Ugonjwa huu hutokea pale figo zinapopoteza uwezo wa kutenda kazi ambayo
hutokea taratibu, na huchukua muda wa takribani miezi kadhaa hata miaka.
Figo zinapopoteza uwezo wake wa kutenda kazi, kusanyiko na limbikizo la
maji, uchafu na sumu hutokea mwilini mwa mgonjwa na pia husababisha
kutokea kwa maradhi mengine kama tulivyoyataja katika vipindi
vilivyopita. Lakini huenda ukajiuliza swali kwamba je, kuna tofauti gani
kati ya ugonjwa sugu wa figo na kushindwa figo kufanya kazi kwa ghafla
yaani Acute Renal Failure? Tofauti ni kwamba ARF hutokea ghafla,
huchukua muda mfupi kati ya siku hadi wiki kadhaa kuwa tatizo kubwa
zaidi. Tofauti nyingine ni kuwa kushindwa kufanya kazi figo kwa ghafla
hutokana na tatizo linaloathiri figo moja kwa moja, mishipa yake ya damu
au mtiririko wa mkojo unaotoka kwenye figo. Aidha ARF mara nyingi
huweza kurekebishwa na mgonjwa akapona kabisa, ingawa kwa baadhi ya
wagonjwa sehemu fulani ya figo inaweza isipate nafuu na ikaendelea
kudorora kiutendaji.
Hatua za Ugonjwa Sugu wa Figo: Ugonjwa sugu wa
figo umegawanywa katika hatua kuu tano, kulingana na ukubwa wa tatizo.
Hatua hizo zimegawanywa kulingana na kiwango cha GFR kilichofikiwa na
figo husika. Glomerular Filtration Rate kwa kifupi GFR ni kiwango
kinachoonesha uwezo wa utendaji kazi wa figo. GFR hupima uwezo wa
glomeruli au chujio la figo katika kuchuja uchafu, maji pamoja na sumu
nyingine kwa kila dakika moja kwa mtu mwenye wastani wa urefu wa mita
mraba 1.73. Kadiri GFR inavyopungua ndivyo inavyoashiria ukubwa wa
tatizo katika figo. Hatua ya kwanza mgonjwa huwa na GFR ya zaidi ya
mililita 90 kwa dakika kwa mita mraba 1.73, ambapo madhara madogo huwepo
katika figo, huku kiungo hicho kikiendelea kuchuja uchafu kama kawaida.
Hatua ya pili ni pale GFR inapokuwa ya kati ya mililita 60-89 kwa
dakika kwa mita mraba 1.73 na katika hatua hii, kiwango cha utendaji
kazi cha figo hushuka kwa kiasi kidogo. Hatua ya tatu, GFR huwa kati ya
mililita 30-59 kwa dakika kwa mita mraba 1.73. Katika hatua hii utendaji
kazi wa figo hupungua zaidi, wakati katika hatua ya nne GFR hushuka
zaidi na kuwa kati ya mililita 15-29 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na
hapa utendaji kazi wa figo huwa wa chini mno. Katika hatua ya tano
mgonjwa huwa na GFR chini ya mililita 15 kwa dakika kwa mita mraba 1.73
hatua ambayo huitwa pia kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo au CRF neno
ambalo tutalitumia zaidi kumaanisha kushindwa kufanya kazi sugu kwa
figo yaani chronic renal failure.
Wapenzi wasikilizaji, kuhusiana na
wanaopatwa zaidi na tatizo hili tunaweza kusema kuwa, ugonjwa sugu wa
figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na
kuendelea. Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha udhibiti wa magonjwa cha
nchini Marekani (CDC), ugonjwa sugu wa figo ni miongoni mwa matatizo ya
kiafya yanayojitokeza kuchukua chati za juu sana nchini humo. Ripoti
hiyo inaonesha kuwa karibu asilimia 17 ya watu wazima wenye umri wa
miaka 20 na kuendelea wanasumbuliwa na ugonjwa sugu wa figo. Aidha
ripoti hiyo inaonesha kuwa karibu watu nusu milioni wapo katika matibabu
ya dialysis au wameshawahi kubadilishiwa figo. Mambo kadhaa
yanahusishwa na ongezeko la ugonjwa sugu wa figo, miongoni mwayo ni
ugonjwa kisukari, shinikizo la damu, unene na uzee. Aidha mabadiliko
katika tabia na namna watu wanavyoishi pia vimeonekana kuchangia
ongezeko hili kwa kiasi kikubwa. Lakini je, tatizo hili kubwa la figo
husababishwa na nini?
