NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Wednesday, February 4, 2015

TANESCO HAIWEZI KUSHUSHA BEI YA UMEME KWA SASA


KUSHUKA kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hakujawapa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) unafuu wa kuwafanya washushe bei ya umeme.
 
Aidha, serikali imesema haifumbii macho suala hilo na imeziagiza Mamlaka husika za Tanesco na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuangalia inapotokea fursa, ili iweze kwenda kwa wananchi.
 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Athumani Mfutakamba (CCM), aliyetaka kufahamu sababu za kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
 
Alihoji, kutokana na anguko hilo kwa nini gharama mbalimbali, ikiwemo bei ya umeme unaozalishwa na TANESCO, IPTL, Aggreko, Symbion haujashuka wakati mafuta yameshuka bei.
 
Akijibu swali hilo, Mwijage alisema uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kwa sasa ni MW 1,226.24 ,mitambo ya kufua umeme kwa maji inazalisha MW 561.84, gesi MW441, na mafuta MW 223.40.
 
Alisema kampuni za IPTL na Aggreko zinaiuzia Tanesco umeme kwa senti za Marekani 28 hadi 40 kwa uniti wakati Tanesco inawauzia wananchi umeme kwa senti za Marekani 16.4 kwa uniti.
 
“Kwa kuangalia takwimu hizo, ni dhahiri kuwa Tanesco inanunua umeme kwa bei juu kuliko inavyowauzia wananchi, hivyo kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hakujawapa nafuu wa kufanya washushe bei,” alisema Mwijage.
 
Alisema hali ya kushuka kwa bei za nishati ya mafuta duniani imetokana na kudorora kwa uchumi katika bara la ulaya, kuongezeka kwa matumizi ya nishati mbadala, kuimarika kwa utumiaji mzuri wa mafuta na ufanisi wa tija katika kuzalisha mafuta kutoka miamba ya Shale na mengineyo

Monday, February 2, 2015

UNYAMA WA KUTISHA - HII NI TANZANIA KWELI????? WAHUBIRI MPO WAPI????????


Huu ni ukatili namba moja kwa wanandoa duniani! Bado picha haijatoka kichwani kwa wakazi wa Manzese jijini Dar kufuatia kifo cha kuchinjwa cha  Josephine Ndengaleo Mushi kinachodaiwa kufanywa na mume wake wa ndoa, Remy Joseph (35).

Tukio hilo la kutisha kusimuliwa achilia mbali kuona, lilijiri saa 9: 10 alasiri ya Januari 29, mwaka huu ndani ya chumba kimoja kilichopo ghorofa ya pili ya  Hotel Friend’s Corner Ltd iliyopo Manzese Argentina, Dar.

Baada ya habari za mauji hayo kusambaa kama moto wa kifuu, waandishi wetu walianza kuichimba habari hii kwa kina.

Kwa mujibu wa mhudumu mmoja wa hoteli hiyo, Januari 28, mwaka huu, Remy na Josephine walifika kwenye hoteli hiyo na kuchukua chumba. Walionekana wenye amani, kwani hakuna sura iliyoonesha kuna tatizo.

“Walikuwa kama wateja wengine. Tena niliwauliza kama wanatoka mkoa, wakasema ni wakazi wa Dar es Salaam, wao ni mke na mume kwa ndoa, waliamua kulala hapa ili kuimarisha mapenzi yao, si lazima kila siku nyumbani,” alisema mhudumu mmoja.

Kwa mujibu wa baadhi ya wahudumu wa hoteli hiyo, siku ya pili, muda wa saa tisa alasiri, walishtuka kuona damu nyingi ikitoka ndani ya chumba walichopanga wawili hao.

“Tulishtuka sana. Tukajua kuna kitu kikubwa kimewapata. Ilibidi tuwagongee mlango ili tujue kilichowapata lakini mlango haukufunguliwa,” alisema mhudumu mwingine.

Kwa vile ukimya ulitawala ndani ya chumba hicho huku damu zikiendelea kutiririka, ilibidi uongozi wa hoteli hiyo yenye sifa ya ulinzi, uwasiliane na Kituo cha Polisi cha Ndugumbi ambacho kipo jirani.

