Kuna usemi flani unatumiwa na watu wengi sana. unasema; “kazi ndio msingi wa maendeleo ya mtu yeyote” . Hata mimi nakubaliana na usemi huu kwani ni kweli kabisa kazi ndio msingi wa hatua yoyote ya maendeleo ya mtu yeyote chini ya msingi mkuu ambao ni Mungu. Kinyume chake, asiyefanya kazi (ya kuajiriwa/kujiajiri) basi atabaki kuwa maskini na mtu wa shida ya kipato, mahusiano mabaya na wanadamu wenzako, kuwa tegemezi nk. Kwa kuwa tunatamani sana kutoka katika kongwa hili la umasikini wa kipato na hali mbaya ya maisha, tunalazimika kufanya jukumu letu kuu la kumuomba sana Mungu ili atuwezeshe kujua na kufahamu mbinu mbalimbali kisha kujifunza na kufahamu kwa makini tena kwa njia rahisi mno za kututoa katika hali hii ya umaskini uliokithiri.

Ikumbukwe kwamba, kujifunza kwa msisimko tu bila ya kuyaingiza mambo hayo uliyojifunza katika mazoezi na vitendo vya makusudi maishani mwetu ni wazi kwamba hayatatusaidia, bali yatabaki vichwani mwetu kama hadithi tu za alfulelaulela na maisha ya kubahatisha maarufu kama akadabraakadabra. Hivyo tumuombe sana Mungu wetu ili mafundisho haya yaweze kubadili maisha yetu kwa uchumi bora na endelevu ili tuweze kupata kipato na kurudishia Mungu zaka na sadaka badala ya kukaa kulalamika kuwa hatuna cha mkurudishia muumba wetu YEHOVA.

Kama ilivyo chunvi ya dunia, ufugaji pia huhitaji upendo, uvumilivu, karama, utu na maombi ya dhati ambayo yatazaa namna nzuri ya kuipenda kwa dhati ya moyo wako kazi hii ya ufugaji. Vinginevyo utabakia kuwa mtu wa kujaribu na kuishia kushindwa kila mara. Kama ilivyo kanuni ya maendeleo yoyote yale, ufugaji wa kuku pia huhitaji; Ubunifu, utundu wa akili, kujaribu bila kukata tamaa, kugundua, kujifunza, kufanyia kazi mawazo yaa wengine, kusoma vitabu na majarida mbalimbali yahusuyo kazi yako, kujishughulisha nk.Hata ukifundishwa darasani huwezi kufundishwa vyote na mwalimu wako, vingine itakubidi utafute mahali pengine kwa ubunifu mkubwa, ugunduzi na mambo mengine mengi ili ufanikishe lengo la kupata elimu bora ya kile unachokitaka. Hii huhusisha akili yako vema katika kujifunza kutoka kwa watu au vitu vingine nk. Lakini mafanikio zaidi yatapatikana pale utakapokuwa katika utendaji zaidi.


UFUGAJI WA KUKU WATANO (5) WA KIENYEJI UPATE KUKU MIA MBILI (200) KWA MIEZI SITA (6) TU!
(Kuku 200 x 5,000 = 1,000,000)
Unaweza ukaniona kama mimi ni kichaa na ninaye ota ndoto za mchana ambazo hazina mafanikio wala tija maana nadharia hii inaweza isiwaingie vizuri watu vichwani mwao. Watu wengi wamekuwa wakisema na kushauri hata kushauriwa hata na wale wasiofaa. Ninaamini wengi wetu hawapendi kuamini kile wanachoambiwa hadi pale watakapoona kwa macho yao ndipo waamini (akina Tomaso). Sikia nikuambie! kama huamini haraka kitu chochote hebu usimkatishe tamaa yule aliyekwambia habari hizo za kukatisha tamaa, badala yake jaribu kupeleleza na kufuatatilia hatua kwa hatua tena kwa makini maelezo uliyopewa, kisha yaweke katika utendaji (tenda/fanya) kwa ufanisi kisha subiri matokeo. Baada ya kupata matokeo sasa unaweza kwenda mbele kidogo ukauliza/kusoma/kujifunza zaidi ili kuona kama kuna mahali umekosea au hukuzingatia kanuni na maelekezo uliyopewa. Baada ya kupata maelezo ya ziada hebu rudia kufanya tena kwakuboresha kupitia maelekezo ya awali na hayo mapya uliyopata yote kwa pamoja ili upime matokeo yake. Hapo sasa utakuwa upo kwenye haki ya kuamini au kutoamini kwamba jambo hilo ni kweli au siyo kweli na siyo kutaa tu kwa ubishi usiokuwa na maana yeyote. Kwa kufanya hivi hakika utapiga hatua mbele katika kuboresha maisha yako ya sasa na ya baadae. Ila ukifanikiwa usije ukamkufuru Mungu aliyekuwezesha.

