NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Wednesday, July 22, 2015

Mbowe Asema UKAWA Wana Mgombea Makini.......Asema Atajulikana hivi punde


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe amesema pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika Ukawa, lakini wanajitahidi kumpata mgombea mmoja.
 
Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika jijini Mwanza, ambapo pia aliwatambulisha wabunge waliohamia Chadema kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge wa Kahama, James Lembeli na mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mara, Ester Bulaya.
 
Mbowe alisema viongozi wanaounda Ukawa, wanaendelea kushirikiana ingawa kuna changamoto kadhaa. Lakini, watatumia kila mbinu kuhakikisha anapatikana mgombea mmoja kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
 
“Tunaendelea kushirikiana lakini kuna changamoto, kama viongozi tutatumia kila mbinu tuwe na mgombea mmoja wa Ukawa na mazungumzo yoyote yanahitaji uvumilivu, kuheshimiana na kushirikiana,” alisema Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai.
 
Hata hivyo, Mbowe alisema umoja huo hautatangaza mgombea wao kwa haraka, kama ambavyo wananchi wanatarajia, kwa sababu tu CCM wamekwisha kumtangaza wao, ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
 
“Tutamtangaza mgombea wetu kwa muda muafaka na watanzania wote watafurahi…hatuwezi kutangaza kwa sababu tu CCM wametangaza mgombea wao,” alisema Mbowe.

Tuesday, July 21, 2015

Mbunge wa Kahama Kupitia CCM, James Lembeli Atangaza Kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na CHADEMA


2015 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu Tanzania, kila siku stori za Siasa zimekuwa kwenye headlines nyingi kuanzia Magazetini, kwenye TV,  mitandaoni  na Radioni .

Mbunge James Lembeli alikuwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili.. kuna habari za baadhi ya Wabunge wametangazwa kuhama Vyama vyao, Lembeli kathibitisha kuhama CCM kwa maneno yake mwenyewe.

"Nimetafakari, nimezungumza na mama yangu kwa zaidi ya saa kumi.. mke wangu na watoto wangu, na kwa kusikia kilio cha wananchi wa Jimbo la zamani la Kahama nimeamua kutangaza kuanzia leo kwamba natangaza kujiondoa uanachama wangu ndani ya CCM" - James Lembeli.

"Nilikipenda lakini nimelazimika kuchukua uamuzi huu, najua nawakera wengi lakini nawaomba waangalie hali ambayo Viongozi wa CCM Wilaya ya Kahama wamesababisha niamue uamuzi huu mgumu.

"Kuanzia leo najiunga na CHADEMA… Namshukuru Rais Kikwete, nafikiri atakuwa mtu wa kwanza kuamini haya ninayosema, mwaka 2010 mizengwe iliyofanyika lengo lake ilikuwa kukata jina langu, kila mtu anafahamu Rais mwenyewe aliwahi kuniambia lakini Rais Kikwete ndiye aliyerudisha jina langu… Ninaahidi nitaendelea kufanya kazi nae mahali popote, na MUNGU naomba anisaidie niweze kuvuka salama katika haya"- James Lembeli.

Monday, July 20, 2015

MAJAMBAZI WALIOVAMIA STAKISHARI, WAKAMATWA

Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limefanikiwa kuwakamata majambazi watano wanaodaiwa kuhusika na tukio la uvamizi katika kituo cha polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema Majambazi hao wamekamatwa Mbagala ambapo katika tukio hilo pia wamekamata pia fedha shilingi milioni 170 na bunduki 16 miongoni mwao ni zile zilizoibiwa katika kituo cha Stakishari.
East Africa Television (EATV)'s photo.

ESTHER BULAYA AITOSA CCM



Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Chama Cha CCM, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Esther Bulaya mbunge machachari , kuitosa CCM kwa kutangaza uamuzi wake wa kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho
CHANZO CHA HABARI ..... EAST AFRICA TELEVISION

Benard Membe Atangaza Kuachana Na Siasa.......Asema Hatagombea Wadhifa Wowote Mwaka Huu


Waziri wa Mambo ya Nje na  ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe, amesema hatogombea wadhifa wowote kwenye uchaguzi mkuu wa  mwaka huu na kwamba anapanga kujishughulisha na masuala yake ya kibinafsi.