Polisi walifika, wakagonga mlango kwa muda mrefu bila kufunguliwa mpaka baadaye sana ambapo mlango huo ulifunguliwa na mwanaume akiwa ameshika kisu mkono wake wa kuume.

Ndani ya chumba kulionekana damu zimetapakaa kila sehemu. Polisi walimsihi mwanaume huyo kuangusha kisu chini ili waongee lakini jamaa aligoma.

“Polisi walimwamuru mwanaume atupe kisu chini, akakataa. Sura yake wakati huo ilikosa mwonekano wa ubinadamu. Ndipo askari mmoja alitumia mbinu ya kivita, alimpiga mkono wake wa kulia kwa kumshutikiza kisu kikaangukia mbali, akawekwa chini ya ulinzi. Kumbe kile kisu mbali na kumuua mkewe alikitumia kujaribu kujichinja koo lakini ikashindikana,” alisema mhudumu huyo.

Mwanaume akiwa chini ya ulinzi na pingu mikononi, polisi waliingia chumbani na kukuta damu kila mahali. Cha kusikitisha zaidi, mwili wa marehemu Josephine ulipigishwa magoti, sehemu ya miguu mpaka magoti ikiwa sakafuni na kifuani kulalia kitanda. 
 
Halafu ulifunikwa shuka.“Kwa mbali ungeweza kusema kuna binadamu anasali kwa namna ambavyo marehemu huyo alivyokuwa amepigishwa magoti,” alisema mhudumu huyo.

Katika hali iliyoonesha kuwa, mtuhumiwa baada ya kutenda ukatili huo alitaka kujinyonga, polisi walikuta waya wa umeme wa tivii ukining’inia kwenye pangaboi lakini ukiwa umekatika.

Polisi walifanya uchunguzi chumbani na kugundua kuwa, marehemu Josephine alichinjwa shingoni, akakatwa mbavu mbili, moyo na maini vilikuwa nje ‘vikimwagika’, mwisho alichomwa kisu utosini.

Pia kwenye chumba hicho, polisi walikuta simu mbili, ya marehemu na ya mtuhumiwa zikiwa zimeharibiwa laini kiasi cha kukosa mawasiliano.

Mwandishi alipata bahati ya kuzungumza na mtuhumiwa huyo kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi Magomeni, Dar ambapo alisema Josephine alikuwa mke wake na wameishi kwa muda zaidi ya miaka kumi na kupata watoto wawili. Hata hivyo, hakuongea zaidi ya hapo.

Msimamizi mkuu wa hoteli hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Zuberi Hussein alipohojiwa  alisema:

“Tuliwapokea hawa watu kama wateja wengine. Walilipa shilingi elfu kumi na tano kwa chumba.  Hatukujua kama haya yangetokea, wahudumu ndiyo walibaini baada ya kuona damu ikitiririka mlangoni.”

Baadaye, polisi waliupakiza mwili wa marehemu kwenye gari kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili huku mtuhumiwa akipelekwa Kituo cha Polisi Magomeni jijini Dar pembeni yake akiwa amelala marehemu mkewe.

Baada ya hapo,Mwandishi wetu alifunga safari hadi eneo la Studio, Kinondoni, Dar nyumbani kwa David Ndeshao Mushi ambaye ni kaka wa marehemu na ndiko sehemu ulipowekwa msiba.

Baadhi ya ndugu wa marehemu walidai kwamba, Josephine na mumewe mara kwa mara walikuwa na migogoro  ya ndoa.

“Ndoa yao haikutulia, walikuwa wanapatanishwa lakini baada ya muda mfupi wanaanza tena ugomvi. Mumewe alikuwa akimhisi vibaya mke wake. Hata hivyo, Desemba mwaka jana, Josephine alienda kuishi kwa kaka yake kutokana na ugomvi,”alisema mmoja wa wanandugu wa karibu.

Kaka mtu  huyo alipohojiwa alisema: “Marehemu alirudi kwangu lakini tulikuwa hatujaongea naye kuhusu ugomvi wao. Nilisafiri mkoani nikamuacha, niliporudi, Jumatano alienda kazini lakini hakurudi. Tulipopiga simu yake akawa hapatikani. Mumewe naye akawa hapatikani hadi taarifa ilipotufikia kwamba kauawa hotelini.

