mpya wa kabila hilo.
 
Hata hivyo, mtoto huyo anayesoma katika shule ya msingi ya Highlands ya mjini Iringa, atalazimika kusubiri kufanya shughuli za kichifu mpaka atakapotimiza umri wa miaka 20.
 
Tangazo lililotolewa mbele ya Rais na ndugu wa karibu wa familia hiyo, Joseph Mungai, ilisema mdogo wa marehemu, Saleh atashikilia wadhifa huo mpaka mtoto huyo atakapofikisha umri huo.
 
Baada ya maziko , Rais Kikwete na msafara wake walizungumza na familia ya marehemu kijijini hapo.

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta Amsimamisha Kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),Madeni Kipande


Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Madeni Kipande kutokana na kile kilichoelezwa kuwa uendeshaji mbovu wa utoaji wa zabuni.

Aidha, amemteua Awadhi Massawe kushika wadhifa huo. Kabla ya uteuzi huo, Massawe alikuwa Meneja wa Bandari.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, Sitta alisema uamuzi huo umetokana na kuwapo malalamiko ya kutofuatwa kwa taratibu za zabuni na ucheleweshaji wa barua kwa wanaoshinda.
 
“Ni muhimu sana taratibu zetu za ununuzi katika bandari ziwe wazi na ziheshimike duniani kote, maana miradi hii ni mikubwa sana inayopitishwa na bodi ya zabuni ya TPA,” alisema.
 
Sitta alisema,  aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Dk Harrison Mwakyembe alianza kushughulikia masuala hayo, lakini hayajakaa vizuri. Alisema hakuna uwazi na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, ikiwemo kubadilika majina ya kamati za kutathmini zabuni.
 
Wakati huo huo  Sitta ameunda timu ya watu sita itakayochunguza tuhuma za Kipande. Imepewa wiki mbili iwe imefanya kazi hiyo.
 
Timu hiyo itaongozwa na Jaji mstaafu, Augusta Bubeshi na Katibu wake, Deogratius Kasinda ambaye ni mtumishi wa Wizara ya Uchukuzi.
 
Wajumbe wengine wa timu hiyo ni Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Manunuzi ( PPRA) Dk Ramadhani Mlinga, Samson Lugigo , Happiness Senkoro na Flavian Kinunda ambao walishawahi kushika nyadhifa za juu ndani ya TPA.
 
“Nimejitahidi kuchukua hawa wastaafu kwa sasa hivi hawatafuti cheo chochote, naamini watatenda haki, watachunguza tu bila kufanya uonevu,” alisema Sitta.
 
Waziri Sitta alisema bandari ni eneo muhimu, kwani takwimu zinaonesha kwamba asilimia 43 ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yanatokana na kodi ya ushuru wa forodha. Kati ya makusanyo hayo, asilimia 87 yanakusanywa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
 
Kwa upande wa Kipande,  alisema hawezi kupinga hatua iliyochukuliwa na waziri .
 
Hata hivyo, alisema anaamini kipindi chote cha uongozi wake, alifanya ambayo yalikuwa sahihi na hana wasiwasi na uamuzi huo.
 
"Mimi sina wasiwasi na hilo sababu huo ni uamuzi wake; lakini nina imani kuwa katika bandari hii, nimefanya kile ambacho nilikuwa natakiwa kufanya,  hivyo sina shaka na hilo," alisema Kipande.
 
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto ametaka serikali kujenga matangi ya kuhifadhia mafuta na kujenga bomba la mafuta kwenda mikoani.
 
Aidha, kamati hiyo imetaka TPA kuangalia uwezekano wa kununua hisa 50 za Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (Tiper) imilikiwe kwa asilimia 100 na Serikali.
 
Kuhusu ujenzi wa matangi, Zitto alisema hatua ya Serikali kujenga matangi yake ya kuhifadhi mafuta, itasaidia kujua kiasi cha mafuta yanayoingia na kuweza kukadiria kodi kwa uhakika.
 
Akitoa mfano wa Kenya, alisema Serikali inamiliki matangi ya kuhifadhia mafuta,  wanayapima kujua kiasi cha mafuta kilichoingia na kukitoza kodi  kabla ya kupelekwa kwenye matangi ya waagizaji.
 