Visababishi vya ugonjwa sugu wa figo
Pamoja na kwamba ugonjwa sugu wa figo hutokana na magonjwa kadhaa ambayo
kimsingi yanaathiri figo yenyewe, visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa
figo ni kisukari na shinikizo la damu. Kisukari cha aina ya 1 na ya 2
husababisha hali iitwayo kisukari cha figo au kwa kimombo diabetic
nephropathy. Shinikizo la damu kama lisipodhibitiwa vyema, baada ya muda
fulani husababisha madhara katika figo. Visababishi vingine vya ugonjwa
sugu wa figo ni pamoja na magonjwa kama vile systemic lupus
erythematosus pamoja na maambukizi ya bakteria jamii ya streptococci
ambao husababisha madhara katika chujio la glomeruli ambayo huathiri
mfumo wa uchujaji uchafu katika figo. Pia magonjwa ya kurithi ya figo
kama vile Polycystic kidney disease. PKD huambatana na hali ya kuwa na
vimbe ndogo ndogo zilizojaa maji (cysts) katika figo. Vimbe hizi hufanya
figo ishindwe kufanya kazi zake sawasawa na hivyo kusababisha ugonjwa
sugu wa figo. Vilevile matumizi ya kila siku ya muda mrefu ya baadhi ya
madawa ya kutuliza maumivu kama vile ibuprofen au acetaminophen yanaweza
pia kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Hali hii huitwa kitaalamu
analgesic nephropathy. Matumizi ya baadhi ya madawa kama antibiotics za
aminoglycosides kama vile gentamicin pia husababisha madhara katika figo
na hatimaye ugonjwa sugu wa figo. Kadhalika hali ya mishipa ya damu
inayosambaza damu kwenye figo kuzeeka, kuwa migumu kiasi cha kushindwa
kutanuka na kusinyaa. Atherosclerosis husababisha upungufu mkubwa wa
damu katika figo husika, kwa kitaalamu hali ambayo inaweza pia
kusababisha madhara zaidi kwa figo na hatimaye ugonjwa sugu wa figo na
hata CRF. Magonjwa kama vijiwe katika figo, kuvimba tezi dume, kuziba
kwa njia ya mkojo pamoja na saratani, vyote vinaweza pia kusababisha
madhara katika figo na hatimaye kusababisha ugonjwa sugu wa figo. Vyanzo
vingine vya ugonjwa sugu wa figo ni pamoja na maambukizi ya virusi vya
Ukimwi ambayo husababisha hali inayoitwa HIV nephropathy, ugonjwa wa
sickle cell unaoweza kusababisha kuziba kwa mirija inayosambaza damu
kwenye figo au upungufu wa damu kwenye figo. Pia matumizi ya madawa ya
kulevya, maambukizi sugu katika figo na saratani za figo.
Vihatarishi vya Ugonjwa Sugu wa Figo
Mtu aliye na mojawapo ya vitu au
magonjwa haya ana hatari kubwa ya kupata ugonjwa sugu wa figo na
hatimaye CRF. Wenye matatizo haya, hawana budi kuhakikisha kuwa figo zao
zinafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kuangalia utendaji kazi
wake. Magonjwa hayo ni kisukari aina zote mbili, shinikizo la damu,
kiwango cha juu cha kolestroli au lehemu katika damu, magonjwa ya moyo,
magonjwa ya ini, magonjwa yanayohusiana na aina mbaya ya protini
(Amyloidosis), ugonjwa wa seli mundu (Sickle cell disease), ugonjwa wa
mzio au mcharuko mwili wa lupus (Systemic Lupus erythematosus), magonjwa
ya mishipa ya damu kama vile magonjwa ya mzio katika artery (arteritis)
au vasculitis, matatizo katika njia ya mkojo ambapo mkojo badala ya
kutoka nje (kushuka chini) hupanda kurudi ndani ya figo (Vesicoureteral
reflux), matumizi ya mara kwa mara ya madawa ya kutuliza mcharuko mwili
au mzio na kuwa na historia ya magonjwa ya figo katika familia
figo zina uwezo wa ajabu wa kukabiliana na hali ngumu na matatizo
katika utendaji kazi wake kwa muda mrefu. Kwa sababu hiyo basi, mgonjwa
sugu wa figo anaweza kudumu katika hali yake kwa muda mrefu bila
kuonesha dalili zozote zile. Dalili za ugonjwa sugu wa figo hujitokeza
pale utendaji kazi wa figo unapokuwa umeshuka na kufikia kiwango cha
