NAFDA

NAMFUA FLAG DEVELOPMENT ASSOCIATION.

Friday, November 6, 2015

Shubiri mwitu tiba ya magonjwa ya kuku
         
Kuku ni moja ya miradi inayofanywa kwa wingi na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo wakulima na wafugaji, na wanaofanya shughuli nyinginezo.


Moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili na kuzungumziwa mara kwa mara ni magonjwa yanayoshambulia kuku, bila wafugaji kufahamu ni nini cha kufanya.


Kumekuwepo na njia mbalimbali za kutibu kuku, zikiwemo za asili na zisizokuwa za asili. Moja wapo ya tiba rahisi ya asili kwa kuku ni kwa kutumia shubiri mwitu maarufu kama Aloe Vera. Mmea ambao umekuwa ukisifika kwa kutibu magonjwa mbalimbali kwa binadamu, wanyama na ndege.
Shubiri mwitu mbali na kutibu kuku, hutumika pia kwa wanyama na binadamu
Shubiri mwitu mbali na kutibu kuku, hutumika pia kwa wanyama na binadamu

Shubiri mwitu (Aloe) imekuwa ikitumika kwa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na mifugo. Mmea huu unatumika sasa kutengeneza sabuni, dawa za binadamu na wanyama na mambo mengine mengi. Kwa sababu ya madawa mengi ya kiwandani kushindwa kutibu baadhi ya magonjwa kwa sababu wadudu wametengeza ukinzani, ipo haja kubwa ya kuweka mkazo kwenye madawa ya asili yatokanayo na mimea. Mmea wa aloe vera unauwezo wa kutibu magonjwa ya kuku hasa mharo mwekundu na kwa kiasi fulani mdondo-Newcastle disease.


Tafiti zilizofanyika kwa kutmia mti huu kutibu ugonjwa wa mharo mwekundu-coccidiosis ambao unamadhara makubwa kwa wafugaji wa kuku zinaonesha kuwa mti huu unaweza kutumiwa kama mbadala wa dawa za viwandani. Maji maji ya mmea huu yana uwezo wa kutibu magonjwa na kuponyesha majeraha yanayotokana na maambukizi ya magonjwa pamoja na kupandisha kinga ya kuku kwa asilimia 50 dhidi ya maonjwa mbalimbali.
 

Kupanda
Mmea wa Aloe vera unaweza kupandwa maeneo ya karibu na mabanda ya kuku ili kurahisisha upatikanaji wake na unakubali maeneo karibu yote.
 

Shubiri mwitu kwa ukuaji wa kuku
Shubiri mwitu inapowekwa kwenye maji inasaidia kwa kiasi kikubwa kuku kukua haraka. Mililita 15 had 20 za maji ya shubiri mwitu yakichanganywa na lita tano za maji kila siku kwa kuku 90 yana uwezo wa kusaidia ukuaji wa kuku na kuongeza uzito ukilinganisha na wale ambao hawajapewa.
 

Uandaaji wa Shubiri mwitu Kunywa
Shubiri mwitu (moja) inaweza kukatwe vipande vipande na kulowekwa ndani ya maji ya kunywa kiasi cha lita 1-hadi 3 kutegemeana na idadi ya kuku. Viache vipande hivyo kwenye maji kwa siku kadhaa hadi unapobadilisha maji ndipo uviweke vingine. Ukiweza kuchuja mchuzi wa shubiri mwitu basi unakuwa ukitumia mililita 15 ndani ya lita tano ya maji ya kunywa kuku kwa kuku 90 kama una kuku wachache basi punguza kiasi cha dawa au ongeza kama ni wengi.


Vidonda
Kuku wenye vidonda kama ilivyo kwa ugonjwa wa mdondo (Newcastle Disease) inakubidi utengeneze unga. Kata vipande vidovidogo vya shubiri mwitu kisha changanya na pumba kidogo, vitwange na kuvichekecha ili upate unga laini.


Anika na kisha tunza vizuri tayari kwa kuutumia mara kuku wauguapo. Kuku wenye vidonda waoshwe vizuri kwa maji safi na sabuni pamoja na chumvi kidogo. Baada ya hapo paka unga wa shubiri kwenye vidonda hivyo.


Njia hii ya asili ni nzuri na muhimu sana kwa utunzaji wa kuku, kwa kuwan hupunguza uwezekano wa matumizian ya madawa makali ya viwandani ambayo yana madhara kwa walaji na mazingira.

Tuesday, September 22, 2015






KILIMO BORA CHA MTAMA
Mtama ni kundi la mbegu ndogo aina ya mazao ya nafaka au nafaka ambayo kwa jina la kisayansi unajulikana kama (Sorghum bicolor), ni mazao yanayolimwa sana duniani kote kwa ajili ya chakula na lishe Mtama hutoa mazao mengi hata kwenye hali ambayo haifai kwa kilimo cha aina nyingine za mazao ya nafaka. Mtama una uwezo mkubwa wa kustahimili ukame.