“ Walichofanya, wamemtaka kila muagizaji kuwa na flow meter  yake na yakitoka kwenye meli yanaingia kwenye matangi ya Serikali na baada ya kujua kiasi na kutozwa kodi hupelekwa kwa walionunua,” alisema.
 
Zitto  alisema wakati umefika sasa kwa serikali kujenga mabomba ya kusafirishia mafuta na kwa kuanzia yakawa matatu, ambayo yatasaidia kuondoa mfumo wa sasa wa kusafirisha kwa magari.
 
“Linaweza kujengwa bomba moja kwenda Mbeya, likawa na matoleo kwa ajili ya mikoa ya Morogoro, Iringa na mikoa iliyo jirani, kwa kufanya hivyo tutaondoka na hali ya sasa ya kusafirisha mafuta kwa magari,”alisema.
 
Alisema katika kuimarisha reli, ni vyema ukaanzishwa mfumo wa kutoza kodi asilimia 1.5 kwa kila bidhaa inayoingia nchini na fedha hizo ziimarishe usafiri wa reli.
 
“Kwa sasa asilimia 99 ya mizigo inasafirishwa kwa barabara, hili si jambo jema kwa uchumi, najua nikisema hivyo wenye malori watalalamika, lakini wanaweza kufanya biashara nyingine,” alisema.
 
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPA, Awadhi Massawe alisema asilimia 60 ya mafuta yanayoingia nchini hupitia kwenye boya la Single Buoy Mooring (SBM).
 
Alisema wamejipanga kujenga mita ya kisasa ya kupimia mafuta maeneo ya Kigamboni huku ile ambayo haitumiki, wamepanga kuiboresha na kuwa ya kisasa.
 
Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa gati namba 13 na 14 ambazo zabuni  yake iliingia utata, Massawe alisema ripoti ya maandishi wataipeleka kwa Kamati hiyo ya Bunge ifikapo Machi Mosi mwaka huu.
 
Pia, Massawe alisema hatua ya kitengo cha kupakua kontena kupewa mtu binafsi, inawapunguzia mapato na kuwa hiyo ndio sekta ambayo inaingiza fedha nyingi.
 
Alisema ili kupambana na hali hiyo, wamejipanga kuimarisha gati namba 1 hadi 7 na kuongeza kina cha bahari ili kuweza kupakua makasha na kuwa kwa mwaka jana waliweza kupakua makasha laki mbili.

Friday, February 13, 2015

Rais Kikwete Afuta ADA ya shule za Sekondari Nchi Nzima


HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ametimiza ahadi yake aliyoitoa Agosti mwaka jana katika Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro, kwamba amekusudia kufuta ada ya shule za sekondari nchi nzima.
 
Akizindua Sera mpya ya Elimu na Mafunzo 2014 katika Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, Kipawa jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alitangaza kufutwa kwa ada ya sekondari, kuanzia mwakani.
 
Kwa tangazo hilo, Bajeti ya mwisho ya uongozi wa Rais Kikwete itakayoanza kujadiliwa Mei mwaka huu, itatakiwa kuwa na fungu la kulipa gharama ambazo wananchi wamekuwa wakitoa kwa watoto wao wanaosoma elimu ya sekondari katika shule za Serikali nchi nzima.
 
Kwa sasa wazazi wamekuwa wakilipa Sh 20,000 kwa shule za kutwa na Sh 70,000 kwa shule za bweni, ili watoto wao wapate elimu ya sekondari.
 
Ubora
Alisema sera hiyo imezingatia stadi za msingi ambazo ni kuandika, kusoma na kuhesabu, ili kuwezesha watoto kujengwa kwenye msingi mzuri na hata kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hilo limezingatiwa.
 
“Hata kwenye mpango wa BRN tumelizungumza ili kuhakikisha inatolewa elimu bora. Tusifanye mambo ya kuchekesha mtoto anafika madarasa ya juu hajui kuandika, kusoma na kuhesabu.
 