chini kabisa. Dalili hizo ambazo baadhi tulizitaka katika vipindi vyetu
vilivyopita ni pamoja na kukojoa sana hasa wakati wa usiku, kuvimba uso
na macho, kuvimba miguu, ongezeko la shinikizo la damu, uchovu na
udhaifu wa mwili kutokana na upungufu wa damu au kurundikana kwa uchafu
na sumu mwilini, kupoteza hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika na
mwili kuwasha, kupata michubuko kirahisi katika ngozi, na ngozi kuwa
nyeupe kwa sababu ya upungufu wa damu. Dalili nyingine ni kupumua kwa
tabu kutokana na mrundikano wa maji katika mapafu, kichwa kuuma,
kujihisi ganzi miguuni au mikononi, kupata shida ya kupata usingizi au
kulala usingizi wa mang'amung'amu, mabadiliko katika uwezo wa utambuzi
kwa sababu ya madhara katika ubongo yanayosababishwa na mrundikano wa
uchafu na sumu za urea, maumivu ya kifua kwa sababu ya mzio katika gamba
la juu la moyo, kutokwa damu kwa sababu ya ukosefu wa chembe
zinazosaidia damu kuganda, maumivu ya mifupa na kuvunjika kirahisi, na
pia kukosa hamu ya tendo la ngono kwa wanaume.
MATIBABU YA UGONJWA WA FIGO
Mojawapo ya njia za matibabu ya figo ni kukisaidia kiungo hicho kufanya
kazi kama kawaida kwa kutumia mashine za kitiba kunakojulikana kama
dialysis. Dialysis ni usafishaji wa figo unaohusiana na utoaji wa maji
yaliyojaa mwilini, uchafu, pia sumu zinazotokana na vyakula au dawa.
Tiba ya 'dialysis' ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji
kuipata, hutakiwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha huku akitakiwa kuipata
tiba hiyo mara nyingine hata mara tatu kwa wiki. Kwa mfano nchini
Tanzania mwenye matatizo ya figo huhitaji shilingi laki 3 kila wiki kwa
ajili ya tiba hiyo ambayo hufanyika mara tatu hadi nne kwa mwezi.
Mgonjwa akifikia hali inayohitajia matibabu haya, huhitaji huduma hii ya
kusafishwa damu kwa mashine kwa umri wake wote, kama hatopandikizwa
figo nyingine. Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitajika kutoka
kwenye damu, mchakato unaofanywa kwa mashine maalumu zinazounganishwa
kwa mgonjwa baada ya figo kushindwa kufanya kazi. Hii ni kwa sababu ni
lazima damu isafishwe na kuondolewa taka hizo zilizoingia kwenye mfumo
wa damu kwani zikibakia huhatarisha maisha. Kwa kawaida figo hufanya
kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya wakati figo
hushindwa kufanya kazi yake hiyo muhimu kutokana na sababu mbalimbali
tulizozizungumzia huko nyuma. Usafishaji wa figo hufanyiwa wagonjwa
ambao figo zao zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na maradhi ambapo tiba
hiyo huwa ni ya dharura
Wakati wa kufanyiwa tiba ya dialysis mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu,
huku kwenye mashine kukiwa na figo ya bandia ambayo kazi yake ni
kupitisha damu, kuisafisha na kuirudisha mwilini. Kwenye mashine maalumu
kunakuwepo na mipira kadhaa ikiwemo ya kupitishia damu kupeleka kwenye
figo bandia inayofanya kazi kama ya mwilini, na mirija mingine ambayo ni
mikubwa kiasi inayotumika kutoa maji yasiyohitajika mwilini na sumu,
huku mingine ikitumika kurudisha damu safi mwilini. Mgonjwa hulala
kitandani wakati wa kufanyiwa tiba hii kwa masaa manne, bila kuchomwa
sindano ya usingizi, kwa kuwa dialysis haina maumivu makali. Vilevile
mgonjwa hutobolewa eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira,
kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa.
Hata hivyo, tiba hii licha ya kuwa na gharama kubwa ambazo wagonjwa
wengi huwa hawazimudu hasa katika nchi masikini, haina uhakika wa
kupunguza tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee.