Hebu anza na kuku Watano (5) tu Majike wenye Rika/Umri mmoja (au wanaokaribiana). Watunze vizuri kwa kuwapatia chakula kilicho na mchanganyiko kamili wa viini lishe vinavyotakiwa katika mwili wa kuku, yaani; wanga, protini, calcium, chumvichumvi, madini joto nk(kama nilivyoeleza hapa chini). Wawekee na Jogoo mmoja mzuri wa kienyeji/kizungu/chotara (kama nilivyoeleza hapa chini juu ya uchaguzi wa majogoo).

Wanapoanza kutaga watayarishie mahali pazuri/Kiota kizuri cha kutagia na kuatamia kwa kuwajengea viota ndani ya banda. Hakikisha mahali hapo hapavuji wala hapapati unyevunyevu wala joto kali sana. Hakikisha mahali hapo pana usalama wa kutosha (mahali wanyama hatari kama vicheche, pakashume, nyoka nk hawawezi kufika).

Kuku wakiendelea kutaga na sasa ukaona wanakaribia kuatamia,Anza kuchagua aina ya mayai unayotaka kuku wako walalie. Hii inamaanisha kuwa; ukichagua mayai makubwamakubwa hayo yanakuwa na vifaranga majogoo na mayai madogomadogo mara nyingi huwa ni ya vifaranga majike. Acha kuwawekea mayai ya mviringo kama mpira!

Hakikisha kuku wote wanasubiriana ili walalie/waatamie kwa pamoja.

Weka mayai 12 hadi 15 kwa kila kiota cha kuku 1 kulingana na umbo la kuku wako. Kuku anaweza kutaga hadi mayai 30 kwa kila msimu wa kutaga unapofika. Unaweza kutumia mayai machache kati ya 30 kwa kumuatamishia kuku wako huku mayai mengine yakisubiri awamu ya pili ya kuatamiwa.Kwa mfano ukiwawekea kuku wako hao watano, Kuku 5 x Mayai 12 = Mayai 60.

Kwa kawaida kuku huatamia/hulalia mayai kwa siku 19 hadi 21/24 tu hadi anapototoa vifaranga. Hakikisha unawawekea kuku walioatamia chakula chenye viini lishe vya kutosha na maji mengi karibu na viota vyao ili wakitoka kwenye viota vyao wale chakula mara moja na kunywa maji kisha warudi haraka kwenye mayai yao. Hii itasaidia kuangua mayai yote 12/15 bila kuharibu yai hata moja. Au hata yakiharikbika basi hayataharibika mengi kama ukiacha kuwawekea chakula waende kufukuzana na panzi na vyakula majalalani huko nje na kuchelewa kurudi kwenye mayai yao.

Wakati ukisubiria siku hizo 21/24 anza kujenga kibanda kidogo ndani ya banda kubwa ulilojenga awali au jikoni au andaa boksi kubwa na gumu kwaajili ya kutunzia vifaranga watakaoanguliwa ndani ya siku 21/24 zijazo.