Mtama unaweza kutumika kwa kuchemshwa na kuliwa kama ulivyo, kusagwa na kutumika kwa uji, kutengenezea vinywaji kama vile bia, kuoka mikate, na aina nyinginezo za vitafunwa. Mmea wa mtama pia hutumika kwa ajili ya malisho ya mifugo kama vile hay  na sileji. Mtama unastawis vizuri kwenye mazingira yenye wastani wa milimita 400 – 700 za mvua kwa mwaka. Pia mtama unavumilia sehemu zinazotuhamisha maji, na unaweza kulimwa sehemu zenye mvua nyingi.

Mtaama unafaa pia kwa sehemu kame zenye wastani wa joto la chini kiasi cha nyuzi joto 18°C, ili kuweza kuota vizuri, na kiasi cha nyuzi joto 25-30°C ili kukua vizuri. Mtama hauwezi kuvumilia barafu. Mtama unaweza kukua kwenye aina zote za udongo. Kwa kiasi kikubwa unafaa zaidi kwenye udongo wa mfinyanzi, lakini pia kwenye udongo ambao una kiasi kidogo cha mchanganyiko wa kichanga. Mtama unaweza kuvumilia uchachu kwenye udongo kuanzia pH 5.0-8.5, na inavumilia udongo wenye chumvi kuliko yalivyo mahindi.

Aina za mtama

Kwa jumla kuna aina zaidi ya 30 za mtama zinazolimwa kama chakula. Mtama hustawi vizuri kwenye joto ikivumilia pia ukame. Hivyo ni nafaka muhimi kwenye maeneo yabisi za Afrika. Katika miaka ya nyuma kilimo chake kiliachwa mara nyingi kwa ajili ya mahindi kwa sababu mahindi huleta mazao makubwa zaidi kwa ekari. Lakini wakati wa ukame mahindi ni hasara na watu hurudi-rudi kwenye kilimo cha mtama.

Aina za mtama zinatofautiana kulingana na rangi zake, kuna nyeupe, nyekundu, na kahawia. Mbegu za asili huwa zinachavushwa kwa urahisi zaidi lakini mavuno yake huwa ni hafifu ukilinganisha na mbegu za kisasa. Hata hivyo, aina za kisasa zinazalishwa kwa gharama nafuu zaidi zinapopandwa kwa kufuata kanuni za kilimo bora.

Serena:  Ina punje za kahawia. Aina hii hustawi kwenye eneo lenye mvua za wastani na hukomaa katika kipindi cha siku 110. Aina hii huwa na shina na mizizi imara, ambapo huweza kuzalisha kiasi cha kilo 3,000 kwa hekari moja. Ambapo zinahitajika kilo 5 za mbegu kwa hekari moja. Aina hii ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa milia, kutu, na madoa ya kahawia kwenye majani.

Seredo:  Hii ni aina nyingine yenye punje za kahawia, na inapendekezwa Kulimwa kwenye eneo lenye mwinuko wa mita 1,500 kutoka usawa wa bahari. Aina hii huchanua baada ya siku 71 na hukomaa katika kipindi cha siku 120. Aina hii huwa ni ndefu, na ina uwezo wa kuzalisha kilo 5000 kwa hekari moja. Ina uwezo wa kukabiliana na ugonjwa wa milia, kutu, mabaka kwenye majani, na madoa ya kahawia kwenye majani.

Gadam: Inafanya vizuri katika sehemu ambazo si kame sana. Katika nchi nyingi mfano Kenya, aina hii ya mtama hutumika kutengenezea bia na pia kwa chakula. Aina hii huvumilia bungo na ugonjwa wa majani.

Hakika na Wahi:  Hizi ni aina mbili za mtama ambazo zimezalishwa na kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga kwa ajili ya kuoteshwa kwenye mashamba yalioathiriwa na viduha. Mbegu hizi zina rangi ya manjano iliyopauka. Unga wa aina zote mbili zinafaa sana kwa kupika ugali.

Utayarishaji wa shamba na kupanda

Kwa kawaida mtama hupandwa kwa kutumia mbegu. Mbegu hupandwa shambani moja kwa moja baada ya shamba kuandaliwa, lakini pia zinaweza kurushwa shambani, kasha zikavurugwa pamoja na udongo. Unapaswa kutayarisha shamba la kupanda mtama, iwe ni kwa ajili ya malisho au chakula kabla mvua za msimu hazijaanza. Zao hili hufanya vizuri zaidi kwenye udongo ulio laini. Linaweza pia kupandwa kwenye udongo ambao haukulimwa vizuri na bado ukaota vizuri.