“Tunatarajia kusafirisha mwili kwenda Moshi, Jumapili (juzi). Mazishi yatakuwa Jumatatu (jana). Marehemu ameacha watoto wawili ambao walikuwa wakiishi Tabata, Dar.”

Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa alikuwa mfanyakazi wa Baa ya Break Point iliyopo jijini Dar. Marehemu alikuwa mfanyakazi katika Kampuni ya TAC iliyopo Upanga, Dar.

Mmoja wa marafiki zake wa karibu alisema Jumatano mchana, mumewe alimfuata kazini na wakawa na mazungumzo, alimtaka waondoke lakini marehemu alikataa.Alimbembeleza sana mwishowe wakakubaliana na kuondoka lakini wakashangaa kusikia alimuua hotelini.

Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni - Mume Amcharanga Mapanga Mkewe, kisa Kachelewa Kupata Ujauzito


Mtu mmoja mwanamume, aliyetajwa kwa jina la John Weghai amemjeruhi vibaya mke wake, Anastazia John (18) kwa kumkatakata na mapanga kwa kile kinachodaiwa kuchelewa kwake kupata ujauzito, katika maisha ya wawili hao waliyoanza Februari mwaka jana.

Tukio hilo la kinyama lilitokea katika Kijiji cha Mariba, Kata ya Mriba, wilayani Tarime mkoani Mara na majeruhi huyo amelazwa katika hospitali ya Halmashauri ya Mji ambapo ameshonwa nyuzi 67.
 
Akizungumzia tukio hilo, msichana huyo alisema kuwa mumewe amekuwa akimpa matatizo mengi katika ndoa yake kiasi cha kumkosesha amani kwa kumpiga mara kwa mara akimtuhumu kuchelewa kupata ujauzito.
 
“Kwa kweli nimekuwa nikipata mateso makubwa tangu niishi na mwanaume huyu, nimekuwa nikipigwa mara kwa mara sababu nachelewa kupata mimba na yeye anataka mtoto.
 
“Naviomba vyombo vinavyotetea na kusaidia matatizo ya ukatili kama haya viweze kusaidia watu wanaofanyiwa maana yanaondoa utu wa mtu na kumfanya kuishi kinyonge,”alisema Anastazia.
 
Alisema siku hiyo alipata majeraha makubwa katika bega na titi lake la kushoto, kitu kinachompatia maumivu makubwa.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Valeria Msoka, alisema wamesikitishwa na tukio hilo, akisema ni ukatili uliopitiliza lakini wataendelea na jitihada za kupambana na matukio ya namna hiyo katika jamii.
 
Alisema muda mfupi tu umepita tokea warejee kutoka wilayani Tarime wakiwa na ugeni mkubwa wa kimataifa kupambana na masuala ya ukatili na kutoa ujumbe kwa wananchi juu ya athari zake lakini kuna watu hawajabadilika.
“Tulitoa maoni kwenye Katiba mpya inayopendekezwa na tunashukuru yamepita juu ya kuangaliwa upya kwa sheria ya wanaofanya makosa ya ukatili kwenye jamii huenda ikaja kuwa suluhisho juu ya matukio haya,”alisema Msoka.
 
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda maalum ya kipolisi Tarime/Rorya limesema mtuhumiwa bado hajakamatwa na jitihada za kina zinaendelea kufanywa ili kuhakikisha anakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
 
Kaimu Kamanda wa Tarime/Rorya, Sweetbet Njwewike alisema katika tukio hilo lililotokea Januari 22 mwaka huu lilichelewa kutolewa taarifa jambo ambalo limechelewesha kupatikana kwa mtuhumiwa.
 
Tukio hilo limetokea siku chache tu tokea mke wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Graca Machel kuwepo wilayani Tarime, akihamasisha kampeni ya kuepuka ukatili kwa watoto na akina mama.

