NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Saturday, January 24, 2015

Ugonjwa sugu wa figo (Chronic Kidney Disease)

Ugonjwa sugu wa figo (Chronic Kidney Disease)Ugonjwa huu hutokea pale figo zinapopoteza uwezo wa kutenda kazi ambayo hutokea taratibu, na huchukua muda wa takribani miezi kadhaa hata miaka. Figo zinapopoteza uwezo wake wa kutenda kazi, kusanyiko na limbikizo la maji, uchafu na sumu hutokea mwilini mwa mgonjwa na pia husababisha kutokea kwa maradhi mengine kama tulivyoyataja katika vipindi vilivyopita. Lakini huenda ukajiuliza swali kwamba je, kuna tofauti gani kati ya ugonjwa sugu wa figo na kushindwa figo kufanya kazi kwa ghafla yaani Acute Renal Failure? Tofauti ni kwamba ARF hutokea ghafla, huchukua muda mfupi kati ya siku hadi wiki kadhaa kuwa tatizo kubwa zaidi. Tofauti nyingine ni kuwa kushindwa kufanya kazi figo kwa ghafla hutokana na tatizo linaloathiri figo moja kwa moja, mishipa yake ya damu au mtiririko wa mkojo unaotoka kwenye figo. Aidha ARF mara nyingi huweza kurekebishwa na mgonjwa akapona kabisa, ingawa kwa baadhi ya wagonjwa sehemu fulani ya figo inaweza isipate nafuu na ikaendelea kudorora kiutendaji.
Hatua za Ugonjwa Sugu wa Figo: Ugonjwa sugu wa figo umegawanywa katika hatua kuu tano, kulingana na ukubwa wa tatizo. Hatua hizo zimegawanywa kulingana na kiwango cha GFR kilichofikiwa na figo husika. Glomerular Filtration Rate kwa kifupi GFR ni kiwango kinachoonesha uwezo wa utendaji kazi wa figo. GFR hupima uwezo wa glomeruli au chujio la figo katika kuchuja uchafu, maji pamoja na sumu nyingine kwa kila dakika moja kwa mtu mwenye wastani wa urefu wa mita mraba 1.73. Kadiri GFR inavyopungua ndivyo inavyoashiria ukubwa wa tatizo katika figo. Hatua ya kwanza mgonjwa huwa na GFR ya zaidi ya mililita 90 kwa dakika kwa mita mraba 1.73, ambapo madhara madogo huwepo katika figo, huku kiungo hicho kikiendelea kuchuja uchafu kama kawaida. Hatua ya pili ni pale GFR inapokuwa ya kati ya mililita 60-89 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na katika hatua hii, kiwango cha utendaji kazi cha figo hushuka kwa kiasi kidogo. Hatua ya tatu, GFR huwa kati ya mililita 30-59 kwa dakika kwa mita mraba 1.73. Katika hatua hii utendaji kazi wa figo hupungua zaidi, wakati katika hatua ya nne GFR hushuka zaidi na kuwa kati ya mililita 15-29 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na hapa utendaji kazi wa figo huwa wa chini mno. Katika hatua ya tano mgonjwa huwa na GFR chini ya mililita 15 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 hatua ambayo huitwa pia kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo au CRF neno ambalo tutalitumia zaidi kumaanisha kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo yaani chronic renal failure.
Wapenzi wasikilizaji, kuhusiana na wanaopatwa zaidi na tatizo hili tunaweza kusema kuwa, ugonjwa sugu wa figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha udhibiti wa magonjwa cha nchini Marekani (CDC), ugonjwa sugu wa figo ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayojitokeza kuchukua chati za juu sana nchini humo. Ripoti hiyo inaonesha kuwa karibu asilimia 17 ya watu wazima wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo. Aidha ripoti hiyo inaonesha kuwa karibu watu nusu milioni wapo katika matibabu ya dialysis au wameshawahi kubadilishiwa figo. Mambo kadhaa yanahusishwa na ongezeko la ugonjwa sugu wa figo, miongoni mwayo ni ugonjwa kisukari, shinikizo la damu, unene na uzee. Aidha mabadiliko katika tabia na namna watu wanavyoishi pia vimeonekana kuchangia ongezeko hili kwa kiasi kikubwa. Lakini je, tatizo hili kubwa la figo husababishwa na nini?