Nafasi:  Mtama unaopandwa kwa ajili ya malisho, unaweza kupandwa kwa nafasi ya sentimita 75×10. Aina za mtama ambazo zinalengwa kwa ajili ya lishe kwa binadamu na wanyama, zinahitaji nafasi kiasi cha sentimita 60×20. Nafasi hutoa mwanya wa kuwa na kiwango kikubwa cha malisho. Mkulima anaweza kupanda mbegu za mtama kiasi cha kilo 2.4-3.3 kwa hekari moja. Ni mara chache sana mbegu hupandwa kwenye vitalu na kuhamishiwa shambani baadaye.

Kupanda:  Mtama hupandwa mvua zinapoanza kunyesha. Mbegu ni lazima zifukiwe ardhini usawa wa sentimita 3 kwenda chini, hii itasaidia kuepuka kuota wakati ambao si msimu kamili wa mvua. Pia zinaweza kufukiwa kiasi cha sentimita 2 wakati ardhi inapokuwa na unyevu. Mtama unahitaji rutuba ya hali ya juu wakati wa kupanda na wakati wa kuota. Ni vizuri kutumia samadi au mboji iliyooza vizuri wakati wa kuandaa shamba.

Mseto:  Unaweza kupanda mtama mseto na mazao jamii ya mikunde, na kuongeza mboji shambani mwako. Hii inaweza kuwa njia nzuri zaidi ya kupata virutubisho vinavyohitajika. Mseto wa mazao jamii ya mikunde inashauriwa iwe ni kama vile maharagwe, kunde, n.k

Uangalizi na utunzaji
Ni lazima kung’oa baadhi ya mimea inapokuwa na urefu wa sentimita 30, au siku 30 baada ya kupanda, ili kuwa na uhakika wa nafasi ya sentimita 10 kati ya mstari na mstari kwa mtama unaokusudiwa kwa ajili ya malisho, na nafasi ya sentimita 20 kati ya mstari kwa mtama uliokusudiwa kwa ajili ya chakula na lishe ya mifugo.

Palizi ya mkono ifanyike walau mara mbili. Shamba la mtama ni lazima liwekwe katika hali ya usafi na kutokuruhusu magugu wakati wote hasa katika kipindi cha mwanzoni




Bofya hapa chini kuona maswali na majibu yaliyokwisha jibiwahttp://ushaurikilimo.org/maswalimajibu.php

Sunday, August 23, 2015

Serikali yamiliki kiwanda cha general tyre kwa asilimia 100

indexx
………………………………………….
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kumiliki kiwanda cha kutengeneze magurudumu ya magari cha General Tyre kwa asilimia 100 baada ya kununua hisa 26zenye thamani ya Dola Moja milioni kutoka kwa kampuni ya Continental AG.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Msajili wa Hazina wakati wa makabidhiano ya nyaraka za ununuzi wa hisa hizo Katibu Mkuu Kiongozi ,Balozi.Ombeni Semfue anasema jitihada za kuhakikisha kuwa serikali inamiliki hisa hizo zilianza tangu mwaka 2012 kwa kufanya mazungumzo ya awali na mwekezaji.
“Kufuatia hatua hii ya kuweza kumiliki hisa kwa asilimia 100 sasa tutakuwa na fursa ya kuzalisha magurudumu yetu wenyewe na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kilichokuwa kikitumia kununua magurudumu kutoka nje” alisema Balozi.Semfue.
Aidha anaendelea kufafanua kuwa hatua itakayofuata ni kutamfuata mwekezaji atakayeshirikiana na Shirika la Maendelao la Taifa (NDC) katika kuzalisha magurudumu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Balozi.Semfue anampongeza Rais Mhe. Jakaya Kikwete kwa kufanikisha zoezi zima la kuhakikisha serikali inamiliki hisa za kiwanda cha General Tyre kwa asilimia 100 na hivyo kufufua uchumi wa jiji la Arusha na Taifa kwa ujumla.
Naye Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru anasema mpaka serikali kuweza kumiliki hisa hizo ni hatua kubwa sana kutokana na vikwazo mbalimbali vilivyokuwa vikiwekwa na mwekezaji wa kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1969.
“Haikuwa kazi rahisi kumiliki hisa hizi bila ya jitihada kubwa iliyofanywa na serikali katika kumshawishi mwekezaji baada ya kuona hana kuwa hakuwa tayari kuwekeza na hivyo kurejesha umiliki kwetu” alisema Mafuru.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe. Uledi Musa, anaeleza kuwa kiwanda hicho kitatoa fursa za ajira zaidi kitakapoanza kuzalisha tofauti na awali ambapo kiliweza kuajiri wafanyakazi 360

Saturday, August 22, 2015


UFUGAJI WA NYUKI .