Membe ambaye alikuwa akitafuta tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania urais mwezi Oktoba lakini akashindwa kufikia lengo hilo, amesema kuwa, hatotafuta nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtama.

Hata hivyo amesema ataendelea kukiunga mkono chama chake cha CCM na atampigia debe mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Bw. John Magufuli.

Awali kulikuwa na tetesi kwamba Membe angegombea ubunge baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Huku hayo yakijiri, chama cha Mapinduzi  (CCM) kinaendelea kupata pigo baada ya baadhi ya wabunge wake kutangaza kuwa hawatogombea tena nafasi zao kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Tayari madiwani 20 wa CCM katika jimbo la Monduli wametangaza kuhamia Chadema na kumtaka mbunge wao, Edward Lowassa kufuata mkondo huo.

CUF Yasema CCM Ilimuonea Edward Lowassa.......Yasema Ipo Tayari Kumpokea Kwa Kuwa Ni Mtu Safi, Asiye Na Doa lolote


Chama  cha Wananchi (CUF), kimeibuka na kumtetea aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (pichani juu), kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilimuonea kwa kukata jina katika ngazi ya Kamati ya Maadili na kushindwa kulifikisha  Kamati Kuu ya CCM (CC).

Lowassa alikatwa jina lake akiwa ni miongoni mwa wagombea 38 wa urais kupitia CCM, lakini inadaiwa kwamba aliondolewa katika hatua za awali kwenye Kamati ya Maadili.

Kadhalika, CUF kimesema kipo tayari kumpokea Lowassa ndani ya chama hicho kwa kuwa ni msafi na hajawahi kufikishwa hata mahakamani kwa ajili ya kushitakiwa kutokana na madai ya rushwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Pilikapilika za uchaguzi nchini kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Star Tv.

Kambaya alirejea ripoti ya Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe mwaka 2008 kuchunguza kashfa ya Richmond ambayo ilimng'oa Lowassa katika nafasi ya Waziri Mkuu.

Alisema katika kamati hiyo, Dk. Mwakyembe aliweka bayana kwamba kila mtu aliyehusishwa ama kutajwa katika kashfa ya Richmond angefikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Kambaya alisema mpaka sasa Lowassa hajawahi kufikishwa mahali popote kushitakiwa na kwamba hatua hiyo inaoonyesha kwamba kiongozi huyo hakuwa na kashfa yoyote.

Alisema lengo la CUF ni kuing'oa CCM na kwamba ukiona kuna mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuitikisa chama hicho na kukipasua wapo tayari kumkaribisha ili washirikiane naye.

Alifafanua kuwa mtu ambaye siyo msafi hawezi kukaribishwa CUF na kwamba Lowassa kama angekuwa mchafu angekuwa ameshitakiwa mahakamani tangu alipojiuzuru mwaka 2008. Katika mjadala huo washirki walijadili matumizi makubwa ya fedha yaliyojionyesha ndani ya CCM tangu mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu ulipoanza.

Watu wengine waliojitokeza kumtetea Lowassa ni pamoja mwanachama mwenye kadi namba nane ya CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye alitamka wazi kwamba kanuni na sheria ndani ya chama zilikiukwa.

Kingunge alisema haki haikutendeka kwa sababu Kamati ya Maadili kwa mujibu wa kanuni na taratibu za CCM haina mamlaka ya kukata jina la mgombea kwa sababu siyo kikao cha maamuzi. Wakati hayo yakisemwa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amewaonya watu wanaokisema vibaya chama hicho na kwamba kitawachukulia hatua.
 
Source: www.mpekuzihuru.com
 

Sunday, July 19, 2015

Lembeli: Sitagombea ubunge kupitia CCM


Mbunge wa Kahama, James Lembeli ameiweka njia panda CCM baada ya kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
 
Uamuzi wa Lembeli umekuja wakati wanachama kutoka sehemu mbalimbali wakitangaza uamuzi wao wa kujiengua CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hasa Chadema ambayo imesomba asilimia kubwa ya wahamaji hao.
 
Akizungumza  jana baada ya kuzagaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii kuwa amekihama chama chake na kuhamia Chadema, Lembeli alisema taarifa hizo ni uvumi uliozagaa jimboni kwake, lakini hajajiunga na chama chochote.
 