Visababishi vya ugonjwa sugu wa figo
Pamoja na kwamba ugonjwa sugu wa figo hutokana na magonjwa kadhaa ambayo kimsingi yanaathiri figo yenyewe, visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa figo ni kisukari na shinikizo la damu. Kisukari cha aina ya 1 na ya 2 husababisha hali iitwayo kisukari cha figo au kwa kimombo diabetic nephropathy. Shinikizo la damu kama lisipodhibitiwa vyema, baada ya muda fulani husababisha madhara katika figo. Visababishi vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na magonjwa kama vile systemic lupus erythematosus pamoja na maambukizi ya bakteria jamii ya streptococci ambao husababisha madhara katika chujio la glomeruli ambayo huathiri mfumo wa uchujaji uchafu katika figo. Pia magonjwa ya kurithi ya figo kama vile Polycystic kidney disease. PKD huambatana na hali ya kuwa na vimbe ndogo ndogo zilizojaa maji (cysts) katika figo. Vimbe hizi hufanya figo ishindwe kufanya kazi zake sawasawa na hivyo kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Vilevile matumizi ya kila siku ya muda mrefu ya baadhi ya madawa ya kutuliza maumivu kama vile ibuprofen au acetaminophen yanaweza pia kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Hali hii huitwa kitaalamu analgesic nephropathy. Matumizi ya baadhi ya madawa kama antibiotics za aminoglycosides kama vile gentamicin pia husababisha madhara katika figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo. Kadhalika hali ya mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye figo kuzeeka, kuwa migumu kiasi cha kushindwa kutanuka na kusinyaa. Atherosclerosis husababisha upungufu mkubwa wa damu katika figo husika, kwa kitaalamu hali ambayo inaweza pia kusababisha madhara zaidi kwa figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo na hata CRF. Magonjwa kama vijiwe katika figo, kuvimba tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo pamoja na saratani, vyote vinaweza pia kusababisha madhara katika figo na hatimaye kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Vyanzo vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ambayo husababisha hali inayoitwa HIV nephropathy, ugonjwa wa sickle cell unaoweza kusababisha kuziba kwa mirija inayosambaza damu kwenye figo au upungufu wa damu kwenye figo. Pia matumizi ya madawa ya kulevya, maambukizi sugu katika figo na saratani za figo.
Vihatarishi vya Ugonjwa Sugu wa Figo
Mtu aliye na mojawapo ya vitu au magonjwa haya ana hatari kubwa ya kupata ugonjwa sugu wa figo na hatimaye CRF. Wenye matatizo haya, hawana budi kuhakikisha kuwa figo zao zinafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kuangalia utendaji kazi wake. Magonjwa hayo ni kisukari aina zote mbili, shinikizo la damu, kiwango cha juu cha kolestroli au lehemu katika damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya ini, magonjwa yanayohusiana na aina mbaya ya protini (Amyloidosis), ugonjwa wa seli mundu (Sickle cell disease), ugonjwa wa mzio au mcharuko mwili wa lupus (Systemic Lupus erythematosus), magonjwa ya mishipa ya damu kama vile magonjwa ya mzio katika artery (arteritis) au vasculitis, matatizo katika njia ya mkojo ambapo mkojo badala ya kutoka nje (kushuka chini) hupanda kurudi ndani ya figo (Vesicoureteral reflux), matumizi ya mara kwa mara ya madawa ya kutuliza mcharuko mwili au mzio na kuwa na historia ya magonjwa ya figo katika familia
figo zina uwezo wa ajabu wa kukabiliana na hali ngumu na matatizo katika utendaji kazi wake kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo basi, mgonjwa sugu wa figo anaweza kudumu katika hali yake kwa muda mrefu bila kuonesha dalili zozote zile. Dalili za ugonjwa sugu wa figo hujitokeza pale utendaji kazi wa figo unapokuwa umeshuka na kufikia kiwango cha chini kabisa. Dalili hizo ambazo baadhi tulizitaka katika vipindi vyetu vilivyopita ni pamoja na kukojoa sana hasa wakati wa usiku, kuvimba uso na macho, kuvimba miguu, ongezeko la shinikizo la damu, uchovu na udhaifu wa mwili kutokana na upungufu wa damu au kurundikana kwa uchafu na sumu mwilini, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika na mwili kuwasha, kupata michubuko kirahisi katika ngozi, na ngozi kuwa nyeupe kwa sababu ya upungufu wa damu. Dalili nyingine ni kupumua kwa tabu kutokana na mrundikano wa maji katika mapafu, kichwa kuuma, kujihisi ganzi miguuni au mikononi, kupata shida ya kupata usingizi au kulala usingizi wa mang'amung'amu, mabadiliko katika uwezo wa utambuzi kwa sababu ya madhara katika ubongo yanayosababishwa na mrundikano wa uchafu na sumu za urea, maumivu ya kifua kwa sababu ya mzio katika gamba la juu la moyo, kutokwa damu kwa sababu ya ukosefu wa chembe zinazosaidia damu kuganda, maumivu ya mifupa na kuvunjika kirahisi, na pia kukosa hamu ya tendo la ngono kwa wanaume.