 “Kuanzia sasa kama mtoto anafika darasa la pili, hajui kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), ni bora asiende darasa la tatu…naamini watoto wakiimarishwa katika stadi za KKK itaondoa matatizo haya,” alisema.
 
Tathimini ya Msingi ya Taifa kwa ajili ya uwezo wa wanafunzi katika KKK, kwa wanafunzi wa Darasa la Pili iliyofanyika mwaka jana, ilibaini kuwa asilimia 98 ya wanafunzi wa Darasa la Pili nchini, walikuwa hawaelewi wanachokisoma.
 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema, tathimini hiyo imefanywa kwa baraka za Wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), ili kupata taarifa kuhusu hali halisi ilivyo ya wanafunzi wa Tanzania kumudu stadi za KKK wanapofika Darasa la Pili.
 
Mafanikio
Mbali na mafanikio ya kufikia uwezo wa kuanza kutoa elimu ya msingi na sekondari bure, huku msisitizo ukiwekwa katika utoaji wa elimu bora, Rais Kikwete pia ilitangaza mafanikio mengine katika sekta ya elimu ambayo yamefikiwa katika uongozi wake wa miaka kumi.
 
Rais Kikwete alisema sasa elimu imepewa kipaumbele katika sera na shughuli za serikali, ndio maana Bajeti ya Elimu, ndio kubwa kuliko bajeti zote.
 
Alifafanua kuwa mwaka 2005/06 bajeti hiyo ilikuwa Sh bilioni 6.7, wakati mwaka huu wa fedha imepanda na kufikia Sh trilioni 3.1.
 
Hatua hiyo ya kibajeti kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni ongezeko la mara tano ya Bajeti ya mwaka 2005 sawa na asilimia 20 ya Bajeti ya Serikali ambayo inatengwa kwa ajili ya elimu.
 
Katika suala la mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema imetoka Sh bilioni 56 kwa mwaka wa fedha 2005/06, hadi kufikia Sh bilioni 345 kwa mwaka huu wa fedha.
 
Aidha, kwa mwaka jana, wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu, waliongezeka kutoka wanafunzi 16,000 mwaka 2005 hadi kufikia 95,000.
 
Kwa upande wa shule za msingi, alisema zimeongezeka kutoka 14,000 kwa mwaka 2005 hadi kufikia shule 16,343 kwa mwaka 2014, huku shule za sekondari zikiongezeka kutoka 531 kwa mwaka 2005, hadi kufikia 4,576, mwaka 2014.
 
Idadi wanafunzi wanaojiunga na sekondari, Rais Kikwete alisema imeongezeka kutoka wanafunzi 524,325 mwaka 2005 na kufikia wanafunzi milioni 1.8.
 
Rais Kikwete alisema pia vyuo vya ufundi vimeongezeka kutoka vyuo 184 mwaka 2005 na kufikia vyuo 744 kwa mwaka 2014, huku vyuo vikuu vikiongezeka kutoka vyuo vikuu 26 mwaka 2005 na kufikia vyuo vikuu 50 kwa mwaka 2014.
 
Alikumbusha kuwa kama sio kuanzishwa kwa shule za kata, idadi ya wanafunzi pia isingeongezeka.
 
“Hali imebadilika, sasa wanafunzi wengi wanakwenda shule na vyuoni na suala la watoto na vijana kupata fursa ya kusoma, sio tatizo katika sekta ya elimu, sasa kinachotakiwa ni kuhakikisha inapatikana elimu bora kwa kuboresha mazingira ya elimu,” alisema Rais Kikwete

Thursday, February 12, 2015

Uandikishaji Wapiga Kura kwa BVR Wasogezwa Mbele na Utaanza Februari 23, 2015


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema katika majaribio ya uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, mfumo mpya wa uandikishaji wa 'Biometric Voter Registration Kit' (BVR), umefanikiwa kwa asilimia kubwa licha ya changamoto kadhaa, na ina uhakika mfumo huo utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika daftari hilo bila matatizo.

Aidha, Tume hiyo imebadilisha tarehe ya kuanza rasmi uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu uliokuwa uanze Februari 16, katika mkoa wa Njombe, hadi Februari 23, mwaka huu, ili kutoa nafasi kwa wadau kuweza kujiandaa vyema. 
 