Tokea zama za kale binadamu wamekuwa wakitafuta

asali inayozalishwa na nyuki. Kwa azma hiyo shughuli

yoyote ya ufugaji nyuki ni kuendeleza zaidi ufanisi wa

haya.

Binadamu na nyuki hutegemeana. Kwani kwa upande

wa nyuki badala ya kuwindwa na kuuawa kwa ajili ya

asali yao hutunzwa na kulindwa. Matokeo ya haya

siyo tu kupatikana kwa asali na nta bali pia

kutambuliwa kwa nyuki kama rasilimali muhimu ya

kuhifadhiwa kulindwa na kustawishwa.

Ukusanyaji wa asali na nta ni shughuli ya kijadi katika

karibu bara lote la Afrika. Wafugaji nyuki wa jadi

hutumia mizinga rahisi ambayo njia ya uvunaji asali

huluta maangamizo ya makundi ya nyuki.

Kwa hiyo iko haja ya kubadilisha njia hii kali ya ufugaji

nyuki na kuanzisha ufugaji nyuki mzuri wenye ufanisi

zaidi. Huu ni ufugaji wa kutumia mizinga ya

masanduku yenye viunzi vya juu au masanduku yenye

fremu.

Shughuli yenyewe inaweza ikawa ni mradi wa

kiwango kidogo ambao unaweza kuendeshwa kirahisi.

Nyuki wanasaidia kuchavusha mimea ya asili na ile ya

kilimo na biashara. Mizinga haichukui eneo lolote la

ardhi na haitegemei pembejeo kutoka nchi za nje.

Yeyote anaweza akaanza ufugaji nyuki na familia

nzima ikaweza kushirikishwa. Njia nzuri ya kujifunza

juu ya ufugaji nyuki ni kufanya kwa vitendo.

Mradi wa Usimamizi wa Mazingira Rufiji (MUMARU) UFUGAJI NYUKI



1.0 SIFA ZIFAAZO KWA MAENEO YA

KUFUGIA NYUKI (MANZUKI)

Eneo lifaalo kwa shughuli za ufugaji nyuki ni lazima liwe na

sifa zifuatazo:

(i) Miti, uoto wowote wa asili na mimea mbalimbali

kwa mfano mazao ya chakula na biashara.

(ii) Maji ya kudumu ambayo hutumika kama sehemu

ya chakula cha jamii nzima ya kundi la nyuki. Pia

maji hutumika kwa kurekebisha hali ya hewa ndani

ya mzinga.

(iii) Eneo la shamba la nyuki ni lazima liwe ni salama

kwa mizinga, mazao yake, mifugo, binadamu, na

mahali ambapo maadui wa nyuki hawapo au

wanaweza kudhibitiwa.

(iv) Kivuli cha kadri na kinga ya upepo ili kuwapunguzia

nyuki kazi kubwa ya ubebaji maji kwa ajili ya

kupunguza joto. Inafaa kufugia nyuki ndani ya

nyumba iliyoandaliwa kwa ajili ya ufugaji wa nyuki

(bee-house)

Mawasiliano ya barabara ni muhimu yawepo ili kurahisisha

uhudumiaji wa makundi ya nyuki pamoja na mazao yake

hadi kufikia sokoni.

2.0 MIZINGA YA NYUKI

Makazi ya asili ya nyuki ni:

(i) Mashimo km vichuguu.

(ii) Mapango ya miti.

(iii) Chini ya matawi ya miti.

Baada ya binadamu kuona kazi ya kuwinda viota vya nyuki

inachosha kwa kutembea mwendo mrefu msituni, hatari ya

wanyama wakali ndipo hatimaye nyuki wakatengwa karibu

na sehemu wanazoishi binadamu kwa kuwaandalia

mizinga.

2.1 MIZINGA YA JADI

Mizinga ya jadi ipo ya aina nyingi kwa mfano mizinga ya

magogo, magome, vikapu, vyungu, matete na kadhalika.

Aina ya mizinga inayotumika hutegemeana na mazingira

ya maeneo. Kwa kawaida mizinga ya jadi / asili huwa na

masega yasiyohamishika.

Mradi wa Usimamizi wa Mazingira Rufiji (MUMARU) UFUGAJI NYUKI



2.1.1 MIZINGA YA MAGOME

Mizinga ya magome hutengenezwa kutokana na magome

ya miti ya miombo ya aina mbili:

(i) Mzinga ambao sehemu ya nje huwa upande

wa ndani.

(ii) Mzinga ambao sehemu ya nje huwa nje ya

mzinga.

Ili kutengeneza mzinga wa gome mfugaji huenda msituni

na kutafuta gome lifaalo kwa kutengeneza mzinga.