MATIBABU YA UGONJWA WA FIGO
Mojawapo ya njia za matibabu ya figo ni kukisaidia kiungo hicho kufanya kazi kama kawaida kwa kutumia mashine za kitiba kunakojulikana kama dialysis. Dialysis ni usafishaji wa figo unaohusiana na utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu, pia sumu zinazotokana na vyakula au dawa. Tiba ya 'dialysis' ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji kuipata, hutakiwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha huku akitakiwa kuipata tiba hiyo mara nyingine hata mara tatu kwa wiki. Kwa mfano nchini Tanzania mwenye matatizo ya figo huhitaji shilingi laki 3 kila wiki kwa ajili ya tiba hiyo ambayo hufanyika mara tatu hadi nne kwa mwezi. Mgonjwa akifikia hali inayohitajia matibabu haya, huhitaji huduma hii ya kusafishwa damu kwa mashine kwa umri wake wote, kama hatopandikizwa figo nyingine. Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitajika kutoka kwenye damu, mchakato unaofanywa kwa mashine maalumu zinazounganishwa kwa mgonjwa baada ya figo kushindwa kufanya kazi. Hii ni kwa sababu ni lazima damu isafishwe na kuondolewa taka hizo zilizoingia kwenye mfumo wa damu kwani zikibakia huhatarisha maisha. Kwa kawaida figo hufanya kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya wakati figo hushindwa kufanya kazi yake hiyo muhimu kutokana na sababu mbalimbali tulizozizungumzia huko nyuma. Usafishaji wa figo hufanyiwa wagonjwa ambao figo zao zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na maradhi ambapo tiba hiyo huwa ni ya dharura
Wakati wa kufanyiwa tiba ya dialysis mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu, huku kwenye mashine kukiwa na figo ya bandia ambayo kazi yake ni kupitisha damu, kuisafisha na kuirudisha mwilini. Kwenye mashine maalumu kunakuwepo na mipira kadhaa ikiwemo ya kupitishia damu kupeleka kwenye figo bandia inayofanya kazi kama ya mwilini, na mirija mingine ambayo ni mikubwa kiasi inayotumika kutoa maji yasiyohitajika mwilini na sumu, huku mingine ikitumika kurudisha damu safi mwilini. Mgonjwa hulala kitandani wakati wa kufanyiwa tiba hii kwa masaa manne, bila kuchomwa sindano ya usingizi, kwa kuwa dialysis haina maumivu makali. Vilevile mgonjwa hutobolewa eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira, kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa. Hata hivyo, tiba hii licha ya kuwa na gharama kubwa ambazo wagonjwa wengi huwa hawazimudu hasa katika nchi masikini, haina uhakika wa kupunguza tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee. Suala hili linasisitiza umuhimu wa kuzitunza vyema figo zetu na kujiepusha na mambo yanayosababisha figo kuharibika. Sio vibaya ukijua mpenzi msikiliza kuwa, mwili wa binadamu una uwezo wa kumudu kazi zake kwa kutumia figo moja tu, licha ya mwanadamu kuumbwa na figo mbili. Hii ndio sababu mtu huanza kuhisi matatizo ya figo pale inapokua figo zote mbili zimeshindwa kufanya kazi na kuharibika. Na pia ndio sababu watu wanaweza kusaidia wagonjwa figo moja na kubakia wakiishi kwa kutumia figo moja iliyobakia bila matatizo yoyote.