BUNGENI LEO: Kangi Lugola ( CCM ) Awasha moto bungeni


MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), amewasha moto bungeni akifunguka kuwa atawaambia wananchi wake wasiipigie kura CCM pamoja na yeye mwenyewe kama maji hayatapatikana jimboni mwake wakati akichangia katika majiadiliano ya hoja za kamati bungeni leo.
 
Pia Lugola amehoji kwa nini nguvu zinazotumika kuwapiga watu kama akina Profesa Lipumba zisitumike kupambana na wawekezaji wanaokiuka masharti ya uwekezaji na kuwanyanyasa wananchi huku akimtaka Waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mhe. William Lukuvi kushughulikia vilivyo kero za ardhi.

BONDIA MAARUFU FRANCIS CHEKA MJINI MOROGORO AFUNGWA JELA MIAKA MITATU

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh9G5TVJJ5l2R93m2uISA0R8n4n-MW-20YXBlgUzmYXxwD2Cy0kMFqHrz9zuxX0Btk1OrN3OWKbHBp0pOKqkoblP2Cq1fdJxeWdeFDtXDCtqsBENXSIw8gyGwxnuepmxFXhYtpLlV3JLOg/s640/Bondia-Francis-Cheka.jpg

Bondia wa ngumi za kulipwa Tanzania, anayeshikilia mikanda lukuki ikiwemo wa mkanda wa WBF, Francis Cheka, amefungwa kifungo cha miaka mitatu jela leo Februari 02/ 2015 kwa kosa la kumshambulia Meneja wake mkoani Morogoro katika mahakama ya hakimu mkazi Morogoro. Kifungo hiki ni fundisho kwa wengine watakaotumia uwezo wao au nyadhifa zao kutenda mambo ndivyo sivyo.

Sunday, February 1, 2015

RUSHWA: Magufuli Awafukuza Kazi Wafanyakazi 400 wa Mizani


Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli amevitaka vyombo vya dola kuingilia kati suala la rushwa kwenye vituo vya mizani za kupimia uzito wa magari yanayosafirisha mizigo, akisema rushwa hiyo imekithiri.

Magufuli alitoa agizo hilo alipotembelea na kukagua kituo cha mizani cha Mpemba wilayani Momba, ambapo alipita kituoni hapo kwa kushtukiza, alipokuwa katika ziara yake ya kukagua barabara akielekea wilayani Ileje.
 
Kupita kwa Magufuli kwenye mizani hiyo, kulitokana na yeye kujionea namna barabara ya kati ya Mbeya na Tunduma ilivyoharibiwa, kutokana na malori yanayosafirisha mizigo inayozidi uzito unaotakiwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mpaka wa Tunduma kabla ya kuvushwa kuelekea nchi jirani.
 
Baada ya kufika kituoni hapo, alihoji maofisa waliokuwa zamu ni kwa nini barabara ionekane kuharibika upande mmoja wa magari yanayotoka Mbeya kwenda Tunduma badala ya pande zote mbili.
 
Maofisa hao walimweleza kuwa kuharibika kwa upande huo wa barabara, kunatokana na malori kutoka Mbeya kwenda Tunduma, kutopimwa uzito kwakuwa hakuna mizani nyingine kabla ya kufika kituoni hapo.
 
Hata hivyo, majibu ya maofisa hayo hayakumridhisha waziri huyo na ndipo akatupia lawama utendaji kazi wa maofisa wa vituo vya mizani, akisema umekithiri kwa kupokea rushwa.
 
Alisema licha ya serikali kuwafukuza kazi watumishi 400 wa idara hiyo mwaka jana na kuajiri upya, bado tatizo la upokeaji rushwa kwa watumishi waliopo ni kubwa mno.
 
“Mwaka jana tuliamua kuwafukuza kazi watumishi 400 waliokuwepo kwa kuwa tuliona wamejikita katika rushwa badala ya kutimiza majukumu yao. Hapo tukaajiri watu walio na elimu nzuri tukijua tumetibu tatizo. Lakini bado rushwa inaendelea. Matokeo yake barabara zetu zinaendelea kuharibika,” alisema.
 
“Watumishi wa vituo vya mizani ni mabilionea wakubwa. Hii yote ni kwa kuwa wanapokea rushwa kutoka kwa watu wanaosafirisha mizigo iliyozidi uzito na kuharibu barabara zetu,” alisisitiza.
 