Apatapo gome lifaalo hukata sehemu ya juu na chini

kuzunguka mti katika urefu anaohitaji. Gome hukatwa

mkato wa wima kwa panga au shoka na baadaye

huimarishwa kwa vigingi tayari kwa kutundikwa juu ya mti

baada ya kuweka chambo.

Picha ya mzinga wa gome na unavyotundikwa

Mradi wa Usimamizi wa Mazingira Rufiji (MUMARU) UFUGAJI NYUKI



2.1.2 MZINGA WA GOGO

Mzinga aina hii hutayarishwa kutokana na gogo la mti

lililoandaliwa kutokana na mahitaji ya mfugaji nyuki. Gogo

hupasuliwa vipande viwili na kuondolewa nyama ya ndani.

Kisha hufunikwa tayari kwa kutundika baada ya kuweka

kivutia nyuki / chambo.

Aina nyingine ya mzinga wa gogo ni gogo lililotobolewa na

kuachwa wazi ndani. Kisha hufunikwa pande zote na

mifuniko ya miti. Mfuniko wa upande mmoja huwekwa

mashimo kwa ajili ya nyuki kutoka na kuingia ndani ya

mzinga.

Picha za mizinga ya magogo na inavyotundikwa

Mradi wa Usimamizi wa Mazingira Rufiji (MUMARU) UFUGAJI NYUKI



2.1.3 MZINGA WA KIBUYU

Mzinga aina hii huandaliwa kutokana na matumizi ya

vibuyu vyenye nafasi ya ndani kubwa (vibuyu vikubwa

vyenye kipenyo cha sentimita 45 au zaidi).

Mlango wa kuingilia na kutoka nyuki na mlango kwa ajili

ya kupakulia asali ni kama picha inavyoovyesha hapa

chini.

Picha ya mzinga wa kibuyu na unavyotundikwa

2.1.4 MZINGA WA CHUNGU

Vyungu pia hutumika kama mzinga kwa ajili ya kufugia

nyuki. Ukubwa wa chungu ndio wingi wa uzalishaji wa

mazao ya nyuki.

Picha ya mzinga wa chungu na unavyotundikwa

Mradi wa Usimamizi wa Mazingira Rufiji (MUMARU) UFUGAJI NYUKI



2.1.5 FAIDA NA HASARA ZA MIZINGA YA KIASILI

(ya jadi)

(i) FAIDA ZA MIZINGA YA KIASILI

(a) Mizinga ya kiasili ni rahisi kutengeneza na

inahitaji mtaji mdogo.

(b) Mizinga ya kiasili haihitaji ufundi mkubwa

kutoka kwa wataalamu.

(c) Mizinga ya aina hii haihitaji mali ghafi

kutoka viwandani.

(ii) HASARA ZA MATUMIZI YA MIZINGA YA JADI

(a) Miti yenye manufaa kiuchumi huharibiwa

kwa kukobolewa na kukatwa.

(b) Uvunaji asali na ukaguzi wa mizinga

(makundi) huwa mgumu na hupoteza muda

mwingi.

(c) Mizinga hasa ya magome hudumu kwa

muda mfupi. Kila ikichakaa mfugaji nyuki

anatumia muda mwingi kuandaa mizinga

mingine mipya.

2.2 MIZINGA YA MASANDUKU

2.2.1 MZINGA WA KATI

Mzinga wa kati ni wenye gharama nafuu na ni rahisi.

Unawawezesha wafugaji nyuki katika nchi za joto

kuwamudu nyuki wao katika njia yenye ufanisi zaidi kuliko

wanapotumia mizinga ya kiasili.

(i) FAIDA NA MATUMIZI YA MZINGA WA KATI

1. Katika utengenezaji vipimo sahihi huhitajika katika

viunzi. Vipimo vingine sio muhimu sana. Mizinga

inaweza kutengenezwa kwa zana rahisi.

2. Ukubwa wa mzinga unaweza ukatofautiana ili uendane

na hali halisi ya eneo la ufugaji.

3. Kila sega hufikiwa bila ya kuondoa masega mengine.

Mbinu hii ya kushughulikia kiunzi kimoja baada ya

kingine husababisha bughudha kidogo kwa kundi la

nyuki.

4. Hakuna uvunaji unaohitajika isipokuwa ule wa masega.

Hivyo mzinga aina hii unaweza kuendeshwa na

wafugaji wasioweza kuinua vitu vizito.

5. Iwapo kuna maadui (wanyama waharibifu) mzinga

unaweza kuning’inizwa kwa waya mbali na ardhi.

6. Aina hii ya mizinga kiuchumi humnufaisha mfugaji

nyuki kupata ongezeko la mazao ya nyuki.