Tiba nyingine ya ugonjwa huu ni ya kupandikiza figo inayojulikana kitaalamu kama kidney transplant. Tiba hii hufanywa hasa kwa mgonjwa ambaye figo yake imekufa na haiwezi kufanya kazi kwa msaada wa dialysis ambapo hupandikizwa au kuitikwa figo ya mtu mwingine mwilini mwake. Tiba hii ya figo ina gharama kubwa sana na ni ngumu kufanyika hasa kwa kuzingatia kuwa figo inayotakiwa kupandikizwa mgonjwa hutoka kwa mtu mwingine. Pia ni vigumu kupatikana mtu atakayejitolea figo yake na abakiwe na figo moja, na hata akipatikana baadhi ya wakati huwa hailingani au haiendani na figo ya mgonjwa suala ambalo hupekekea kufanyika tiba hiyo kuwa kugumu na mafanikio yake kuwa madogo. Pia tiba hiyo huwa na madhara kiafya hasa kwa walio kwenye hatua ya tano ya tiba hiyo. Madhara hayo ni pamoja na maradhi ya moyo, miguu kukaza na maumivu ya kifua
Pia mtu mwenye matatizo ya figo anapaswa kupunguza kiasi cha sodium au chumvi anayokula. Kiasi cha maji mwilini hudhibitiwa na sodium na pale madini hiyo inapozidi mwilini husababisha maji kubakia mwilini. Hali hii huweza kusababisha ongezeko la uzito ghafla, kuvimba kwa viungo vya mwili, shinikizo kubwa la damu, kushindwa kupumua na hatimaye kusababisha ugonjwa wa moyo. Vyakula vyenye sodium kwa wingi ni vyakula vilivyosindikiwa kwa chumvi kama nyama, samaki na soseji za makopo. Mgonjwa anapaswa kujenga tabia ya kutoongeza chumvi kwenye chakula wakati wa kula. Vilevile anapaswa kupunguza kiasi cha potassium katika mlo wake. Madini ya potassium yanapozidi mwilini husababisha misuli kuwa dhaifu na mapigo ya moyo kubadilika na yakizidi sana huweza kusababisha kifo cha ghafla. Ni muhimu kudhibiti kiasi cha potassium kwa ukaribu. Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maparachichi, ndizi mbivu, maboga, machungwa, peach, peasi, matunda yaliyokaushwa na maharagwe. Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kidogo ni pamoja na zabibu, machenza, mahindi mabichi, cauliflower, na matango. Unaweza kupunguza kiasi cha potassium kwenye chakula kwa kuchemsha na kumwaga maji ya ziada.
Pia mgonjwa wa figo anapaswa kupunguza kiasi cha phosphorus. Uwiano wa calcium na phosphorus mwilini ni muhimu kuwezesha afya njema ya mifupa, misuli na neva. Phosphorus inapozidi mwilini mifupa huwa myepesi na rahisi kuvunjika suala linatokana na mwili kushindwa kuhifadhi na kuitoa calcium kwenye mifupa. Vyakula ambavyo vina phosphorus kwa wingi ni pamoja na maziwa na vyakula vya jamii ya maziwa, nyama, shellfish, vyakula ambavyo havijakobolewa, maharage, karanga, korosho na chokoleti. Wagonjwa wa figo pia huhitaji vitamini na madini ya nyongeza kutokana na kutokula aina mbalimbali za vyakula na hivyo kuweza kusababisha upungufu wa baadhi ya virutubishi. Damu inapochujwa kwa njia ya dialysis pia huondoa vitamini kwenye damu kwa hivyo vitamin hizo ambazo ni dharura kwa mwili hupaswa kufidiwa kwa kula virutubishi vya nyongeza au supplements. Virutubishi vya nyongeza vinapaswa kutolewa kwa mgonjwa wa figo baada ya ushauri wa daktari