NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Tuesday, May 26, 2015

BVR Kigoma yalalamikiwa......Wananchi Walala Kituoni Kujiandikisha


Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektoronik BVR umelalamikiwa na wananchi katika manispaa ya Kigoma Ujiji kutokana na kuchelewa kuandikishwa licha ya wananchi kulala kwa zaidi ya siku mbili katika vituo vya kuandikishia.

Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo huo limeanza katika kata za Kagera, Buhanda, Businde, Machinjioni, Rubuga na Kasimbu huku kata nyingine zikisubiri awamu ya pili hali ambayo inawafanya wananchi wa kata nyingine kwenda kujiandikisha katika kata zilizoanza zoezi hilo kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi.
  
Kutokana na hali hiyo wameomba kuongezwa kwa muda wa uandikishwaji wapiga kura na kuweka utaratibu mzuri ambao utawezesha wananchi wote wenye sifa kuandikishwa
  
Kwa upande wake afisa mwandikishaji msaidizi katika kata ya Buhanda Sufiani Baruani amesema zoezi hilo linakabiliwa na tatizo la idadi kubwa ya wananchi kulingana na uwezo wa mashine zilizopo.
  
Awamu ya kwanza ya uandikishaji wapiga kura mkoani Kigoma imeanza katika baadhi ya kata Mei 21 huku ikiripotiwa kusimama kwa zoezi hilo katika kata ya Nguruka kutokana na kuishiwa kadi huku maelfu ya wananchi wakiwa bado hawajaandikishwa.

Mbio za Urais Za Benard Membe Zitaanzia Kijijini Kwake


Siku mbili baada makada waliokuwa wamefungiwa kwa makosa ya kukiuka kanuni za CCM kuachiwa huru, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameeleza nia yake kuwa wakati ukifika atachukua fomu kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
 
Membe alibainisha nia hiyo kwa mara ya kwanza juzi usiku wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na kuwa atatangaza azma hiyo muda wowote kuanzia sasa akiwa jimboni kwake, Mtama mkoani Lindi.
 
“Sasa ni rasmi kuwa nina nia ya kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitatangaza nikiwa kijijini kwangu… mahali nilipoanzia safari ya kwenda shule, safari ya kwenda usalama wa Taifa na safari ya kwenda Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema.
 
Membe alikuwa miongoni mwa makada sita CCM waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi wakituhumiwa kuanza kampeni mapema kinyume na taratibu za chama hicho kilicholazimika kuwachukulia hatua za kinidhamu.
 
Makada hao walifungiwa tangu Februari, 2014 na pamoja naye ni mawaziri wakuu wa zamani; Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
 
Akifafanua juu ya dalili za kutimia kwa ndoto yake za kuiongoza nchi, Membe alisema Mwenyezi Mungu ana namna nyingi za kufikisha ujumbe kwa mja ampendaye katika kumtumikia kwa mtindo autakao yeye.
  
“Nimegundua kuwa unaposema naomba nioteshwe… naomba nioteshwe kumbe Mungu anayo namna nyingine. Anawaotesha wengine kwa ajili yako na ndivyo alivyofanya,” alisema.
 
Kuhusu hilo, Membe alisema kila mtu anasubiri kuona CCM inatoka vipi na hata vyama vya upinzani vinasubiri hilo na ndiyo maana navyo vimenyamaza.
 
Mpaka sasa ni chama cha Tanzania Labour (TLP), kilichokwisha teua mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo, Macmillan Lyimo.
 
“Watanzania wote macho yao yapo CCM, wanasubiri kuona inafanya nini. Tunaona vyama vingine vimekaa kimya, wanasubiri CCM iseme ili nao wafuate. Wanapiga kelele za Ukawa…Ukawa lakini hawawezi kufanya chochote. Hata kama tutasogeza muda mbele bado wataendelea kusubiri,” aliongeza.
 
Hali ya usalama Burundi
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuzungumzia hali ya usalama inayoendelea kuyumba nchini Burundi kwamba kikao cha mawaziri kinatarajia kuketi baada ya muda mfupi jijini Arusha ili kuona namna ya kutatua mzozo uliopo.
 
Alisema Tanzania isingekwa radhi kuona mapinduzi ya utawala wa Rais Pierre Nkuruzinza yanafanywa wakati akiwa nchini tena kwa mwaliko na gharama za nchi hii. Alisema hiyo ingemaanisha Tanzania inahusika nayo.