Pamoja na hayo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wameonesha wasiwasi juu ya utaratibu mzima wa uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu kupitia BVR, kuwa kama utafanyika na kumalizika kwa wakati, kutokana na tume hiyo kuchelewa kufanya mambo mengi, ikiwemo elimu ya uraia na kutoa ratiba ya uandikishaji. 
 
Akifungua mkutano ulioandaliwa na tume hiyo kwa ajili ya kukutana na vyama vya siasa kujadili uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Damian Lubuva, alisema tume hiyo ilianza utaratibu wa majaribio ya uandikishaji kwa kutumia mfumo huo katika mikoa mitatu ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro na Katavi.
 
“Kwa ujumla uandikishaji ulifanyika vizuri na kwa mafanikio katika maeneo yote, idadi ya watu walioandikishwa pia katika maeneo hayo iliongezeka na kuvuka lengo ambalo tume iliweka kwa zaidi ya asilimia 100 licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa, hii ni dalili nzuri kwamba mfumo huu utafanikiwa,” alisema Jaji Lubuva. 
 
Alisema tume hiyo katika eneo la Kawe mkoani Dar es Salaam ililenga kuandikisha wananchi 14,312, lakini waliandikishwa wananchi 15,123 sawa na asilimia 105.67, Kilombero mkoani Morogoro waliandikishwa wananchi 19,188 wakati lengo la Tume lilikuwa wananchi 17,290 sawa na asilimia 110.9. 
 
“Pia katika mkoa wa Katavi, wilayani Mlele, tuliweka lengo la kuandikisha wananchi 11,104 lakini kupitia mfumo huu wa BVR ambao katika kila kituo tulitumia BVR kit 80, tuliandikisha wananchi 11,210,” alisisitiza. 
 
Aliwahakikishia wanasiasa hao kuwa, kutokana na majaribio ya mfumo huo katika mikoa hiyo, pamoja na kubaini changamoto kadhaa, tume hiyo ina uhakika mfumo huo ni imara na unaweza kutumika kuandikishia Watanzania wote katika muda uliopangwa bila matatizo. 
 
Hata hivyo, alisema tume hiyo imebadilisha muda wa kuanza uandikishaji kutoka Februari 16 hadi 23, mwaka huu, ambapo katika mkoa wa Njombe pekee wanatarajia kutumia vifaa vya BVR takribani 250 huku vifaa vingine 7,050 vikisubiriwa kuwasili nchini kwa ajili ya uandikishaji kuendelea maeneo mengine. 
 
“Suala la ratiba tunalifahamu na tutaitoa muda wowote, tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya vifaa hivi ambavyo vinatokea China, awamu ya kwanza vifaa takribani 2,000 vitawasili wiki ya kwanza ya mwezi Machi, napenda nitoe wasiwasi, Tume iko huru, wazi na haina chochote inachokificha wala kutumika na mtu,” alisema. 
 
Aidha, Jaji Lubuva, alisema kutokana na taarifa za sensa, tume hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji wapiga kura kutoka vituo 24,919 vya zamani hadi vituo 36,109.
 
Naye Mkurugenzi wa tume hiyo, Julius Malaba, alisema katika majaribio ya mfumo huo wa BVR, changamoto kadhaa zilijitokeza ikiwemo mfumo mzima wa BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na programu zinazotumiwa na mfumo huo pamoja na maeneo ya uendeshaji uandikishaji huo. 
 
 “Changamoto zote hizi tumezifanyia kazi kwa kuzirekebisha. Katika BVR zitakazotumika mkoani Njombe nazo zimefanyiwa marekebisho kutokana na changamoto zilizojitokeza, ila tumechukua tahadhari za uhakika ili kuhakikisha utaratibu mzima unafanyika bila tatizo,” alisema Malaba. 
 
Wakitoa maoni yao kuhusu mada hiyo, wengi wa viongozi wa vyama vya siasa walionesha wasiwasi na kutokuwa na imani na tume hiyo kwa kushindwa kuwasilisha ratiba nzima ya uandikishwaji nchi nzima ikiwa ni pamoja na utaratibu huo kuanza huku vifaa vingi vikiwa bado havijawasili. 
 
