CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), kimesema
kuwa kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa lengo la
kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kubomoa mfumo unaowanyonya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, kimewahakikishia Watanzania kuwa ujio wa chama
hicho ni wa kuleta mageuzi ya kweli kwa taifa badala ya porojo kama
vyama vingine vinavyofanya.
Akihutubia wananchi jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika
Uwanja wa Shule ya Msingi Ukombozi, mjini Singida, Kiongozi wa
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuwa hivi sasa Taifa limekuwa na
shauku ya ACT kushirikiana na vyama vingine kama njia ya kufanikisha
malengo ya kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), madarakani.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni lazima Taifa lijengwe upya kwa
matumaini, ikiwamo kuhakikisha vyama vinakuwa na ushirikiano wa dhati
utakaoleta mageuzi ya kimfumo na uchumi kwa Watanzania wote.
“Kumekuwa na shauku ya wananchi kwa sisi kushirikiana na vyama vingine
vya siasa ili kufanikisha malengo yetu ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi
kwa kuubomoa mfumo wa uchumi unaonyonya wananchi. Msimamo wetu upo wazi
na tumeueleza mara kadhaa.
“ACT- Wazalendo tunaunga mkono juhudi zozote za kushirikiana kwa vyama
na hili linathibitishwa na jina letu, Alliance na msimamo wetu kuhusu
mabadiliko ya Katiba. Kubwa tunataka ushirikiano utakaonufaisha wananchi
na si ushirikiano wa kugawana nafasi za uongozi,” alisema Zitto.
Kiongozi huyo wa ACT alisema chama chao hakina tatizo na kipo tayari
kushirikiana na chama chochote kilichokuwa tayari kushirikiana nao,
ikiwemo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kuunganisha nguvu
kukitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema umoja huo ni lazima uwe na malengo ya kujenga uchumi shirikishi
wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, wenye mfumo wa hifadhi ya jamii
kwa wananchi wote na wenye kutokomeza umasikini.