“Hilo haliwezi kufanyika kwa nchi hii. Tulilazimika kumrudisha na kama wanataka kufanya mapinduzi wayafanye wote wakiwa huko. Tanzania siyo nchi ya kuichezea na tusingeweza kukubali kuona hilo linatokea."
 
Alitanabaisha utata uliojitokeza baada ya Rais Nkuruzinza kutaka kugombea tena muhula wa tatu kuwa ulishafafanuliwa na mahakama nchini humo ambayo ilimruhusu kugombea.
 
“Tuliposuluhisha mgogoro wao wa awali, Bunge lao la mpito liliridhia kuwa Nkurunziza aiongoze nchi hiyo mpaka uchaguzi mkuu utakapofanyika. 
  
"Aliiongoza Burundi kwa miaka mitano uchaguzi ukafanyika na akachaguliwa. Katiba ya nchi hiyo inatoa muda wa miaka 10 kwa kiongozi mmoja lakini kwa yeye miaka mitano haikutokana na kuchaguliwa, ndiyo maana aliruhusiwa na Mahakama,” alisema.
 
Alifafanua pia kuwa usalama wa kila nchi ni muhimu kwa mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hiyo ndiyo maana wakuu wa nchi hizi walilaani mapinduzi hayo punde tu yalipofanyika wakati wakuu hao wakikutana nchini.
 
Akifafanua kuhusu mchakato wa kusuluhisha pande mbili zinazokinzana nchini humo, Membe alisema iwapo mawaziri watashindwa kupata suluhu katika kikao kinachotarajiwa kufanyika, watalazimika kumshauri Mwenyekiti wa EAC, Rais Jakaya Kikwete hatua zaidi za kushughulikia amani ya nchi hiyo.
 
Hadi sasa makumi ya wananchi wameuawa tangu kuanza kwa vurugu nchini Burundi huku maelfu ya wakimbizi wakikimbilia Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Saturday, May 23, 2015

Hospitali ya AMI Yafungwa Rasmi


HATIMAYE Hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Center ya Masaki Dar es Salaam, imefungwa rasmi na mmiliki wa jengo kukabidhiwa funguo zake.
 
Hospitali ya AMI na ya gharama ya juu  ilikuwa ikitoa matibabu kwa viongozi wa ngazi za juu wa Serikali, wabunge , mabalozi na wafanyabishara wakubwa wa ndani na nje ya nchi.
 
Kufungwa kwa hospitali hiyo kumetokana na kushindwa kulipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi 26, inayofikia zaidi ya dola za Marekani milioni 1.6, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni tatu.
 
Makabidhiano hayo yalifanyika jana hospitalini hapo kati ya Mwakilishi wa Kampuli ya udalali wa Mahakama ya MEM Auctioneers and General Brokers Ltd, Elieza Mbwambwo kwa Meneja wa jengo hilo, Zurfiq Hassanar, dalali huyo wa mahakama alisema hatua hiyo ya kuhamishwa kwa hospitali hiyo imetokana na uamuzi wa Mahakama Kuu.
 
“Ninapenda kusema leo (jana), tunakabidhi jengo na funguo zake kwa Meneja wa jengi hili kwa niaba ya mteja wetu, wiki mbili zilizopita tulikamata mali  baada ya AMI kushindwa kulipa deni kama ilivyoamriwa na mahakama.
 
“Mahakama Kuu ilichoamuru mali za AMI zikamatwe na kupigwa mnada  ili kuweza kulipa deni lao la pango na kisha kuondolewa kwenye jengo na kumkabidhi mmiliki  wake Navtej Singh Bains,” alisema Mbwambo.
 
Mali zilizokamatwa ni magari matatu ya kubebea wagonjwa (Ambulance), vitanda maalumu vya kulaza na kuwahudumia wagonjwa, gari ndogo aina ya Mark II, mashine mbalimbali pamoja na samahani zilizokuwa zikitumiwa katika jengo hilo.
 
“Tulipokuja awali tulitoa taarifa kwa ndugu wa wagonjwa wawe wamewaondoa wagonjwa wao na sasa jengo ni nyeupe halina mtu ndani, hata mali tilizokamata tutazipiga manda ingawa tunajua haziwezi kufikia thamani ya fedha zinazodaiwa, maana kwa sasa kuna maombi mengi ya watu wanataka kufungua hospitali hapa,” alisema
 
Alisema mashine za CT -Scan, X-ray ni miongoni mwa zitakazopigwa manda huku atakayepanga katika jengi hilo akipewa kipaumbele cha kwanza.
 