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, alisema bado kuna masuala mengi yenye utata ambayo tume hiyo haijayafafanua likiwemo suala la programu zipi zinazotumiwa na mfumo huo, lini vifaa vyote vitawasili na kwanini mpaka sasa hakuna ratiba ya uandikishwaji wapiga kura. 
 
“Tunaomba ratiba kamili ya uandikishwaji, mnasema mmeongeza muda ili tujipange na kutoa mawakala, sasa tutajipangaje wakati hata hatujui ratiba yenyewe, lakini pia bado elimu ya uraia iliyotolewa hasa juu ya BVR kwa wananchi na watendaji watakaoendesha uandikishaji haitoshi, tuna wasiwasi, naomba jambo hili baadaye lisivuruge nchi,” alisisitiza Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba. 
 
Hata hivyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliitaka NEC kutokukaa kimya na kujibu hoja mbalimbali zinazojitokeza ili kuondoa utata na dhana potofu zinazosambazwa na baadhi ya watu kuhusu mfumo huo ambazo endapo hazitojibiwa kiuhakika wananchi huziamini.
 
“Kuweni wawazi, msichoke kuwafafanulia watu na kumbukeni kuwa zoezi hili ni muhimu lisipofanyika vizuri tunaweza kujuta mambo yakiharibika.
 
“Nasema hivi kwa kuwa siku zote mambo yakiharibika au uongo ukisambazwa na kuaminiwa bila majibu, lawama zote huiangukia CCM,” alihadharisha. 
 
Akijibu changamoto zilizotolewa na viongozi wa vyama vya siasa, Lubuva alisema watazifanyia kazi, huku akiongeza kuwa suala la ratiba itatolewa hivi karibuni, lakini akadokeza kuwa, baada ya uandikishaji kuanza Njombe, itafuatia mikoa mingine huku Zanzibar na Dar es Salaam zitakuwa za mwisho.

ASKARI APIGWA CHUPA NA DEREVA WA BODABODA


Askari wa Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo la Mzinga, Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ya Temeke.

Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa kwenye doria kwa kutumia pikipiki maarufu kama Tigo na walipofika eneo la Mzinga walimkamata dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa kwenye pikipiki yake.
 
“Polisi walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika kwamba alikuwa na makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva wenzake walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa askari kwa kumpiga chupa usoni,” alisema Kihenya.
 
Aliongeza kuwa “Tumekamata bodaboda kumi na tano na tayari tunaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini wahusika wakuu na tuweze kuwafikisha mahakamani kwa kosa la shambulio,” alieleza.
 
Mashuhuda wa tukio hilo walisema fujo hizo zilikuwa kubwa kiasi kwamba polisi walilazimika kuwatawanya washambuliaji kwa kupiga risasi za moto hewani.
 
“Mimi nilifunga duka nikakimbia maana kulikuwa hakukaliki hapa, walipompiga yule askari, uso wote ulitapakaa damu ndipo wakarusha risasi hewani. Kila mtu alikimbilia anakojua mwenyewe,” alisema moja wa mashuhuda aliyeogopa kutajwa jina lake.
 
Kwa upande wake, Sanja Justin, alisema yeye alikuwa ana safari ya kwenda Mbagala na alipokaribia kituoni cha basi, alisikia mlio wa risasi na kuamua kukimbia na kurudi nyumbani. 
 
“Nilitaka kwenda kupanda gari nielekee Mbagala lakini nilipofika karibu na kituo nikasikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kila mtu alikuwa kwenye harakati za kukimbia ili kujiokoa na matatizo,” alisema.
 
Eneo la Mziga limekuwa na matukio mengi ya kihalifu ambapo mwishoni mwa mwaka jana kuliibuka kikundi cha kihalifu kilichojiita Black Amerika na kusababisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo. 
 
Hata hivyo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kulidhibiti kundi hilo na kurejesha hali ya utulivu kwa wakazi wa eneo hilo.