Alisema ni wakati sasa kwa vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) na Idara ya Upelelezi ndani ya Jeshi la Polisi, kufanya uchunguzi kwa maofisa wa vituo vya mizani nchini.
 
Alisema iwapo vyombo hivyo vitalifanyia kazi suala hilo, visisite kuchukua hatua stahiki kwa watumishi watakaobainika na kuzitaka pia ofisi za makatibu tawala wa mikoa, kufuatilia suala hilo

POLISI ACHOMOKA LINDO USIKU NA KWENDA KUUA RAIA


Jeshi la Polisi Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, limeingia katika kashfa baada ya askari wake kutuhumiwa kumuua raia.

Raia huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mdonga, fundi wa magari, Januari Mtitu (20), inadaiwa kuwa aliuawa kwa risasi na askari mwenye namba G 6352, Abduel Nyuki.

Tukio hilo lilitokea Januari 23, mwaka huu, saa 7:00 usiku, na mtuhumiwa anafanya kazi katika Kituo cha Polisi Ludewa.

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Juma Madaha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa tayari askari anayetuhumiwa na raia wengine wawili, wamekamatwa.

Habari zinaeleza kuwa wakazi wa eneo la tukio, walipandwa na hasira na kumfanya Mkuu wa huyo wa Wilaya kulazimika kuwatuliza kwa kuwataka wapunguze hasira ili wasiwadhuru polisi wengine kwa sababu siyo wote waliohusika na tukio hilo.

Kauli ya Mkuu huyo wa Wilaya ilitokana na mgomo wa mafundi wa magari kukataa kutengeneza jeneza na kutaka kuandamana huku wakilitaka Jeshi la Polisi kulitengeneza wenyewe ama kulipa fedha kwanza ndipo litengenezwe.

“Sasa hivi tumechoka kuteswa na kunyanyaswa na polisi, wanaacha kukamata wahalifu badala yake wamewageukia wananchi ambao hawana hatia na leo hii wamemuua mwenzetu bila kosa,” mmoja wa mafundi hao alisema.

Mdogo wa marehemu, Imani  Mtitu, alisema kabla ya kupigwa risasi, kaka yake alisikia akizungumza na mtu kwa njia ya simu huku wakijibizana kwa ukali na baada ya muda mfupi, walifika watu wakagonga mlango wa marehemu na alipokataa kufungua, waliuvunja na muda mfupi ulisikika mlio wa bunduki.

“Nilipotaka kutoka ili kumpa msaada kaka yangu, niligundua kuwa mlango umefungwa kwa nje na nilipofanikiwa kutoka nilikuta marehemu (Mtitu) akiwa amelala chini damu zinatoka, lakini anashindwa kuongea,” alisema Imani.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ludewa, Galiya Moshi, alisema chanzo cha tukio hilo ni askari Nyuki akiwa lindoni kwake katika Benki ya NMB tawi la Ludewa, alipigiwa simu na mpangaji mwenzake kwamba katika chumba chake kulikuwa na wizi, ndipo alipoacha lindo saa 7:00 usiku na kumfuata marehemu nyumbani kwake baada ya kutajwa na rafiki zake kuwa ndiye aliyehusika.

Moshi alisema kuwa watu wengine wawili ambao majina yao tunayahifadhi, wanashikiliwa na polisi.

Watu hao wanashikiliwa kutokana na kumpeleka askari huyo nyumbani kwa marehemu.

Alisema kuwa katika upekuzi, marehemu alikutwa  na vielelezo  mfukoni mwake ambavyo ni  ‘flash’ na ‘remote’ ya tv, vitu ambavyo vilitambuliwa na mtuhumiwa.

Licha ya kuwa na mvutano huo, marehemu alizikwa katika makaburi ya Lugarawa mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya baada ya mvutano mkali uliokuwapo kati ya wananchi wa kijiji cha Lugarawa, wazazi na Polisi ambao walikuwa wakituhumiwa kumuua marehemu kwa makusudi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa askari huyo ameshafukuzwa kazi.