Hatua hii ya kufukuzwa kwenye jengo imefikiwa baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria baina ya AMI na mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki wa jengo hilo, Navtej Singh Bains. 
 
Taarifa zaidi inasema kwamba akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zilikutwa zikiwa zimefungwa na fedha zote zikiwa zimetolewa.

Amri ya kufurushwa kwa AMI ilitolewa Mei 7, mwaka huu na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. 
 
Ofisa Mtendaji Mkuu wa AMI Plc, Theunis Peter Botha, ambaye pia ni Mkurugenzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya AMI Tanzania, aliwasilisha ombi Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa imefilisika.
 
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake hospitalini hapo, Rose Sesoa, alisema pamoja na kufungwa kwa hospitali hiyo hivi sasa hawajui hatima yao.
 
“Tunaiomba Serikali ichukue hatua sasa.Wakija wawekezaji wageni wawabane kwa maswali maana leo hili limetokea na hapa tupo Staff zaidi ya 100 hatujui tufanye nini. Kikubwa  ni makato ya NSSF ambayo imekuwa ikituma watu wake lakini wakifika hapa wanapewa bahasha na kunyamaza huku Makato hayapelekwi,” alisema Sesoa.
 
AMI Tanzania inamilikiwa na Kampuni mama ya AMI Plc ya London ambayo iliondolewa kwenye Soko la Hisa la London mnamo Februari 2014 baada ya jaribio la kuuza mali zake zilizopo nchini Maputo bila kibali kutoka kwa wanahisa.
 
Pia kumbukumbu zinazoonyesha kuwa Lancet Laboratory (T) Ltd iliwasilisha ombi la dharura dhidi ya kufungiwa kwa Hospitali ya AMI ikiwa inaidai hospitali hiyo zaidi ya Sh  milioni 150.
 
Hata hivyo wakati inafungwa hospitali hiyo, baadhi ya wazabuni walikuwa hospitalini hapo huku wakiwa hajui la kufanya juu ya hatima ya malipo yao.

Thursday, May 21, 2015

Kipindupindu Chalipuka kwa wakimbizi wa Burundi Walioko Katika Kambi ya Kigoma.


WAKATI hali ya usalama nchini Burundi ikiwa bado tete, wakimbizi 558 walioko katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma wanaugua ugonjwa wa Kipindupindu.
 
Ugonjwa huo ulilipuka hivi karibuni baada ya wakimbizi hao kuingia nchini wakikimbia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.
 
Akizungumza jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe, alisema hadi sasa wakimbizi 15 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
 
Alisema tangu Aprili 24 mwaka huu wakimbizi 2,458 walikuwa wakiharisha na kutapika na sampuli 11 kati ya 13 zilizochukuliwa juzi zilithibitisha kuwa wanaugua ugonjwa wa kipindupindu.
 
“Tumeshirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na tayari tumepeleka timu ya wataalamu ambao wametembelea maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kutathmini na kutoa elimu ya afya kwa umma.
 
“Tumefanya tathmini katika mikoa ya Kagera, Geita na Katavi ambayo inapakana na Burundi,” alisema Dk. Kebwe.
 
Alisema wamepeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya dharura pamoja na kuanzisha mfumo wa kufuatilia magonjwa yakiwemo ya mlipuko katika maeneo yaliyoathiriwa.
 
Kwa mujibu wa Dk. Kebwe, ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kula chakula au kunywa kinywaji chenye vimelea vinavyosababisha kuharisha ambavyo hupatikana kwenye kinyesi, matapishi au majimaji kutoka kwa mgonjwa.
 
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuharisha mfululizo bila maumivu ya tumbo, kinyesi cha majimaji kinachofanana na maji ya mchele, kutapika mfululizo, kuishiwa nguvu na kwamba ndani ya masaa sita kama hakuna huduma mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
 
Kuhusu gharama za matibabu, alisema wametoa kwenye akiba ya magonjwa ya dharura na mlipuko lakini zitarejeshwa baadaye na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
 
Alitoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, usafi wa vyoo, kunywa maji safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya kutoka chooni na kusafisha vyakula

Rais Pierre Nkurunziza Asogeza Mbele Uchaguzi wa Wabunge Kwa Siku 10


Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amesogeza mbele uchaguzi wa wabunge kwa siku 10 hadi Juni 5 mwaka huu kufuatia jaribio la mapinduzi.