Wednesday, February 11, 2015

Wakulima wa Miwa Mvomero Waandamana Kudai Malipo


Jeshi la polisi wilayani Mvomero mkoani Morogoro limezuia maandamano ya wakulima wa miwa Turiani waliotaka kuandamana kwa lengo la kulalamikia kiwanda cha Mtibwa kushindwa kulipa madeni yao kwa muda mrefu.

Wakizungumza kwa jazba wakulima hao wakiwemo wazee wamesema hawaoni sababu ya jeshi la polisi wakiwa na silaha kuwazuia kufanya maandamano ya kudai haki yao kwani ni muda mrefu wanalalamikia kiwanda bila majibu.
 
Ingawa wamepewa muda kuwa kufikia tarehe 20 mwezi huu watakuwa wamelipwa, wamesema endapo hawatatimiziwa ahadi hiyo wananchi watalazimika kuhamishia makazi yao kiwandani hadi kieleweke.

Diwani wa kata ya Mtibwa Lukas Mwakambaya na ambaye alihojiwa na jeshi la polisi kwa saa kadhaa katika kituo cha polisi Mtibwa akizungumza na wananchi amesema jeshi la polsi limezuia maandamnao hayo kutokana na kukosa kibali.
 
Amesema hakuona sababu ya jeshi la polisi kutumia silaha na kuweka utepe kuzua wakulima  wasiingie kiwandani kudai haki yao kwani walifanya biashara na kiwanda na wana haki ya kulipwa jasho lao.

Naye meneja wa kiwanda cha Mtibwa Sugar Ahmed Yahaya amekiri  madai ya wakulima hao ni ya msingi na ameshindwa kulipa kwa wakati kutokana na kuharibika kwa soko la sukari la ndani baada ya kupata hasara kufuatia  uingizaji holela wa sukari bila ushuru ambapo ameahidi tarehe 20 mwezi huu atafanya malipo yote ya wakulima.

TAKUKURU YAAPA KUTOKUMUACHA MTU KATIKA SAKATA LA ESCROW


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kuwa haikurupuki katika kuwashughulikia na kuwafikisha mahakamani viongozi wanaotuhumiwa kujipatia fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kwamba ushahidi pekee ndiyo itakaofanya kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.

Akizungumza mara baada ya kuzindua jengo la ofisi ya mkoa la Taasisi hiyo mjini Kigoma juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema hakuna atakayeachwa katika sakata hilo iwapo ushahidi utathibitisha pasi na shaka kwamba alihusika.
 
Alisema uchunguzi dhidi ya viongozi na watu mbalimbali waliohusina na uchotaji wa fedha hizo unaendelea na kwamba ushahidi utakapokamilika kila mmoja atapata kile anachostahili bila kumuonea mtu.
 
“Hatutaki kukurupuka katika kushughulikia watuhumiwa wa sakata la Escrow na muhimu ni ushahidi ambao utawatia hatiani watuhumiwa, ni aibu kwangu kumfikisha mtuhumiwa mahakamani na mwisho wake siku ushahidi hautoshi na mtuhumiwa kuachiwa huru,” alisema Dk Hoseah.
 
Aliwataka wananchi kuwa na imani na chombo hicho katika kushughulikia suala hilo na kwamba haki itatendeka kwa kuwashughulikia watuhumiwa wote kwa haki badala ya kufuata kelele zinazopigwa kwamba hawafanyi kitu au kuwashughulikia watuhumiwa wakubwa.
 
Tangu kuibuka kwa sakata la kuchotwa kwa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) baada ya kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara baina ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali.
 
Hizo ni pamoja na kuvunjwa kwa Bodi ya Wakurugenzi Tanesco, kutenguliwa kwa Uwaziri wa Dk Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, lakini pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alijiuzulu mwishoni mwa mwaka jana, kama ilivyokuwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyejiuzulu mwezi uliopita.
 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Eliakim Maswi amesimamishwa ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake juu ya ushiriki wake katika sakata hilo lililoteka mkutano wa 16 na 17 wa Bunge ambao uliibuka na maazimio manane, yakiwemo ya kuwawajibisha waliotajwa kuhusika kwa namba moja ama nyingine uchotwaji wa karibu sh bilioni 300 katika akaunti ya Escrow.