Baada ya kuku hao 5
 kuangua vifaranga wako 60 hapo ndipo kazi kubwa ya kulea vifaranga inapoanza. Elewa kuwa ili upate mafanikio haraka hakikisha kuwa kazi ya kulea vifaranga inakuwa yako na siyo ya kuku! Kwanza, Unatakiwa kuondoa na kuchoma moto/kufukia mabaki yote ya mayai na kuboresha usafi wa banda lote ili kuepusha magonjwa kama vile kuharisha, viroboto, papasi nk. Hapo unaweza kuwatoa vifaranga wako wote 60 mmojammoja kadri wanavyoanguliwa hadi kufikia kifaranga wa mwisho, yaani Yule wa 60 na kuwaweka katika kibanda kidogo/boksi ulichokijenga na kuwawekea mayai mengine mama zao (yale 15/18 kati ya 30 uliyoyabakiza) ili waatamie tena kwa siku 21 hadi 24 zingine. Unapotoa kifaranga kutoka kwa kuku aliyeatamia humfanya kuku Yule ashindwe kutoka kwenye mayai maana hana mtoto wa kulea.

Akimaliza kuangua mayai yote na ukamuwekea mengine ni rahisi kwake kuendelea kuatamia maana atasubiri kupata vifaranga na ndipo atajikuta amelalia kwa siku 21 zingine bila wasiwasi. Kwa kufanya hivyo utakuwa tayari umejipatia vifaranga/kuku zaidi ya 100 ndani yawiki 7 tu! Sasa Unatakiwa kuwajali sana kuku hawa wanaolalia kwa mara ya pili kwa kuwapa chakula cha kutosha, maji, majani ya makongwe, mchicha, mchunga nk ili wapate vitamini na madini mengine muhimu kwa afya zao. Fanya hivyo hata watakapokuwa wametotoa na ukawanyang’anya vifaranga. Hii itawasaidia ili wasinyonyoke sana manyoya maana kuku wengi hunyonyoka manyoya wanapoatamia. Kwa kufanya hivi, kuku wako watakaa kwa wiki 2 hadi 3 bila vifaranga na kisha wataanza kutaga tena na kuatamia kama mwanzo.

Vifaranga
 wako hakikisha unawatengenezea chumba chao kido ndani ya banda kubwa/jikoni, kisha wawekee chanzo chochote cha joto kama vile; taa ya chemli/jiko la mkaa/vizinga vya moto nk ili wasiathiriwe na baridi hasa wakati wa usiku. Umakini mkubwa sana unatakiwa hapa! Hakikisha unakuwa makini wakati wa usiku ili kuongeza na kupunguza joto ndani ya kibanda cha vifaranga maana wakati huu maranyingi joto hupungua na ubaridi huongezeka na hivyo unaweza kuua vifaranga wako.