“Ni uvumi tu na uvumi wenyewe umechangiwa na swali nililoulizwa leo na wananchi kwamba ‘mbona toka mchakato wa kuchukua fomu umeanza hatujakuona’ na mimi nikawajibu kuwa ‘sitachukua fomu’,” alisema.
 
Lembeli (pichani) alisema amechukua uamuzi huo kutokana na rafu inayoendelea jimboni humo na maneno ya baadhi ya wanachama, wakiwemo viongozi kuwa hatakiwi na vigogo ndani ya CCM.
 
Lembeli, mmoja wa wabunge waliokuwa mstari wa mbele wakati wa kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, alisema sababu za kutotakiwa huko zinatokana na dhana potofu ya baadhi ya viongozi kwamba michango yake ndani na nje ya Bunge inaivua nguo Serikali.
 
“Tangu mchakato wa uchukuaji wa fomu umeanza baadhi ya wanachama wengi tu wameitwa kwenye vikao visivyo halali karibu kata zote wakiwa na kadi zao na kuorodheshwa na kupewa maagizo ya kunikataa kwenye kura ya maoni na wengine wanapewa Sh5,000,” alisema
 
Lembeli alidai kuwa mbaya zaidi ni kwamba zipo kadi mpya za CCM zinazotolewa kiholela bila kufuata utaratibu na licha ya kulalamikia hali hiyo hakuna hatua zilizochukuliwa.
 
Alisema kutokana na yote hayo, aliwahi kusema kwenye mkutano wa hadhara kuwa kuna njama hizo, lakini badala ya CCM kufanyia kazi madai hayo, wakamuita mbele ya Kamati ya Maadili.
 
“Kwenye kamati ya maadili nilituhumiwa kuwa nakidhalilisha chama na kutakiwa niwataje nani walioniambia sitakiwi. Niliwajibu, tena kwa maandishi na kuwapa orodha, lakini mpaka leo kimya ina maana mimi bado ni mtuhumiwa,” alidai.
 
“Mimi siyo mtoto mdogo. Naelewa nini kinaendelea na ndiyo maana nimesema sitachukua fomu ya kugombea ubunge kwa mazingira haya. Bado sijatangaza kuhama CCM”.
 
Wakati Lembeli akisisitiza suala la kuhama kwake ni fununu tu, habari nyingine zilidai huenda akagombea ubunge kwa tiketi ya Chadema kutokana na kutokubaliana na mchakato huo anaodai ni batili.
 
Lembeli anaonekana kuwa mwiba ndani ya Serikali ya CCM baada ya kuiongoza Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ya Bunge katika uchunguzi wa uendeshaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili na kuibuka na taarifa iliyoonyesha kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
 
Mawaziri hao ni Balozi Hamis Kagasheki, Dk. David Mathayo, Dk. Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na Ezekiel Maige.
 
Lembeli pia nusura ajikute nje ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2010 wakati alipopigiwa simu na katibu mkuu wa CCM wa wakati huo, akiambiwa achukue fomu za kuwania ubunge wa jimbo jipya la Ushetu.
 
Wakati huo, Lembeli alidokezwa siku ya mwisho na ofisa mmoja wa Tume ya Uchaguzi kuwa hakukuwapo na jimbo hilo na kulazimika kufanya jitihada katika muda mfupi kuchukua fomu kwenye Jimbo la Kahama na kufanikiwa kushinda kiti hicho.
 
Hivi karibuni, Lembeli alitofautiana na taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ya kuwasafisha mawaziri na katibu wa wizara waliowajibika kutokana na kashfa ya escrow na Operesheni Tokomeza.
 
Lembeli alisema kitendo cha kuwasafisha viongozi hao ni kuipeleka nchi gizani.
 
“Yuko hapa (waziri mkuu wa zamani, Edward)Lowassa. Japo mimi sipendi wizi na ufisadi, katika kashfa ya Richmond nilikuwa mmoja wa waliopiga kelele awajibike. Lakini wengine wamesafishwa, kwanini naye asisafishwe,” alisema baada ya taarifa hiyo ya Ikulu.
 
“Kama ni kusafishana tusafishwe wote, tuanze upya ndipo nchi hii itatawalika, vinginevyo huko mbele kuna giza nene.”