Suala hili linasisitiza umuhimu wa kuzitunza vyema figo zetu na
kujiepusha na mambo yanayosababisha figo kuharibika. Sio vibaya ukijua
mpenzi msikiliza kuwa, mwili wa binadamu una uwezo wa kumudu kazi zake
kwa kutumia figo moja tu, licha ya mwanadamu kuumbwa na figo mbili. Hii
ndio sababu mtu huanza kuhisi matatizo ya figo pale inapokua figo zote
mbili zimeshindwa kufanya kazi na kuharibika. Na pia ndio sababu watu
wanaweza kusaidia wagonjwa figo moja na kubakia wakiishi kwa kutumia
figo moja iliyobakia bila matatizo yoyote.
Tiba nyingine ya ugonjwa
huu ni ya kupandikiza figo inayojulikana kitaalamu kama kidney
transplant. Tiba hii hufanywa hasa kwa mgonjwa ambaye figo yake imekufa
na haiwezi kufanya kazi kwa msaada wa dialysis ambapo hupandikizwa au
kuitikwa figo ya mtu mwingine mwilini mwake. Tiba hii ya figo ina
gharama kubwa sana na ni ngumu kufanyika hasa kwa kuzingatia kuwa figo
inayotakiwa kupandikizwa mgonjwa hutoka kwa mtu mwingine. Pia ni vigumu
kupatikana mtu atakayejitolea figo yake na abakiwe na figo moja, na hata
akipatikana baadhi ya wakati huwa hailingani au haiendani na figo ya
mgonjwa suala ambalo hupekekea kufanyika tiba hiyo kuwa kugumu na
mafanikio yake kuwa madogo. Pia tiba hiyo huwa na madhara kiafya hasa
kwa walio kwenye hatua ya tano ya tiba hiyo. Madhara hayo ni pamoja na
maradhi ya moyo, miguu kukaza na maumivu ya kifua
Pia mtu mwenye matatizo ya figo anapaswa kupunguza kiasi cha sodium au
chumvi anayokula. Kiasi cha maji mwilini hudhibitiwa na sodium na pale
madini hiyo inapozidi mwilini husababisha maji kubakia mwilini. Hali hii
huweza kusababisha ongezeko la uzito ghafla, kuvimba kwa viungo vya
mwili, shinikizo kubwa la damu, kushindwa kupumua na hatimaye
kusababisha ugonjwa wa moyo. Vyakula vyenye sodium kwa wingi ni vyakula
vilivyosindikiwa kwa chumvi kama nyama, samaki na soseji za makopo.
Mgonjwa anapaswa kujenga tabia ya kutoongeza chumvi kwenye chakula
wakati wa kula. Vilevile anapaswa kupunguza kiasi cha potassium katika
mlo wake. Madini ya potassium yanapozidi mwilini husababisha misuli kuwa
dhaifu na mapigo ya moyo kubadilika na yakizidi sana huweza kusababisha
kifo cha ghafla. Ni muhimu kudhibiti kiasi cha potassium kwa ukaribu.
Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kikubwa ni pamoja na maparachichi,
ndizi mbivu, maboga, machungwa, peach, peasi, matunda yaliyokaushwa na
maharagwe. Vyakula vyenye potassium kwa kiasi kidogo ni pamoja na
zabibu, machenza, mahindi mabichi, cauliflower, na matango. Unaweza
kupunguza kiasi cha potassium kwenye chakula kwa kuchemsha na kumwaga
maji ya ziada.
Pia mgonjwa wa figo anapaswa kupunguza kiasi cha
phosphorus. Uwiano wa calcium na phosphorus mwilini ni muhimu kuwezesha
afya njema ya mifupa, misuli na neva. Phosphorus inapozidi mwilini
mifupa huwa myepesi na rahisi kuvunjika suala linatokana na mwili
kushindwa kuhifadhi na kuitoa calcium kwenye mifupa. Vyakula ambavyo
vina phosphorus kwa wingi ni pamoja na maziwa na vyakula vya jamii ya
maziwa, nyama, shellfish, vyakula ambavyo havijakobolewa, maharage,
karanga, korosho na chokoleti. Wagonjwa wa figo pia huhitaji vitamini na
madini ya nyongeza kutokana na kutokula aina mbalimbali za vyakula na
hivyo kuweza kusababisha upungufu wa baadhi ya virutubishi. Damu
inapochujwa kwa njia ya dialysis pia huondoa vitamini kwenye damu kwa
hivyo vitamin hizo ambazo ni dharura kwa mwili hupaswa kufidiwa kwa kula
virutubishi vya nyongeza au supplements. Virutubishi vya nyongeza
vinapaswa kutolewa kwa mgonjwa wa figo baada ya ushauri wa daktari