Friday, August 21, 2015

JE NI WAJIBU MWANAMKE KUMTUNZA MWANAUME KISHERIA?.
Na  Bashir  Yakub.
Kisheria  ndoa inapokuwa  imefungwa   kuna  haki  za  msingi  ambazo  huibuka.  Hizi  huitwa  haki  za  moja  kwa  moja  ( automatic  right). Huitwa  haki  za  moja  kwa  moja   kwakuwa   hazina  uhiari  katika  kutekelezwa  kwake.  Kuwapo  kwa  ndoa  ndio  kuwapo  kwake  na  hivyo  haihitaji  mtu  kuziomba. Kimsingi  haki  hizi  zipo  nyingi  ambapo  tutaona  baadhi  yake hapa   huku  makala  yakijikita  katika   haki  moja ya  matunzo  kwa  wanandoa.

1.BAADHI  YA  HAKI  ZINAZOIBULIWA  NA  NDOA.
( a ) Haki  ya  tendo  la  ndoa.  Hii  ni  haki  ya  lazima  kwa  wanandoa  na  kutokuwepo  kwake  kunaweza  kubatilisha  ndoa iwapo  mmoja  wa  wanandoa ataamua  kufanya  hivyo. Ni  haki  ambayo  huchukuliwa  kama  ndio ndoa yenyewe  na  hivyo  kuifanya  kuwa  na  umuhimu wa pekee.

( b ) Haki  ya  kutumia  jina la mume. Hii   ni haki  aliyonayo  mwanamke  ambapo  anaruhusiwa kutumia  jina  la  mme  wake  badala  ya  lile  la  baba  yake. Hata  hivyo  sheria  haikueleza  iwapo  mwanaume  naye  anaweza  kutumia  jina  la  mke  wake,  au  la  baba  wa  mke  wake, au la  ukoo  wa  mke  wake.  Pia si  tu  mwanamke  ameruhusiwa  kutumia  jina  la  mme  wake  isipokuwa  hata  lile  la  ukoo  wa  mme  wake.

( c ) Haki  ya  kutumia  mali  za  familia  kwa  pamoja. Haijalishi  mali  hizo  ni  mwanamke  mwanaume  ataruhusiwa  kutumia na  haijalishi  mali  hizo ni  za  mwanaume  mwanamke  ataruhusiwa  kutumia. Isipokuwa  yawe  matumizi  ambayo  hayako  kinyume  cha  sheria.

( d ) Haki  ya  kutunza  watoto/mtoto kama  yupo. Ikiwa  familia  imebarikiwa  na  mtoto/watoto basi  wanadoa  kwa  pamoja  wanawajibika  kuwatunza  watoto  hao  kila  mtu kwa  nafasi  yake. Hii  ina  maana mwanamke  anawajibika  zaidi  kuwa  mwangalizi  mkuu wa  kila  siku  wa  watoto  huku  mwanaume  akilazimika  kutoa  matumizi   hasa  yale ya  kifedha.

( e ) Haki  ya  kugawana  mali  pindi  ndoa  inapovunjika. Hii  huhusisha  mali    zote  ambazo  huitwa  mali  za  machumo  ya  pamoja  baina  ya  mwanamke na  mwanaume.

( f ) Pia  ipo  haki  ya  kurithi  na  kurithiana  iwapo  kuna  kifo  cha  mmoja  wa  wanandoa. Mwanamke  aweza  kurithi  mali  za  mme  wake  halikadhalika  mwanaume. Hii  huenda  mpaka  kwa  watoto  waliopatikana  katika  ndoa  ambapo   huweza  kurithi  mali  za  baba, mama  au  wote  wawili.

( g ) Haki  ya  matunzo  baina  ya  wanandoa.  Hii  ndiyo  itakayojadiliwa  japo  kwa  ufupi .

2.  MWANAUME  KUMTUNZA  MWANAMKE.
Sura  ya  29  ya  Sheria  ya  ndoa  kifungu  cha  63 ( a )  kinasema  kuwa  ni  wajibu  wa  kila  mwanaume  kumtumza  mke/wake zake  kutokana  na  njia  za  kipato  chake.  Neno  njia  za kipato  chake  maana  yake  ni  namna  anavyopata   kipato  ndivyo  atavyotakiwa  kutoa  matunzo  kwa  mwanamke.  Haiwi  kuwa  mwanaume  anapata  kipato  kidogo  halafu  alazimishwe  kutoa   matunzo  makubwa.  Ushahidi  wa  namna  anavyopata  kipato  chake  ndio  utakaoainisha  kiasi  cha  matunzo  kwa  mke  wake.

Aidha kwa  mujibu  wa  kifungu  hicho  matunzo  yanayoongelewa  hapa  yanahusisha   makazi,  mavazi, chakula  na  huduma  nyingine  kama  za afya  n.k. Kitu  cha  msingi  hapa  ni  kuwa  ni  lazima  kwa  mwanaume  kutoa  vitu  hivi  kwa mke  wake.