NAMNA YA KULEA VIFARANGA.
Katika ulezi wa vifaranga kama kuku utawanyang’anya vifaranga vyao utatakiwa kuwajengea banda dogo (ndani ya banda kubwa/uzio) ili uwawekee chanzo cha joto kama taa/jiko la mkaa (kama ni sehemu/majira ya baridi). Kama utatumia jiko la mkaa unatakiwa kuacha kwanza hadi mkaa mweusi uwake wote ndipo uweke bandani maana mkaa ukitoa moshi unaweza kuathiri vifaranga vyako. Angalia namna ya kuweka jiko lako la mkaa juu kidogo ili vifaranga wasiungue. Hakikisha taa yako haitoi moshi sana na haivujishi mafuta. Pia uwe na akiba ya mafuta ya taa ya kutosha. Usiweke mafuta mengi kwenye taa maana inaweza kulipuka ikakuletea hasara. Vifaranga wasizidi 50 kwa boksi 1. Hakikisha umewasha taa/jiko lako ndani ya boksi saa tatu au zaidi kabla ya kuwaweka vifaranga ili chumba/boksi lipate joto kabla ya vifaranga kuwasili. Njia hizi zinahitaji uangalifu wa hali ya juu sana kwani kuhatarisha/kuua vifaranga ni kuhatarisha maendeleo yako. Kama utaamua kutumia umeme pia ni vizuri zaidi maana inapunguza hatari zaidi.
=Mambo muhimu ndani ya Banda.
  1. Sakafu nzuri (iliyotengenezwa kwa saruji/udongo ili isituamishe maji. Isiwe na nyufa ili iweze kusafishwa kwa urahisi.
  2. Hakikisha kuwa banda linakuwa na Viota (vitagio) vizuri kwaajili ya kutagia. Viota viwe na urefu wa Sentimita 30 na upana sentimita 30 na kina sentimita 35. Sehemu ya mbele izibwe kwa sentimita 10 tu chini. Sehemu zote hizo zizibwe kwa ubao. Kama kuku wako ni wakubwa unaweza kuongeza upana, urefu na kina kiasi cha kutosha mfano, Upana na Urefu 35cm, kina 55cm nk. Hakikisha kiota/kitagio kinakuwa na giza kiasi maana kuku hupenda kutaga mahala pa giza kidogo/palipojificha. Giza litasaidia kuku asiweze kula mayai au asiweze kudonoana na kuku wengine. Kiota pia kinatakiwa kiwe mahali ambapo ni rahisi kwa kuku kuingia na kutoka, pia iwe ni rahisi kusafisa.

Ndani ya kiota kuwekwe majani makavu/maranda ya mbao laini na kinyunyize dawa ya unga ya kuzuia viroboto/utitiri kabla ya kuweka nyasi.
AIDHA, ni vizuri sana kuwawekea kuku wanaoatamia mayai wakati wa usiku maana ukimuwekea wakati wa mchana anaweza kuyaacha.
Kuku anayetarajiwa kuatamia ni vema akachunguzwa kama anao utitiri/viroboto/chawa kwenye manyoya yake. Wadudu hawa humkosesha raha kuku anayeatamia na wengi huacha mayai na kukimbia/wasitulie kwenye viota vyao. Hali inapelekea kuanguliwa kwa vifaranga wachache. Unaweza kumuona mtaalam wa mifugo kwa ushauri zaidi.
  1. Banda liwe na vichanja maana kuku hupenda kulala juu ya vichanja maana nao ni ndege.
  2. Vyombo safi na vizuri kwaajili ya chakula na maji.
  3. Walazie majani makavu/maranda ya mbao/makapi ya mazao sakafuni kwa banda zima.

UCHAGUZI NA UHIFADHI WA MAYAI.
Mayai huharibika kwa urahisi sana yasipo tayarishwa na kutunzwa vizuri kwa uangalifu. Matayarisho huanzia bandani hadi ndani kwa kufanya yafuatayo;
  • Hakikisha viota vyote ni safi wakati wote.
  • Chakula kiwe ni cha kuimarisha gamba la yai na vyakula vingine.
  • Vyombo vya kukusanyia mayai viewe safi na imara.
  • Kusanya mayai mara2 hadi 3 kwa siku ili kuepuka mayai kuvunjwa/kuliwa/kuchafuka kwa mayai mengi na kupoa haraka.
  • Ondoa mayai yaliyo na nyufa na maganda yasiyo imara.
  • Safisha mayai mara baada ya kukusanya na kabla ya kuweka kwenye chombo cha kuhifadhia saa 12-24. Mayai yanaweza kuoshwa kwa maji ya uvuguvugu (nyuzijoto 35oc) na kusugua taratibu kwa mkono ili kuondoa uchafu (kama upo). Lakini unashauriwa kusugua kwa mkono bila maji ili kusafisha maana maji hupunguza ubora wa yai na maranyingi yai huharibika haraka.
  • Weka katika vyombo visafi kwa kuelekeza sehemu ya yai iliyo pana iwe juu na sehemu nyembamba iwe chini, beba kwa uangalifu.
  • Hifadhi mayai katika sehemu ya baridi nyuzijoto10 hadi 16 za sentigredi.
  • Mayai yapangwe kwa daraja kwa kufuata ukubwa na rangi ili kuvutia wateja na kuongeza bei. Pia unaweza kuweka kwa kufuata muda unapoyaokota kutoka bandani. Weka lebo yenye tarehe ili usichanganye wakati wa kuwaatamishia kuku wako/kuuza.