Msemaji wa Rais, Willy Nyamitwe ameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa kufuatia jaribio la mapinduzi la wiki iliyopita na vurugu zilizofuatia ni bora kusogeza mbele uchaguzi huo kwa muda.
 
"Uchaguzi huo wa wabunge ulikuwa umeratibiwa kufanyika Mei 26 mwaka huu lakini sasa inatubidi kuusogeza mbele mpaka Juni 5 mwaka huu ili kuwasikiza washirika wetu wa kimataifa pamoja na tume ya uchaguzi ambayo pia inatumia muda huo kutatua maswali yaliyoulizwa na vyama vya upinzani" alisema Nyamitwe.

Mpaka sasa tarehe rasmi ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanywa Juni 26 mwaka huu bado haijabadilika na nia ya Rais Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu ipo palepale.

Wednesday, April 29, 2015

Rais Kikwete Azindua Meli Mbili Za KIVITA Kwa Kishindo Jijini Dar


RAIS Jakaya Kikwete, jana amezindua na kuzitunukia Kamisheni meli mbili za kivita za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Kamandi ya Wanamaji ambazo zitatumika kufanya doria na kulinda mipaka ya majini katika Bahari ya Hindi.

Meli hizo zimepewa majina ya P77 Mwitongo na P78 Msoga zenye urefu wa mita 60 na zina uwezo wa kufanya doria katika kina kirefu cha maji.

Rais Kikwete alisema, kupatikana kwa meli hizo kumeifanya Tanzania kuandika ukurasa mpya wa uhusiano kati yake na China ambao uliasisiwa na waasisi wa mataifa hayo hayati Mwalimu Nyerere na Mao Tse Tung.

Alisema meli hizo zimekuja nchini kwa msaada wa Serikali ya Watu wa China zikiwa na uwezo wa kubeba silaha nzito kila moja ikiwa na mizinga miwili mikubwa na midogo sita.

"Jeshi letu la Wanamaji wakati linaanzishwa 1971, lilisaidiwa na Serikali ya China meli 13, rada na wataalamu wetu kupatiwa nafasi mbalimbali za mafunzo...meli hizi zitatuongezea ulinzi katika mipaka yetu majini.

"Kilio kikubwa cha jeshi letu kilikuwa uwezo mdogo wa meli zetu, tumekuwa na kazi ya kutafuta meli hizo na sasa tuna mpango wa kuchukua meli nyingine kubwa zaidi zenye uwezo, kilichobaki ni taratibu za kifedha tu," alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, lazima Tanzania ijenge uwezo wa kulinda mali zetu, mipaka, samaki na mitambo ya gesi ambayo imesimikwa baharini hivi karibuni.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi, Dkt. Hussen Mwinyi, alisema Serikali ya China imekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania.

Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua mara baada ya kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam jana April 28, 2015
Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata picha ya kumbukumbu na makamanda wa meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam jana April 28, 2015Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema jeshi hilo limepiga hatua katika ununuzi wa dhana za kivita na kuendeleza mafunzo ya kijeshi.


Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Chifu Edward Wanzagi wa kabila la Wazanaki (kati) pamoja na Mbunge wa Afrika Mashariki Mhe Makongoro Nyerere baada ya kuzindua rasmi meli vita mbili za doria bahari kuu TNS Msoga na TNS Mwitongo kwenye sherehe zilizofanyika Kamandi ya Jeshi la Maji Kigamboni jijini Dar es salaam jana April 28, 2015.
 
(PICHA NA IKULU)

Tuesday, April 21, 2015

HABARI MPYA LEO TAREHE 21.04.2015 : Majambazi Yatiwa Mbaroni jijini Dar Yakiwa na Bunduki 2

Watuhumiwa wa Ujambazi wakiwa wamewekwa chini ya Ulinzi mara baada ya kutiwa mbaroni kwenye mataa ya Red cross katikati ya jiji Dar es salaam mchana huu.
 
Inaelezwa kuwa Majambazo hao walimvamia na kumpora raia mmoja wa kigeni (Mzungu) maeneo ya Kinondoni na kufanikiwa kukimbia, lakini kumbe wakati wanafanya tukio hilo kuna raia aliwaona na alijitolea kuwakimbiza kwa gari na kufawanikiwa kuwablock maeneo hayo ya Red Cross ambapo huwa na askari wengi wa doria, wamekamatwa na bunduki mbili.