3.  MWANAMKE  KUMTUNZA  MWANAUME.
Kifungu  hichohicho  cha  63 ( b ) kinasema  kuwa  utakuwa  ni  wajibu  wa  kila  mwanamke  lakini  mwenye  uwezo  kutoa  matunzo  kwa   mume  wake  iwapo  mume  huyo  ana  ulemavu/hajiwezi  jumla  au  sehemu  ya  mwili  wake, kiakili  au  kimwili  na  hivyo  kutokuwa  na  uwezo  wa  kuingiza  kipato  kutokana  na  hali  hiyo.

Kwa  kifungu  hiki  tunaona  kuwa mwanamke  anao  wajibu  wa  kumtunza  mume  wake   lakini  iwapo  tu kwanza  ana  uwezo, pili mwanaume  awe  na  tatizo  ambalo  kwalo  hawezi  kuingiza  kipato  na  tatizo  hilo  liwe la  kimwili  au  kiakili. Kumbe  basi  tunaona  kuwa mwanaume  kumhudumia  mwanamke ni  lazima  hata  mwanamke  awe  mzima  wa  afya  huku   hafanyi  kazi  wakati  mwanamke  kumhudumia  mwanaume  ni  pale  tu  atapokuwa  ana  tatizo  ambalo  linamfanya  asiweze  kufanya  kazi. Lakini  pia  sheria  imesema  mwanamke  atatoa  huduma  iwapo  ana  uwezo wakati  neno  iwapo  ana  uwezo  haikuliwekwa  kwa  mwanaume.Kwa mwanaume  kutoa  ni  kutoa  tu.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

Thursday, August 20, 2015


KILA ALIYEJIANDIKISHA ANA WAJIBU WA KUPIGA KURA

Jaji Mstaafu, Damian Lubuva.
Kwanza nimshukuru Mungu kwa kuweza kutupa uhai leo na kujiona tuko katika nchi yetu iliyojaa amani.
Naamini kwamba katika maeneo yote ya nchi, wazalendo wa nchi hii walijitokeza bila kulazimishwa kwenda kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (BVR)kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Mkoa wa mwisho kuhitimisha rasmi kazi hiyo iliyoanza kwa kusuasua mwanzoni mwa mwaka huu ni Jiji la Dar es Salaam.Kabla ya uandikishaji, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilikuwa imekadiria kwamba mwaka huu kutakuwa na watu milioni 24 wenye sifa za kujiandikisha na hatimaye kushiriki katika uchaguzi huo wa kuwachagua madiwani, wabunge na rais.
Kwa dalili zinavyojionesha, idadi hiyo ya watu milioni 24 inaweza isifikiwe kwa sababu ya matatizo yaliyojitokeza wakati wa uandikishaji ambayo yaliwakatisha tamaa baadhi ya watu kutokana na usumbufu uliokuwepo.
Hata hivyo, kama idadi hiyo itakaribiwa, itakuwa si haba na jambo muhimu baada ya hapo ni waliojiandikisha kuhakikisha kila mmoja anapiga kura. Unapopiga kura ndipo unapoonesha uzalendo wako, kwani unasababisha kupatikana kwa kiongozi bora, usipopiga kura elewa kwamba unachangia kwa kiwango cha juu kusimika viongozi wasiofaa katika nchi hii yenye changamoto nyingi za maendeleo.
Nimesema hivyo kwa sababu kumeanza kutokea tatizo la watu kutotaka kupiga kura na badala yake kutumia zoezi la uandikishaji kupata vitambulisho tu, yaani ile kadi ya mpiga kura kugeuzwa kitambulisho.
Nilisikitika sana kuona katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, zaidi ya nusu ya waliojiandikisha kupiga kura hawakupiga kura, hii ilinisikitisha sana na kwa kweli yule ambaye hakupiga kura ajiambie katika nafsi yake kwamba hakuitendea haki nchi yetu.
Hili ni tatizo kwa sababu kila aliyejiandikisha anatakiwa kupiga kura. Kutopiga kura maana yake ni kuacha masuala muhimu ya nchi yaamuliwe na wachache badala ya walio wengi na ambao hawakupiga kura wakati walikuwa wamejiandikisha mwaka 2010 wajue kwamba walichangia kupata viongozi wabovu katika nchi hii.
Najua kwamba zoezi la uandikishaji wapiga kura ulikuwa na kasoro nyingi na za kukera kwa wananchi waliojitokeza. Baadhi ya matatizo hayo yalikuwa ya kujirudia kiasi kwamba wengine walianza kuhoji kama wahusika wanajifunza kutokana na mwenendo wa mchakato mzima wa uandikishaji.
Naamini kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi chini ya Jaji Mstaafu, Damian Lubuva na serikali kwa ujumla itakuwa imejifunza kutokana na mchakato huu na taifa litajiepusha na mkanganyiko kama huu kwenye chaguzi zijazo.
Binafsi nitafurahi kuona idadi kubwa ya waliojiandikisha kupiga kura wanafanya hivyo. Tunajua kuwa katika chaguzi nyingi duniani, si rahisi kwa watu wote waliojiandikisha kupiga kura wapate fursa ya kupiga kwa sababu tofauti.
Lakini, kama tunavyoona kwa jirani zetu wa Kenya, tunaweza walau kupata wapiga kura waliofika asilimia 75 ya waliojiandikisha.
Katika baadhi ya nchi za wenzetu, wako wananchi ambao husafiri kutoka Ulaya na Marekani kwa lengo la kuwahi kupiga kura nchini mwao, huo ni uzalendo ambao nasi tunatakiwa kuujenga.Watanzania hawawezi kuacha kupiga kura kwa sababu yoyote ile. Kama unataka kiongozi unayemtaka ashinde katika uchaguzi, unatakiwa kupiga kura.
Watu wengi wakipiga kura, hata uongozi unaoingia madarakani unakuwa na amani kwa vile unafahamu umeingia kwa mamlaka ya walio wengi. Ndani ya moyo wako weka dhamira kwamba ‘uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni lazima nipige kura’, vinginevyo wote watakaoacha kupiga kura wataonekana ni wasaliti wa nchi yao wasio wazalendo.
NEC YAWAOMBA VIONGOZI WA DINI KUTOKUWA NA UPANDE WAKATI WA KUWAELIMISHA WANANCHI KUHUSU UCHAGUZI MKUU UJAO.
 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji, Damian Lubuva akitoa mada leo jijini Dar es salaam kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali waliohudhuria mkutanoni .
 Baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria mkutano ulioandaliwa na NEC leo jijini Dar es salaam wakifuatilia mada iliyokuwa zikiendelea.
 Wanasekretarieti ya maandalizi ya mkutano NEC na wadau mbalimbali  na baadhi ya waandishi wakifuatilia mjadala kuhusu wajibu wa viongozi wa dini kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Jaji, Damian Lubuva akiteta jambo na mmoja  wa makamishna wa Tume hiyo Prof Amon Chaligha leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa NEC na wadau mbalimbali.
 Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akitoa mada kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi na hatua zilizofikiwa hadi sasa leo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa viongozi wa madhehebu ya dini.