Kuchagua mayai ya kuatamishia kuku kwaajili ya kuangua vifaranga.
Mayai yanayofaa kwa kuatamiwa na kuanguliwa ni vema yawe na ukubwa wa wastani, yasiwe na ufa/nyufa, yasiwe ya mviringo kama mpira, yasiwe na uchafu wowote juu ya gamba lake, yasiwe yametengwa kwa zaidi ya wiki 1 (siku 7).

MINYOO.
Hawa ni wadudu wanaoleta madhara kwa kuku na wanyama wengine pia. Kuku hupata minyoo kwa kula vyakula vyenye wadudu/vimelea vya wadudu hao.

Dalili. Kuku Hudumaa, manyoya huwa hafifu, hupungua damu na uzito, utagaji wa mayai hupungua, minyoo huweza kuonekana kwenye kinyesi.

Namna ya kuzuia minyoo.
  • Safisha banda mara kwa mara (ukiweza tumia dawa za kuua wadudu)
  • Badilisha matandazo mara kwa mara.
  • Safisha vyombo vya chakula na maji mara 2/3 kwa siku.
  • Tenganisha kuku wakubwa na wadogo.
  • Wape kuku dawa za kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3.
  • Muone mtaalam kwa ushauri zaidi.

MAGONJWA YANAYOWEZA KUSABABISHWA NA UPUNGUFU WA CHAKULA/VIINI LISHE.
Iwapo kuku watapewa chakula chenye viini lishe kidogo/kisicho na viini lishe muhimu kama vile; Protini, Wanga, Madini na Vitaminiwanaweza kupata madhara yafuatayo;
  • Kudumaa,
  • Kupungua uzito,
  • Kupungukiwa na damu,
  • Mifupa kupinda/kuvimba/kutokuwa imara,
  • Utagaji wa mayai hupungua na uangaji wake pia huwa hafifu,
  • Ganda la yai huwa laini,
  • Manyoya huwa machache na laini,
  • Kujikunja kwa shingo/miguu na vidole,
  • Kuwa na majimengi mazito chini ya ngozi ya kifuani,
  • Kupata magonjwa mara kwa mara,
  • Hali hii inaweza kusababisha Kuku kufa.

Namna ya kuzuia.
  1. Kuku wapewe chakula chenye mchanganyiko wa viinilishe vyote muhimu kama vile Vitamini, madini na Chokaa kufuatana na umri/aina na mahitaji yake.
  2. Wapewe majani mabichi kama mchicha, kabichi na majani ya mapapai.
  3. Wapewe mchanganyiko wa vitamin na madini kama chokaa na chumvi kwa kiwango maalum maana ikizidi pia yaweza kuathiri kuku.

MUHIMU.
Ili liziua magonjwa ya kuku na kupata faida kubwa kwa kufuga kuku, ni muhimu sana mtu anayehudumia kuku bandani aweze kutambua haraka dalili za magonjwa ya kuku kama nilivyoeleza hapo juu ikiwa ni pamoja na kuzingatia usafi wa banda. Ni lazima ajue tabia ya kuku ya kila siku. Kuku mgonjwa unaweza kumtambua kwa kuangalia yafuatayo;
  1. Tabia ya kuku.
  2. Kinyesi cha kuku (mabadiliko ya kinyesi).
  3. Ulaji wa chakula na unywaji wa maji kama umepungua.
  4. Utagaji wa mayai na uimara wa mayai kama vimepungua.
  5. Kuku kutochangamka.
  6. Vifo ni dalili ya mwisho.

Kama utaona kuna kuku mgonjwa bandani basi mtenge na wenzie kama unavyowafanyia vifaranga. Ili uweze kuwahudumia peke yao. Wengine ambao hawajaonesha dalili wapewe dawa ya kinga haraka iwezekanavyo kupitia ushauri wa mtaalam wa mifugo aliye karibu.

Chanjo na matibabu yoyote yafuate ushauri wa mtaalam/mtengenezaji wa dawa husika bila kupuuzia ili upate mafanikio. Hii itakuwezesha kupunguza/kuponya magonjwa na kupunguza gharama za matibabu na vifo. Hakikisha kuwa chanjo/tiba zinatoka kwa mtaalam anayejua kutunza chanjo/dawa kwenye ubaridi unaotakiwa kulingana na maagizo ya mtengenezaji.

ANGALIZO
Mambo yafuatayo yanaweza kusababisha magonjwa au kupunguza uzalishaji hivyo kuleta hasara zisizo za lazima kwa mfugaji.;
  1. Kufuga kuku wengi kwenye eneo dogo.
  2. Chumba/banda lisilo na hewa na mwanga wa kutosha.
  3. Banda kuwa chafu.
  4. Vyombo vichache/visivyotesheleza kwaajili ya chakula na maji.
  5. Vyombo vichafu vya maji na chakula.
  6. Chakula kisicho na viini lishe vya kutosha/kichache.
  7. Kubadili ladha ya chakula.
  8. Kuchelewa kudhibiti magonjwa ya kuku.
  9. Kuchanja/kutibu kuku bila utaratibu/ushauri wa kitaalam.
  10. Kutishia kuku wakati wa kuingia bandani/kuwashika/kuwasumbuasumbua.
  11. Mabadiliko ya hali ya hewa.
  12. Kufuga kiholela bila kuwachambua.

MWISHO
  • Chagua njia bora na rahisi inayokufaa kulingana na eneo ulilopo na mahitaji yako pia. Angalia njia itakayokupa faida kwa gharama ndogo.
  • Chagua kuku wenye uwezo wa kukua haraka, wanaostahimili magonjwa, wanaotaga mayai mengi, wanaoweza kuangua vifaranga wengi na kuwalea.
  • Chagua jogoo aliye na uzito mzuri na mwenye kucha fupi.
  • Uwiano wa jogoo kwa majike iwe ni jogoo 1 kwa majike/mitetea 10.
  • Kuku anayetazamiwa kuatamia mayai anatakiwa asiwe na chawa/viroboto/utitiri.
  • Kuku ambaye hakidhi sifa za kuwa kuku bora anayefaa kuwa kwenye kundi inafaa aondolewe ili asilishwe kwa hasara awapo bandani.

Waafrika tulio wengi hatuna utamaduni wa kutunza kumbukumbu. Ni vizuri basi uanze kutunza kumbukumbu za mwenendo wa kazi zako za ufugaji wa kuku. Hii itakurahishia sana kujua faida, hasara na hata kujua namna bora ya kuboresha ufugaji wako. Kwa mfano;
  1. Kumbukumbu za uzalishaji mayai zitakuwezesha kujua kiasi cha mayai yanayotagwa kwa siku. Idadi ikiwa chini ya 60% utagaji huo siyo mzuri hivyo utatafuta sababu ya tatizo nk. Utagaji unatakiwa uwe 70% hadi 95%.
  2. Kumbukumbu ya vifo itakusaidia kujua hatari itakayokujia. Mfano vifo vikizidi 1% inaashiria tatizo la ugonjwa. Hivyo uchunguzi ni lazima ufanyike ili kutatua tatizo.
  3. Kumbukumbu za mapato na matumizi pia zitakusaidia kujua faida na hasara nk. Hapa utajua ni ghara kiasi gani ulitumia kufuga na faida kiasi gani umepata baada ya mauzo ya mayai/kuku husika.