MWANDISHI WETU -MAELEZO-DAR ES SALAAM

Tume ya Taifa ya uchaguzi  NEC  imewaomba viongozi wa dini zote kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wapiga kura bila kuonyesha hisia za kuegemea upande wowote wa mgombea  ili waweze kufanya maamuzi sahihi  wakati wa uchaguzi Mkuuu ujao.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti   wa NEC, Jaji Damian Lubuva kwenye Mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam uliowakutanisha wadau hao wa uchaguzi na kuwakumbusha wajibu wao katika jamii hususani katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu.

Alisema kuwa  taasisi za kidini zinaaswa kama walivyo wadau wengine katika kipindi hiki cha uchaguzi kuhubiri amani na kuendelea kutoa elimu kwa watanzania ili zoezi hili liishe kwa amani na kuwaacha watanzania wakiwa  na umoja na mshikamano licha ya tofauti za kiimani zilizopo miongoni mwao.

“Tume inawataka, nyinyi  viongozi wa dini, mnapotoa mafundisho ya uchaguzi kwa waumini wenu kuhakikisha hamuonyeshi hisia za kuwa upande wa chama chochote cha kisiasa na zaidi kuepuka kushawishi waumini wenu kuegema chama au mgombea fulani” amesema Jaji Lubuva.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo , Askofu Philemon Phiri wa kanisa la EAGT-Mikocheni -A ameiasa Tume  hiyo  kusimama katika haki, uhuru na kuhakikisha wanatangaza washindi bila kuonyesha upendeleo  ili kuivusha nchi ikiwa  salama.

Mshiriki mwingine kutoka Kanisa la Moravian Mchungaji Alamu Kajuna alisema kuwa amani ndiyo tunu kwa kila mwanadamu, hatutegemei vurugu wakati  huu wa uchaguzi maana amani inapotoweka wanaoumia ni wananchi wakiwamo waumini wao hivyo wao kama taasisi zinazoshirikiana na wananchi kwa karibu kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili tupate viongozi kwa amani

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekutano na viongozi hao na wadau wengine ikiwa zimebaki siku mbili kuanza kwa kampeni hapo Jumamosi ijayo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.